Hamad kufukuzwa CUF


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version

ALIYEJIAPIZA kumng’oa Maalim Seif Shariff Hamad ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), sasa kufukuzwa uanachama, imefahamika.

Hamad Rashid Mohammed, mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba, ndiye amekuwa akisema anataka kuchukua nafasi ya katibu mkuu wa CUF kwa madai kwamba Maalim Seif ameshindwa uongozi, amedhoofisha chama na hana fikra mpya.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, taratibu za kumchukulia hatua Hamad pamoja na wenzake wanaopanga kumuengua Maalim Seif tayari zimeanza.

Hamad na wenzake wanaweza kuwa wameshafukuzwa kwenye chama hicho kabla ya 5 Februari mwaka kesho.

Habari zinasema maandalizi ya vikao vya kumfukuza Hamad na wenzake yalitarajiwa kuanza jana Jumanne (27 Desemba 2011), ambapo Hamad alitakiwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu na Maadili.

Hamad na wenzake wanasema tangu Maalim Seif ateuliwe kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), chama kimedhoofika hasa Tanzania Bara ambako kwa sasa CUF “kinaonekana kama tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Mawasiliano kati ya viongozi wakuu wa chama hicho ambayo yametawanywa jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili sasa yanasema, Hamad hawezi kusalimika.

Mawasiliano hayo kati ya Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho taifa, katibu mkuu Maalim Seif, Julius Mtatiro, naibu katibu mkuu Tanzania Bara na Khamisi Khassani, mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa CUF, yanaonyesha Hamad atafukuzwa wakati wowote kuanzia sasa na 5 Februari 2012.

Mbali na Hamad wengine wanaotajwa kuchukuliwa hatua au kufukuzwa, ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Khassani Doyo na mbunge wa zamani wa Micheweni, Pemba, Shoka Khamisi Juma.

Kwa mujibu wa mawasiliano hayo, tayari Maalim Seif ameagiza kuitwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya chama wale anaowaita, “Hamad na genge lake” ili wahojiwe.

Anasema mara baada ya kazi ya kuwahoji kukamilika, kamati ya maadili iwasilishe taarifa yake kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kuchukua hatua.

Akiandika kwa njia ya imeili kwa Profesa Lipumba, 14 Desemba 2011, saa 10:04 asubuhi, Maalim Seif anasema, “Tayari nimeshauriana na Makamu (Makamu mwenyekiti wa CUF, Khamis Machano Alli) na tumeona kuna haja ya jamaa yako (Hamad Rashid) na genge lake kuitwa katika kamati ya nidhamu na maadili kuhojiwa.”

Maalim anasema tayari ushahidi wa kutosha umekusanywa na idara ya usalama dhidi ya Hamad, Doyo na Shoka na kwamba sharti Hamad afukuzwe ndani ya chama hicho.

Anasema, “KUT ichukue uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uongozi vinara wao na wengine kupewa karipio,” anaeleza Maalim katika mawasiliano yake hayo na Profesa Lipumba.

Anasema, “KUT ifikishe taarifa yake katika kikao cha Februari 2012 mbele ya Baraza Kuu Taifa (BKUT) kwa uamuzi.” Anasema iwapo itaonekana kuna haja ya kuitishwa kwa mkutano wa dharula wa baraza kuu basi hilo lifanyike haraka iwezekanavyo.

Akisisitiza umuhimu wa Hamad Rashid na wenzake kufukuzwa ndani ya chama hicho, Maalim anasema amekubaliana na ushauri wa Profesa Lipumba wa kuwadhibiti kinidhamu viongozi hao.

Anasema wanachama walio wengi wa chama hicho “wanatudadisi kwa nini hatuchukui hatua?” Anasema, “Sasa ni kumuacha jamaa yako aendelee kufanya kazi aliyopewa na rafiki yake ya kukivuruga chama au chama kimvuruge yeye!”

Hata hivyo, Maalim Seif hajaeleza katika mawasiliano hayo, huyo anayeitwa “rafiki” wa Hamad Rashid aliyempa kazi ya kuivuruga CUF ni nani.

Bali MwanaHALISI limeona nyaraka iliyoandaliwa na idara ya usalama ya chama hicho, pamoja na baadhi ya mawasiliano kati ya Profesa Lipumba, Maalim Seif, Ismail Jussa, Juluis Mtatiro na Khamis Khassani, zikitaja waziri mkuu Mizengo Pinda na mahali pengine mbunge wa Monduli Edward Lowassa, kuwa ndiyo wanaompa nguvu Hamad kuvuruga CUF.

Akionekana kukerwa na tabia hiyo, Maalim anasema, “…leo jamaa yako (Hamad Rashid) kafikia hadi kukodi wahuni na wavuta bangi wanaokadiriwa kufikia 150 kuwahujumu BGs (kikosi cha ulinzi cha CUF)!”

Anasema, “Ikihitajika hata kikao cha dharura cha BKUT kiitishwe. Sisi tunahisi chama ki-act decisively, hasa dhidi ya jamaa yako. Yeye muono wetu tumfukuze kwenye chama na akiamua kwenda mahakamani na mahakama kutoa maamuzi ya kumpendelea yeye, mwache awe mbunge wa mahakama kama ilivyokuwa kwa akina Asha Ngede na Naila Majid Jidawi.”

“Ikishajulikana kuwa si mwanachama tena,” anasema Maalim, “atakuwa hana mashiko! Muache aende CCM (Chama Cha Mapinduzi) au CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) akawe mgombea mwenza!”

Awali akiandika kwa Profesa Lipumba, Maalim Seif anasema, “Nimefurahi kwa mahojiano yako na DW (kituo cha redio na Tv cha Ujerumani cha Deutsche Welle) kuwa ukatibu mkuu hautafutwi kwa mbinu za kimafia.

Anasema tayari Mtatiro ametahadharisha jeshi la polisi mkoani Tabora juu ya Hamad Rashid na wenzake. Maalim anasema Mtatiro ameeleza mkuu wa polisi wa mkoa wa Tabora (RPC) na mkuu wa polisi wa wilaya ya Urambo kuwa wanaokwenda mkoani mwao kufanya mikutano ya hadhara ndio waliosababisha fujo jijini Dar es Salaam.

Barua ya Mtatiro ya 15 Desemba 2011 kwenda kwa mkuu wa polisi wa mkoa wa Tabora, inatuhumu viongozi wawili waandamizi wa chama hicho, Khassani Doyo na Amir Kirungi, kuzunguka wilaya zote nchini bila kuzijulisha mamlaka za chama zilizowekwa kikatiba na kuhamasisha wanachama wake wakihame chama chao.

Hata hivyo, mpango wa Maalim Seif kutaka kufukuza wenzake kwenye chama unapingwa na mjumbe wa baraza hilo, Abubakari Rakesh. Katika mawasiliano yake na Profesa Lipumba, 14 Novemba 2011, Rakesh anasema ni bora Profesa Lipumba kuingilia kati mgogoro kati ya Hamad Rashid na Maalim Seif kuliko kuendekeza utamaduni wa kufukuzana.

Anasema, “…mimi ni kijana wa chama hiki wa muda mrefu…Maalim Seif ni katibu wangu mkuu na Hamad Rashid ni kiongozi wa chama ninayemheshimu sana...nakushauri uingilie kati mgogoro huu ili viongozi hawa waondoe tofauti zao, vinginevyo chama kinaelekea kubaya.”

Rakesh alikuwa anamweleza Profesa Lipumba jinsi anavyosakamwa kutokana na mchango wake alioutoa kwenye mkutano wa baraza kuu uliofanyika kwenye hotel ya Lamada, ambapo pamoja na mambo mengine, aliungana na baadhi ya wajumbe waliokuwa wamemtuhumu Maalim Seif kushindwa kutenda kazi zake Tanzania Bara.

Awali Mtatiro akiandika kwa Profesa Lipumba anasema, Doyo na Kirungi wameelekea mkoani Tabora kwa ziara ya kila wilaya; msisitizo wao uko kwenye jimbo la Urambo Magharibi ambako Kirungi aligombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na 2010.

Anasema, “Wanakwenda huko kufanya kampeni ya wazi ya mikutano ya hadhara na vikao vya ndani kwa lengo kubwa la kutoa notisi ya siku 30 kwa katibu mkuu (Maalim Seif) na mwenyekiti (Profesa Lipumba) wajiuzulu, vinginevyo ngome ya chama yote ihamie CHADEMA.”

Mtatiro anasema, “Tuhuma zao ni kuwa mwenyekiti, japokuwa anatokea Tabora, ameshindwa kabisa kukijenga chama na kuwa amepoteza mwelekeo na eti hata katika uchaguzi wa Igunga mwenzie Mbowe (Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA) alipigana wiki kadhaa, lakini mwenyekiti wetu amekimbilia nje ya nchi.”

Pili, Mtatiro anasema, Doyo na Kirungi wanadai kuwa katibu mkuu amepoteza mwelekeo na anaua chama Bara, kwa hivyo lazima waondolewe kwa notisi.”

Katika mawasiliano mengine, Maalim anamtuhumu mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwani kutaka kuhujumu ziara yake mkoani Lindi. Anasema Baruani alishawishi baadhi ya watu wasijitokeze kwenye mapokezi yake kwenye uwanja wa ndege wa Lindi.

Anasema, “Nasikia alipingwa vikali na mkutano ulifanikiwa sana. Bila kumtaja, wakati najibu risala yao niliwaeleza kuwa hakuna mgogoro katika chama, isipokuwa kuna mtu na wenziwe wanachochea ionekane kuna mgogoro, na nikaeleza yaliyotokea….”

Iwapo Hamad atafukuzwa CUF, atakuwa mbunge wa pili wa upinzani kuachia ubunge ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja tangu kumalizika uchaguzi mkuu. Mwingine aliyefukuzwa uwanachama, ni mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR- Mageuzi, David Kafulila.

Kwa upande wake, Habibu Mnyaa, mbunge wa Mkanyageni, Pemba anamtuhumu Jussa kwa hatua yake ya kutoshiriki vikao vya Maalim Seif kisiwani Pemba.

Akiandika kwa Profesa Lipumba, Mnyaa anasema kikao hicho kilifanyika kwa usalama na amani na wajumbe walitoa michango yao kwa uwazi na kwa nia ya kujenga chama.

Hata hivyo, Mnyaa anasema, pamoja na kwamba makamu mwenyekiti wa chama chake alihudhuria mikutano iliyoitishwa na Maalim Seif, lakini Jussa hakuhudhuria mkutano hata mmoja ingawa alikuwa kisiwani Pemba wakati huo. Hakueleza sababu.

Lakini taarifa zinasema, baadhi ya viongozi wa CUF wanamtuhumu Jussa kumpotosha Maalim Seif kwa maslahi yake binafsi na kukivuruga chama cho kwa maslahi ya CCM.

Wanatoa mfano wa uchaguzi mkuu uliopita, ambapo Jussa alishindwa kukusanya kura kwenye baadhi ya majimbo na kisha kumshinikiza Maalim Seif kukubali matokeo ya urais hata kabla karatasi za kura hazijapatikana.

Mbunge wa Ole, Rajab Mohamed ambaye katika toleo lililopita alitajwa kama mmoja wa wanaomuunga mkono Hamad, amesema “hahusiki kwa namna yoyote na mpango huo.”

Ameliambia gazeti hili kwa njia ya simu juzi kuwa hawezi kushiriki na hajapata kushiriki kikao chochote chenye lengo la kuchafua chama. “Mimi ni mbunge mpya jimboni, ninaheshimu viongozi wangu ngazi zote hivyo siwezi kushiriki vikao haramu,” alisema.

Idara ya usalama ya CUF ndiyo iliyosambaza taarifa za kuwamo Rajabu kwenye mpango wa kumng’oa Maalim Seif.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: