Hamad Tao: Mrema wa zamani si leo


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Hamad Rajab Tao anamweleza mwenyekiti Augustine Mrema kama mtu aliyekwisha kisiasa.

Anadai kuwa Mrema, ambaye pia ni mbunge wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro, anakichafua chama na kwa sasa “amepoteza mvuto kwa siasa za sasa za harakati.”

“Hawezi tena (siasa hizo). Ni kujiuzulu kwa sababu kwa kuwa tu mwenyekiti wa TLP kwa miaka 12, tayari amedhihirisha sasa habari yake imekwisha,” anasema Tao katika mahojiano maalum na gazeti hili yaliyofanyika juzi.

MwanaHALISI ilitaka kujua kwa undani hasa kitu gani kinachosababisha mtafaruku mpya ndani ya TLP hata kulazimu Katibu Mkuu wake, Jesse Makundi ajiuzulu na Kamati Kuu kumsimamisha Tao.

Tao anasema Mrema atajijengea heshima ya pekee akiamua kukaa kando ya uongozi wa juu na kuongeza kuwa ni muhimu akafanya hivyo sasa ili kutoa nafasi kwa chama kujijenga upya.

Anasema iwapo Mrema atapumzika uongozi, chama kitamsimamia tena agombee ubunge utakapofika uchaguzi mkuu ujao hapo mwaka 2015. “Isitoshe, bado ataendelea kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu,” anasema.

Tao anamtuhumu Mrema kuwa uongozi wake umechangia kushusha mvuto waliokuwa nao wananchi juu ya TLP.

Ushahidi wa hilo, anasema ni matokeo mabaya ya uchaguzi ambapo mwaka 2000-2005 chama hicho kilikuwa na wabunge watano na madiwani 85, lakini sasa kina mbunge mmoja tu na madiwani 30 pekee nchi nzima.

“Mrema anaendesha chama hiki bila kufuata katiba na bila kufuata sheria. Anafanya chama kama shamba lake binafsi.

“Yeye ni mwenyekiti wa chama, yeye ni mwenyekiti wa bodi ya udhamini, yeye ni signatory (muidhinishaji wa kutoa fedha benki), yeye ni mdhibiti wa hesabu za chama… tena yeye ndio mwenyekiti mtendaji. Haiwezekani namna hii hiki ni chama cha Watanzania,” anasema.

Katika kudhihirisha kuwa Mrema anapaswa kupumzika uongozi, Tao anatoa mfano wa wanasiasa mahiri walioachia ngazi za uongozi wa juu baada ya kuzeeka.

Kwamba Mrema, anayeona amezeeka, inafaa afuate nyayo za Edwin Mtei na Bob Makani waliong’atuka mapema kutoka uongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Anasema, “Ona mifano hii ya viongozi mbalimbali wa siasa. Muasisi wa CHADEMA, Edwin Mtei na Bob Makani ambaye sasa anabaki mwenyekiti mstaafu tu. Hawa walijua wakati umewapita.”

Tao anavuka mipaka ya Tanzania na Afrika. Anasema hata Pele au Edison Arantes do Nascimento, mwanasoka mahiri wa karne, amekaa kando ya viwanja mara tu alipogundua wakati umempita.

Mrema anatuhumiwa na Tao kwa kushindwa kufanya kazi na watendaji mbalimbali waliokuwa pamoja katika vyama vya siasa tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa nchini mwaka 1992.

Anawataja Mabere Marando, Prince Bagenda na Makidara Mosi ambao walikuwa pamoja na Mrema katika Chama cha NCCR-Mageuzi, alikohamia baada ya kuihama CCM mwaka 1994.

Kutoka NCCR-Mageuzi, Mrema alihamia TLP alikokaribishwa na Leo Lekamwa pamoja na Harold Jaffu, Sheikh Ali Idd Ali.

Tatizo kubwa la Mrema, Tao anadai, ni kushindwa kufuata uongozi wa pamoja - Collective Leadership badala yake akipendelea kufanya kila kitu.

“Labda mwenzetu mwenyekiti hajui. Mambo haya wanachama wanayalalamikia. Shida iliyopo ni kwamba tunapompa taarifa ya yanayoendelea, anakuona wewe ni adui wake. Sasa amefikia hatua kuamini mimi Tao namchonganisha na wanachama. Nifanye hivyo ili nipate nini,” Tao anahoji.

Tao analalamika kuwa kwa sababu ya hayo, Mrema amehamasisha wapambe wake wamsimamishe (Tao) kwenye nafasi yake; lakini anasema, “Nimekata rufaa Halmashauri Kuu na pia nimemwandikia Msajili.”

Kuna kitu ambacho Tao hataki kukinyamazia ndani ya TLP. Anasema ingawa katiba ya chama chao inaelekeza barua yake ya rufaa aipeleke kwa Sekretarieti, amesita kufanya hivyo kwa kuhofia kutotendewa haki.

Chimbuko la hofu yake hiyo anasema ni kule sekretarieti hiyo inayojumuisha wajumbe kumi, kutawaliwa na viongozi watokao kabila moja tu la Uchagga ambalo ndilo la nyumbani kwao Mrema. Wajumbe hao ni sita.

Anasema hoja yake ipo kwenye Sheria ya Uchaguzi Na. 9, kifungu kidogo cha (2), sehemu (a) chenye vipengele (i) na (ii) ambavyo vinasema: Uongozi haupaswi kuundwa kwa kuangalia vigezo vya ukabila au udini.”

Sivyo ilivyo kwa TLP. Tao anasema kwamba ukiacha Makundi aliyejiuzulu, Kamati Kuu ina wajumbe 30, lakini 20 kati yao ni “watu wa Mrema.”

“Ndipo ninaposema nasubiri Halmashauri Kuu yenye wajumbe zaidi ya 100 ambao ni makini. Hawa watafanyia kazi rufaa yangu na sina shaka watatenda haki. Ni imani yangu watanirejesha madarakani.”

Tao, aliyewahi kuhamia CHADEMA mwaka 2009, baada ya kuongoza TLP akiwa katibu mkuu, anasema hajatia nia ya kuondoka au kujiuzulu uongozi katika chama hicho.

Anasema hana mpango huo kwa sababu ametoka mbali nacho. “Chama hiki tumekitoa mbali sana hadi sasa kuwa kinafahamika na kukubalika. Lakini tatizo ni mwenyekiti Mrema kukiyumbisha chama,” analalamika.

Tao anasema wanachama wanahoja ya kutaka kujua kwanini chama hakiitishi vikao vya juu vya kikatiba kama vile kikao cha halmashauri kuu kwa wakati.

Kikao cha mwisho cha Halmashauri, kwa mujibu wa Tao, ni kile kilichofanyika mwezi Aprili mwaka jana. “Jambo hili ni kinyume na utaratibu kwa vile katiba inataka halmashauri iitishwe angalau mara moja kwa mwaka.

Na hili amelibainisha wazi katika barua yake ya malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa. Anasema wanachama wanataka kujua taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za chama lakini imekuwa vigumu kuzipata.

Sababu ya hilo anasema ni Mrema ambaye japo chama kina mweka hazina kama inavyotakiwa kisheria, “yeye hataki kuona kitu kama hicho. Katika hali kama hii, kwanini basi mtu usitie shaka kuwa huenda ni mbinu za kutumia vibaya fedha za wanachama.”

Tao anasema amelalamikia pia suala hilo katika barua yake kwa Msajili. “Nimemwandikia (Msajili) mapendekezo kwamba azuie kwa muda ruzuku yetu ya chama ili mwenyekiti afuate taratibu. Nashangaa mpaka sasa hakuna majibu,” anasema.

Barua hiyo kwa Msajili aliiandika Julai mosi na kuituma siku hiyohiyo.

Tao anasema hadi sasa TLP haijaitisha kikao cha Halmashauri ili kujadili taarifa ya kueleza matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi kulingana na sheria mpya ya gharama za uchaguzi pamoja na kufanya tathmini ya uchaguzi kwa chama hicho.

Anamlalamikia Mrema kwamba hajaitisha kikao hicho na hivyo kusababisha ukiukaji wa sheria hiyo inayosimamiwa na Msajili wa Vyama nchini.

Tao anasema katika uchaguzi uliopita, chama hicho kilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda ubunge kwa majimbo ya Chunya, mkoani Mbeya ambako mgombea wao, Wolfgong Ngaka alishindwa na Victor Mwambalaswa wa CCM kama alivyoshindwa Sunday Sanga, jimbo la Mtama, mkoani Lindi dhidi ya Bernard Membe kwa tofauti ya kura chache.

“Kama wangepata sapoti (wagombea hao), nadhani tungefanikiwa. Lakini Mrema alionyesha ubinafsi wa wazi kwa kuchukua vifaa kama magari, vipaza sauti na fedha zote kwenda nazo Vunjo. Mbaya zaidi TLP ilikuwa na mgombea urais Mutamwega Mugahywa, lakini mwenyekiti akimpigia debe mgombea wa CCM. Huku ni kuvuruga chama,” anasema Tao akimtuhumu Mrema.

“Watu wanatushangaa, hata huko Chunya na Mtama, tungeshinda, lakini wananchi wanahoji mbona bosi wetu anaipigia debe CCM badala ya mgombe wake. Mrema amerudi CCM kwa mlango wa nyuma. Hii ni mbaya sana, bora angefanya kama wenzake akina Thomas Ngawaiya, Tambwe Hizza na akina Akwilombe ambao wametangaza wazi,” anasisitiza.

Tao hakubali kwamba ana ugomvi binafsi na Mrema na kwamba huwa wanawasiliana ma kusisitiza, “Nampenda, namheshimu lakini ustaa una mwisho. Yeye hawezi tena kuwa staa wa siasa na anajua wanachama wanataka kuona viongozi wao wanafanya siasa kuwakomboa siyo kujikomba.”

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: