Hamid Karzai: Jasusi wa CIA aliyesaidia Taliban


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai

SWAHIBA mkubwa wa Marekani, rais wa Afghanistan, Hamid Karzai anaonyesha kurudi tena madarakani.

Karzai ameshinda uchaguzi mkuu uliofanyika wiki mbili zilizopita. Aligombea tena kiti hicho dhidi ya wagombea wengine, akiwamo waziri wa zamani wa nchi za nje, Abdullah Abdullah.

Matokeo yaliyomrejesha madarakani bado hayajatangazwa rasmi. Ni kutokana na hofu, hasa kwa Marekani, ambayo ina maelfu ya askari Afghanistan. Kwamba huenda kukazuka machafuko.

Matokeo yasiyo rasmi yanaonyesha kuwa Karzai ameshinda kwa zaidi ya asilimia 54 ya kura zote, ingawa vikundi vingi vinasema masanduku ya kura katika baadhi ya vituo yalijazwa kura bandia.

Uchaguzi huu ulifanyika wakati nchi iko katika mapambano na wapiganaji wa Taliban dhidi ya majeshi ya uvamizi ya Marekani na washirika wake kutoka Umoja wa Kujihami wa Nchi za Ulaya (NATO).

Mapambano kati ya askari wa Marekani na vikosi vya Talban yamepamba moto na sasa yanampa wakati mgumu Rais wa Marekani, Barack Obama, kuamua iwapo aongeze askari au awaondoe kabisa wale waliopo.

Tayari tathmini imefanywa na mkuu wa vikosi vya Marekani nchini humo. Inaonyesha kuwa Marekani haitashinda vita hiyo bila kupelekwa askari zaidi.

Wanaofuatilia masuala ya eneo hilo wanafahamu kuwa Iran, inayopakana na Afghanistan, ilifanya uchaguzi wake wa urais zaidi ya mwezi mmoja kabla, uchaguzi uliogubikwa pia na utata.

Vyombo vya habari vya magharibi, vikiongozwa na Marekani, viliuponda uchaguzi wa Iran na kuonyesha kulikuwa na wizi wa kura ili kumpa ushindi Mahmoud Ahmadinejad. Kwa uchaguzi wa Afghanistan, nchi hizo zimekuwa kimya.

Harakati zote za Marekani nchini Afghanistan zimedumu hadi sasa kutokana na mtu mmoja tu, aliyetayarishwa na kupambwa vilivyo na Marekani kutwaa urais, na baadaye kumpa ulinzi mkubwa.

Ni Hamid Karzai, ambaye wachunguzi wa mambo wanasema hana mamlaka yoyote nchini mwake na badala yake anatajwa kama meya wa Jiji la Kabul tu.

Wafuatiliaji wa masuala ya kivita wa Marekani wamekuwa wakitaja kuwa wakati George Bush anatwaa madaraka mwaka 2001 Afghanistan haikuwamo katika mpango wake wa kuivamia kijeshi.

Azma kubwa ya Bush ilikuwa ni kuivamia Iraq katika kukamilisha kile alichokianza baba yake, George Bush, katika vita ya kwanza ya Ghuba miaka ya 1990.

Mashambulizi ya majengo katika miji ya New York na Washington, ya 11 Septemba, 2001, yalitibua ratiba ya Bush na kulazimika kuivamia Afghanistan ili kuwasaka magaidi wa Al Qaeda, kilichodaiwa kuhusika na tukio hilo, ambacho kinaongozwa na Osama bin Laden, aliyepewa hifadhi nchini humo na watawala wa Taliban.

Baada ya majeshi ya Marekani kuundoa utawala wa Taliban, kulihitajika kuwapo serikali ili nchi hiyo isionekane inakaliwa kijeshi na Marekani.

Mtu huyo ni Hamid Karzai, Muafghanistan msomi na wakala wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), tangu wakati wa mapambano ya wapiganaji wa Mujahideen dhidi ya majeshi ya iliyokuwa Urusi ya Kisovieti, waliokuwa wakiikalia baada ya kupinduliwa kwa serikali ya Mohammed Daood mwaka 1977.

Hamid Karzai alikuwa kiungo muhimu kati ya CIA na Mujahideen, ambao ndio chimbuko la Taliban, katika harakati za kuyaondoa majeshi ya Kisovieti.

Kazi hiyo aliifanya kwa kushirikiana na mbabe wa kivita nchini humo, Gulbuddin Hekmatyar, aliyewahi kuwa waziri mkuu katika miaka ya 1990. CIA ilimtumia kupigana na majeshi ya Kisovieti miaka ya 1980, ingawa mara nyingi alionekana ndumilakuwili.

Hekmatyar alikuwa akimiliki mashamba makubwa ya zao la poppy, linalotoa opium ambayo hutengenezwa dawa za kulevya.

CIA, ikishirikiana na Karzai, ilimsaidia Hekmatyar kupata soko huko Ulaya na nchi nyingine na fedha zilitumika kuendesha vita dhidi ya Warusi, huku Marekani ikitoa mamilioni ya fedha pia.

Tatizo lililowapata Wamarekani huko Afghanistan ni namna ya "kumuuza Karzai" kwa Waafghanistan ili akubalike. Wananchi wengi walikuwa hawamfahamu. Na wale waliomfahamu, walijua ni mfuasi wa Taliban tu.

Kabla ya mkutano wa Berlin, ulioandaliwa na Marekani ili kuchagua serikali ya mpito mwaka 2002, ulijumuisha vikundi mbali mbali vilivyowapinga Taliban. Ilibidi Karzai aangaliwe vyema kutokana na uhusiano wake na Taliban.

Kazi hiyo ilifanywa na CIA, wakishirikiana na Wizara ya Ulinzi ya Marekani. Desemba 2001, walimtembeza vijijini, hasa jimbo la Uruzgan, Magharibi mwa nchi hiyo, lililokaliwa na majeshi ya Marekani.

CIA ilitumia pesa nyingi kuwalipa watawala wa jadi na wenyeji wengine ili watafutwe vijana wa kupiga picha ya pamoja na Karzai, huku wakiwa wamevalia sare za wapiganaji wakishika silaha.

Picha hizo zilitangazwa kwenye televisheni na magazeti ili kuonyesha kuwa Karzai ni mzalendo na mpiganaji hodari dhidi ya utawala wa Taliban.

Mbinu ilifanikiwa. Karzai alikubalika akashinda uchaguzi wa urais mwaka 2004. Taliban wanalifahamu hilo. Wamedhamiria kumng'oa.

0
No votes yet