Hamad Rashid anatamani kuwa popo


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Hamad Rashid Mohammed

KWA siku mbili mfululizo niliwasha kompyuta yangu niandike hiki nitakachoandika leo, lakini nikawa nasita na kujizuia kufanya hivyo.

Hata hivyo, kile wanachoita wazungu ‘guts’ yaani hisia za ndani hazikuniacha, ndiyo maana nimeamua kuingia uwanjani.

Hili si lingine ila ni maamuzi ya baadhi ya wabunge wa upinzani wanaosukumwa pamoja na watu wengine, mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, la kuunda kambi ndogo ya upinzani bungeni. Huyu namtaja kwa makusudi kwa sababu katika kundi hilo ninamweka juu sana .

Huyu ni kiongozi muhimu mno katika siasa za upinzani hasa ndani ya Bunge tangu mwaka 2000. Kiongozi huyu amekuwa Kiongozi wa Upinzani bungeni, tangu alipoenguliwa kwenye nafasi hiyo, mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini (CHADEMA), Dk. Amani walid Kabourou.

Hamad Rashid alikalia kiti hicho akiongoza jumuiko la vyama vya upinzani vilivyokuwa na wabunge, ambavyo ni Chadema na UDP. Awali walikuwapo mbunge mmoja mmoja wa NCCR-Mageuzi na TLP kabla ya Mahakama Kuu kutengua ushindi wao.

Jumapili iliyopita, Hamad Rashid akiwa pamoja na baadhi ya wabunge wa chama chake, na wale wa NCCR-Mageuzi, walielezea nia yao ya kuunda kambi ndogo ya upinzani usio rasmi bungeni kwa kile alichodai kuwa Chadema ambao wana wabunge wa kutosha kuunda kambi rasmi ya upinzani, hawataki kuwashirikisha kwenye kambi hiyo.

Kwa maneno mengine, Hamad anaeleza kuwa Chadema watake wasitake wanawajibika kuwashirikisha kwenye uundwaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, vinginevyo wataunda yao .

Mwaka jana habari za kutaka Chadema ambao kikanuni wana sifa za kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni bila kushirikisha chama kingine, zilitawala mijadala mingi mara baada ya uchaguzi mkuu na kila chama kujua kilikuwa kimepata wabunge wangapi.

Kambi ya upinzani rasmi bungeni ina faida zake katika mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Ni fursa ya kutoa changamoto kwa serikali na kwa kweli ni nafasi ambayo serikali kwa njia moja au nyingine hugharimia shughuli za kambi hiyo, kama vile ofisi, gari na vitendea kazi vingine kwa Kiongozi  wa  kambi hiyo na wasaidizi wake. Hawa ni wale wanaojulikana kama mawaziri vivuli.

Kiongozi wa upinzani na wasaidizi wake, yaani mawaziri vivuli, hupewa upendeleo maalum kujibu kwanza hoja mbalimbali zinazotolewa na waziri katika sekta husika.

Hili limekuwa na faida kubwa katika kuleta changamoto mbalimbali bungeni na kuongeza uwajibikaji kwa upande wa serikali.

Binafsi sitaki kuingia kwenye mtego wa watu wengine wanaoamini kwamba Hamad Rashid analilia kambi isiyo rasmi ya upinzani isiyoshirikisha vyama vyote, kwa sababu anatamani marupurupu aliozoea kupata akikalia kiti hicho, ila ninamtazama kwenye mantiki ya kisiasa kwa sasa nchini.

Nirejee nyuma kidogo, hakuna wakati wowote katika historia ya Bunge la vyama vingi ambako ilipata kutokea CUF kuwa na sifa ya kuunda kambi ya upinzani peke yao.

Mwaka 1995 baada tu ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, CUF iliongoza  kambi rasmi ya upinzani.

Lakini urasmi huo ulikubalika tu baada ya kuingia makubaliano na UDP ambacho kilikuwa na wabunge wanne, Isaac Cheyo (Bariadi Magharibi), Danhi Mkanga (Bariadi (Mashariki), Erasto Tumbo (Kisesa) na Teddy Kasela-Bantu (Viti Maalum).

Wakati huo NCCR- Mageuzi walikuwa na wabunge wengi Tanzania Bara kuliko chama kingine cha upinzani; kilikuwa na wabunge 28 akiwamo Mabere Marando; Dk. Masumbuko Lamwai, James Mbatia, Balozi Paul Ndobho, Ndimara Tegambwage na  Makongoro Nyerere.

Ukitazama wasifu wa wabunge hao, hakika ingelikuwa nia ya CUF ilikuwa ni kuunda kambi ya upinzani wenye nguvu mwaka 1995-2000 haiingi akilini waliwezaje kuwaweka kando akina Mabere Marando, Dk. Lamwai, Ndimara na Mbatia. Nia haikuwa hoja hii anayojaribu kuijenga Hamad leo.

Nakumbuka kulikuwa na baadhi ya wabunge wa CUF bila kutafuna maneno waliokuwa wametokea Pemba ambao walipewa nafasi za kuwa mawaziri kivuli hakika walikuwa kivuli kweli kweli, wakati huo kiongozi wa upinzani alikuwa Fatma Maghimbi mbunge wa Chakechake.

Tukijadili mwaka 2000 na hata mwaka 2005, CUF waliwaalika wabunge wa vyama vingine kuunda upinzani rasmi si kwa sababu ya kupenda, ila kwa sababu kikanuni wasingeweza kuunda kambi hiyo kivyao.

Kwa maneno mengine, kanuni ndizo ziliwafikisha CUF kuwa na uchaguzi wa kushirikiana na vyama vingine kuunda upinzani rasmi bungeni si mapenzi kwa vyama vingine na kutaka kuwatumikia wananchi kama ambavyo Hamad Rashid anataka umma usadiki leo.

Lakini suala la sasa la ushirikiano wa CUF na Chadema ni tata zaidi kuliko hata kwa hoja ya idadi ya wabunge na kanuni tu, hili ndilo ninaloliita hali halisi ya kisasa nchini.

CUF ni shehemu ya serikali ya CCM walau kule visiwani Zanzibar, lakini kwa mujibu wa muundo wa Muungano wa Tanzania , serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina muunganiko na serikali ya Muungano.

Rais wa Zanzibar ambaye ndiye anashirikiana na CUF kule Zanzibar akiwa anatoka CCM ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri la ris Jakaya Kikwete, yaani serikali ya CCM.

Hawa wanakubaliana kwa pamoja katika Baraza la Mawaziri la Muungano na Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa sasa wa Zanzibar hawezi kuacha kuwa sehemu ya makubaliano hayo, kama ambavyo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, hawezi kukwepa kuwa sehemu ya makubaliano ya pamoja katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Katika mkanganyiko kama huo, Hamad anataka kusema kuwa ushirikiano na Chadema hautaleta mkanganyiko katika mambo ya kimsingi kwa maana ya misimamo na mbinu za kukabiliana na serikali ambayo kwa Chadema ni wapinzani kwa asilimia mia wakati CUF ni wapinzani chotara.

Wamo au wana mguu ndani ya serikali zote, moja kwa moja au kwa mhusiano ya kimifumo.

Ni kwa kutafakari hali hii, Hamad Rashid kwa kuwa ni guru katika siasa za Tanzania, si mwanasiasa wa kubahaisha, anaelewa vizuri sana, amepikika kiasiasa na kuiva, angewasaidia Watanzania walewe kuwa kwa sasa haki ya kuunda kambi ya upinzani ni ya Chadema.

Anatakiwa kueleza kuwa wao kiufundi na kimantiki kuwa sehemu ya kambi hiyo, ni kujaribu kuvaa sifa za popo.

0
Your rating: None Average: 4.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: