Hamid Mbwezeleni: Zanzibar si nchi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version

HAMID Mbwezeleni, wakili maarufu nchini, ndiye aliibua hoja, katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na baadaye Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano kwamba, "uhaini hauwezi kufanyika Zanzibar, kwa sababu Zanzibar si nchi, bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano"

Je, sasa madai kwamba Zanzibar ni nchi yanatoka wapi?

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI, wiki hii, ofisini kwake Malindi, Unguja, Mbwezeleni anasema, "Kwa mujibu mujibu wa sheria na katiba zote mbili, Zanzibar si nchi. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano."

Mbwezeleni anasema, "Hili ni suala linalokuzwa na watu wanaosaka urais mwaka 2010. Hawa ndio wanaosema kwa sauti kubwa kwamba Zanzibar ni nchi."

Anasema, "Nimekaa hapa (Visiwani) kwa miaka 20 mfululizo. Nina ubavu wa kusema haya. Kwanza nayajua, lakini pili, yananihusu."

Mbwezeleni pia amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu (SMZ), katika kipindi cha utawala wa Dk. Salmin Amour. Anasema, "mjadala juu ya suala hili uliishafungwa."

Anasema "Ibara ya kwanza ya Katiba ya Zanzibar, inasema Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."

Eneo la Zanzibar linalotajwa na katiba "ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vilivyozungukwa na bahari yake kabla ya Muungano ambayo ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar."

Anasema, "Katiba ya Muungano, Ibara ya kwanza inasema pia kwamba eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo."

Anasema tatizo kubwa hapa ni kwamba wanaozungumza kwa sauti kubwa kwamba Zanzibar ni nchi, hawaifahamu historia ya Zanzibar.

"Lakini hawazungumzii Tanganyika. Wengi wa hawa wanaozungumza kwamba Zanzibar ni nchi, hawaijui sheria na hata historia ya Zanzibar," anasema.

Anasema katiba ya sasa ya Zanzibar imetungwa mwaka 1984, kabla ya hapo Zanzibar haikuwa na katiba, bali ilikuwa inatumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

"Baada ya Muungano, Zanzibar haikuwa tena na katiba. Kilichotokea, iliruhusiwa kufanya mambo ambayo hayakuwa katika Muungano," anasimulia.

Anasema baada ya Mapinduzi, Zanzibar ilikuwa na sheria yake. Sheria hiyo ndiyo iliyounda Ofisi ya Rais, Makamu na Baraza la Mawaziri. Lakini sheria hiyo ilikufa mara baada ya kusainiwa kwa Muungano 26 Aprili 1964.

Hata Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963 (wakati wa utawala wa Sultani) ilikufa siku ileile baada ya Mapinduzi; sheria hizo pamoja na zile za Tanganyika zilikufa na kuingizwa katika Muungano.

"Kuunda jeshi, kwenda kushambulia, zilikuwa ni pawa (nguvu) za Tanganyika na Zanzibar. Baada ya Muungano, zilihamishiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," anasema.

Anasema tatizo kubwa hapa ni kwamba watu wanaichukulia serikali ya Muungano kama serikali ya Tanganyika, au Bara. Hawaichukulii kama serikali ya Muungano.

Akiingia kwa undani zaidi, Mbwezeleni anasema suala hilo la Zanzibar kutokuwa nchi, tayari lilishaamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Anasema, "Unakumbuka wewe; kulikuwa na shauri mahakamani juu ya jambo hili. Katika kesi ya Uhaini iliyowakabili wanachama 18 wa Chama Cha Wananchi (CUF); ni mimi niliyejenga hoja hii kwamba Zanzibar si nchi."

Anasema, mahakama ya rufaa chini ya majaji Augustino Ramadhani, Lewis Makame na Kahwa Lugakingira iliridhika kuwa Zanzibar si nchi, bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano. Hukumu hiyo ilitolewa Machi 200.

Baada ya hukumu hii, serikali haikuomba Mahakama ya Rufaa kupitia upya uamuzi wa majaji hao watatu.

Sasa Mbwezeleni anasema, "Pinda (Waziri Mkuu, Mizengo Pinda) anapata wapi uwezo wa kuwataka mwanasheria mkuu wa serikali ya Muungano na mwenzake wa Zanzibar, wakutane na kupata tafsri ya kisheria katika jambo hili"

Anasema, kwa mujibu wa taratibu na sheria, kazi ya serikali si kutafsri sheria, bali kuandika rasimu ya sheria. Ni kazi ya Bunge kupitisha sheria na kazi ya Mahakama kuzitafsri sheria hizo.

Huku akikaza macho, Mbwezeleni anasema, "Nani ana ubavu wa kusema hapa kwamba, kwa mujibu wa sheria na katiba, Zanzibar ni nchi"

Katika hilo, Mbwezeleni anatupa lawama zake kwa viongozi wa serikali ya Muungano. Anasema wamekuwa na tabia ya kunyamazia kile alichoita, "Vitendo vya watawala wa Zanzibar kuvunja katiba."

Anasema viongozi wa serikali ya Muungano wanajua kwamba Katiba ya Muungano haiwezi kuvunjwa na katiba ya Zanzibar, lakini wamekuwa wakikaa kimya.

Anasema kwa mfano, katika mkataba wa Muungano eneo la Forodha na Usalama wa taifa, yanatajwa kuwa ni mambo ya Muungano.

Lakini Zanzibar wameyachomoa na kuyafanya mambo yake. Wameunda majeshi na kusema yanaweza kushambulia hata nje ya mipaka ya Zanzibar, anasema.

Anasema, "Zanzibar, wameunda ZRB (Bodi ya Mapato Zanzibar), badala ya kazi hiyo kufanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kama sheria inavyotamka. Haya ni mambo yaliyonyamaziwa na serikali ya Muungano na tayari yamaenza kuleta matatizo."

Aidha, Mbwezeleni anasema hata suala la Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu Ulimwenguni (OIC), linapotoshwa na baadhi ya wanasiasa, huku serikali ya Muungano ikiwa kimya.

Anasema wananchi wanadanganywa kwamba haya ni mambo ya kidini. Wanaopotosha, anasema, hawasemi kwamba haya mambo ni ya Muungano; kwamba suala la mikopo, sarafu na Benki Kuu ya Taifa, ni suala la Muungano.

Aidha, hawasemi kuwa OIC ni taasisi inayotoa mikopo na hivyo siyo suala la kidini.?

Kwa mujibu wa katiba, mikopo yote ya nje iko chini ya serikali ya Muungano. Hilo hawalisemi na serikali ya Muungano imenyamaza, anaeleza.

Mbwezeleni anasema yeye ni mwenyeji wa Zanzibar na Tanzania Bara. Mama yake ni kutoka Bumbwini, mkoa wa Kaskazini Unguja. Baba yake ni kutoka Kisarawe, mkoani Pwani, Tanzania Bara.

Kabla ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alipata kutumikia Jeshi la Polisi na kufikia cheo cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO). Alijiunga na jeshi hilo mwaka 1968 na kustaafu mwaka 1985.

"Wazanzibari tusitie ulimi puani. Zanzibar ilipoteza utaifa wake miaka 40 iliyopita. Je, hawa wanaoibuka leo, wametoka wapi," anauliza.

Anasema, "Leo tunataka serikali tatu, mimi sikatai hilo. Hata wakitaka serikali nne, kama CCM kitataka zitakuja. Lakini bado haziwezi kutatua matatizo ya wananchi."

Kinachotakiwa ni Zanzibar kujenga viwanda na kukuza uchumi wake, anasema na kuongeza, "Haya hayawezi kuzuiwa na serikali ya Muungano."

"Tuache ubabaishaji," anasema Mbwezeleni na kuongeza, "Tujenge viwanda, tuimarishe uchumi, badala ya kupiga porojo za Zanzibar ni nchi, Zanzibar nchi! Hayo hayawezi kutusaidia."

0
No votes yet