Hakuna viwanja vya wahamaji Kipawa


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version

SERIKALI mkoani Dar es Salaam imeumbuka. Haina ardhi ya kuwagawia wakazi wa Kipawa kwani viwanja 400 ilivyosema vimepimwa eneo la Pugu, vina wenyewe.

Wakazi wa Kipawa waliozuiwa kwa miaka 12 kuendeleza makazi yao, kuanzia 15 Oktoba walipewa siku 45 za kuhama ili kupisha kazi ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.

Tarehe hiyo pia serikali ilianza kutoa hundi za malipo ya fidia kwa wakazi hao licha ya upinzani mkali uliotokana na msimamo wa kupinga malipo ya fidia yanayozingatia Sheria ya Ardhi ya mwaka 1967.

Wanataka malipo yaanzie 1997 ilipofanyika tathmini ya mali zao, hadi mwaka 2001 yazingatie sheria ya mwaka 1967. Malipo ya mwaka 2002 hadi sasa wanataka yazingatie sheria hiyo, kama ilivyorekebishwa mwaka 1999.

Katika kusisitiza msimamo huo, 12 Oktoba, 2009 wakazi hao waliipa serikali notisi ya siku 90 itii, vinginevyo, wataishitaki mahakamani. Notisi iliwasilishwa 12 Oktoba na inatarajiwa kumalizika 9 Januari mwakani.

Zoezi la kukabidhi viwanja nalo limekwama kwasababu hakuna viwanja vilivyo tayari kwa ajili ya wanaohama Kipawa.

Kitongoji cha Pugu Kimani, mtaa wa Pugu Kinyamwezi, kinachopakana na kitongoji cha Mgaule, Buyuni kinachoelezwa kuwa serikali ililipa fidia na kupima viwanja 400, kuna mgogoro wa ardhi.

Makabidhiano ya viwanja hivyo kati ya serikali na wakazi wa Kipawa yalishindikana baada ya wenyeji wa maeneo hayo kugoma wakisema, “tuna haki ya kutumia maeneo tunayomiliki kwa miaka mingi.”

Badala ya kukabidhi watu viwanja, serikali iliishia kuwaonyesha eneo lenye viwanja vyao. Kampuni binafsi ya Geoinformatics Consultants Limited iliwaeleza, “viwanja vyenu vipo eneo hili.”

Wananchi wakajibu,“Hukutuleta huku kutuonyesha eneo, utukabidhi viwanja ambavyo ofa tayari tunazo.” Haikuwezekana maana eneo lote lina makazi ya watu ambao wakati huo walikutwa wakisafisha kwa mapanga na majembe.

Serikali ya Mtaa wa Pugu Kinyamwezi inafahamu vizuri chimbuko la mgogoro wa ardhi katika eneo hilo. Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pia unatambua hilo, tangu enzi za uongozi Abbas Kandoro.

Wapo walioibuka na kujigawia maeneo kisha kuyauza kwa wanaoyamiliki. Hati za manunuzi ya maeneo hayo, zinathibitisha kwamba uvamizi huo unahusisha mtaa wa Buyuni.

Tatizo hilo lililochochewa na utamaduni wa baadhi ya viongozi kuchanganya siasa katika utendaji kazi za serikali. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Selemani Tsere, alipofika eneo hilo mwaka 2007, badala ya kuamuru wakazi wa Pugu Kimani waondoke, alisema, “Ninawaagiza muvune mazao yenu na msipande tena.”

Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara na wanakijiji wa Pugu Kinyamwezi na vitongoji vyake.

Wiki iliyopita, wakazi 200 wa kitongoji cha Mgaule, Pugu Mwakanga, walizuia ujenzi wa barabara iliyotakiwa kuanzia hapo katika maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya makazi mapya ya wahamiaji kutoka Kipawa.

Mgaule hawana tatizo na maendeleo yanayotarajiwa, wanalalamika kutoshirikishwa katika mipango hiyo. Hawajui hatima yao na mali zao.

Hoja ni kwamba serikali inapanga maendeleo bila kushirikisha walengwa. Katika maeneo mengine, inatuhumiwa kujumuisha katika ramani ya mipango miji, maeneo ya Pugu Kinyamwezi pasina maafikiano na wenyewe.

Baadhi wanasema hawajalipwa fidia lakini ardhi yao imepimwa viwanja na kugawiwa wakazi wa Kipawa. Hakuna anayejua hatima ya suala hili.

Ufuatiliaji wangu umebaini majina yasiyopungua 10 ambayo ardhi wanayomiliki iliingizwa kwenye ramani bila kuthaminiwa wala wao kushirikishwa, yapo ofisi za kampuni ya Majengo Estate Developers iliyofanya tathmini ya mali za Pugu Kinyamwezi.

Aidha wengine 16 walioshiriki uthamini na ardhi yao kupimwa viwanja na kugawiwa kwa wahamiaji kutoka Kipawa, hawajalipwa fidia, pia wanatambuliwa na kampuni hiyo.

Malipo yao yameandaliwa na inasemekana watalipwa mara baada ya wakazi wa Kipawa kulipwa fidia.

Chimbuko la mgogoro ni utendaji wa kudhania badala ya kuzingatia taratibu. Serikali inapanga bila kushirikisha wote wanaoguswa na maendeleo hayo.

Kilichobaki ni kuendeleza mabavu kama silaha ya mwisho ya serikali kujinasua katika lawama. Hakuna historia inayoonyesha kuwa mabavu hushinda umma.

0
No votes yet