Hamza baba, uungwana unalipa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma

NAFURAHI kuona Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma ameramba matapishi yake mwenyewe. Amegeuka.

Hamza ameivua Marekani na tuhuma alizoitupia pale aliposema hadharani kuwa nchi hiyo imehusika katika matukio ya milipuko ya mabomu iliyokuwa yameshamiri kisiwani Pemba.

Japo amefanya hivyo kwa kuzidisha udanganyifu – akidai kwamba yeye hajawahi kusema wamehusika – bado ukweli unabaki palepale kwamba “amejirudi kwenye uhalisia wa mambo.”

Hamza alitamka hadharani na kukaririwa na vyombo vya habari ikiwemo Televisheni ya Serikali ya Mapinduzi, TVZ, akiituhumu serikali ya Marekani kufahamu kinachoendelea Pemba wakati wa uandikishaji wapiga kura, baada ya nchi hiyo kutoa taarifa kwa raia zake wasifike Pemba kwa kuwa yanayotokea yanaashiria ukosefu wa amani.

Taarifa ya ilani ya Marekani iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje (State Department) mjini Washington na nakala ya taarifa hiyo kupatikana mjini Zanzibar, ilisema wazi kuwa ilitokana na utafiti walioufanya.

Lakini hata pale msemaji wa wizara hiyo alipotoa taarifa ya pili akirejelea matamshi ya ovyo ya Hamza, alisisitiza kuwa Marekani imechukua hatua hiyo kwa maslahi ya raia zake wala haikuhitaji kumuuliza kiongozi yeyote wa Tanzania.

Bila ya shaka matamshi ya ovyo ya Hamza yaliikasirisha Marekani, na hatua hii mpya ya waziri huyo kujirudi ndani ya Baraza la Wawakilishi inaonekana haikuwa hivihivi, bali ni kwa kuzingatia maafikiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania.

Tatizo la Hamza kuwa hataki kuwa muungwana katika kujirudi. Anajizonga kwa kuanzisha uhasama na vyombo vya habari; eti vilimsingizia. Hivi Hamza asingiziwe ili iwe nini? Anajulikana mkate wake umeongezeka siagi miaka hii kutoka ule wa kutegemea ushoni aliokuwa akitegemea Mikunguni.

Ninaisema kwa makusudi hii ili akae vizuri na mtindo anaouanzisha wa kurudisha lawama kwa wasiohusika kwa kosa alilojitia mwenyewe, tena kwa hiari yake na raha zake.

Lakini hii haikuwa mada yangu, ila nimelazimika kugusia hapo kwa kuwa nilipata kumsihi Hamza kuwa “hayawezi madhambi ya SMZ.”

Leo nikitaka hasa kueleza hofu yangu kwamba kwa kuwa mwenendo wa dola haujabadilika; kwamba haijafuata ukweli kuwa inanyonga haki za wananchi; basi sitarajii mabadiliko yoyote uandikishaji wapiga kura utakapoingia Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ni dhahiri kwamba misimamo ya viongozi wa vyama vya upinzani itabaki ileile ya kukataa kushiriki katika mduara wa ushetani wa kuhalalisha maovu yanayotendeka dhidi ya mfumo wa demokrasia.

Ninamaanisha kuwa hawatahamasisha wananchi wanaowatii kujitokeza kwenye vituo vya uandikishaji ili kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar.

Na siyo tu kwamba hawatawahamasisha watu kujitokeza vituoni, bali pia watawaelekeza kujipanga vizuri ili kuzuia wale waliopatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi wasiandikishwe.

Naiona hali hiyo kwa sababu bado tatizo liliopo – ambalo limekwamisha uandikishaji wenye ufanisi kiasi cha kusikitisha wakuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kama inavyodhihirika katika taarifa zake kwa umma – halijatatuliwa.

Tatizo ni kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, ambacho kuanzia mwaka 2006, kimeingizwa katika sheria ya uchaguzi kama shurti kwa kila Mzanzibari kukimiliki ndipo atambuliwe na kuandikishwa kama mpiga kura, kingali kinatolewa kibaguzi kwa kuzingatia nani kura yake ataitia kwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa yule ambaye machoni mwa wenye kulea mfumo wa kidhalimu, ataonekana si miongoni mwa wakereketwa au makada wa CCM, itabaki tu kuwa shida kwake kuruhusiwa kupata kitambulisho na hivyo kujikuta hapenyi kwenye wigo wa watu wema.

Kwa mfumo wa utawala uliopo hadi sasa, watu wema ni wale tu ambao hata kama si hadharani, lakini wana sura ya kupigia kura mgombea wa CCM tu na si vinginevyo.

Asiyekuwa na chapa ya CCM kwenye paji lake la uso, ajue kura ya 2010 ataisikia tu. Ataisikia kwa sababu kwa kuwa hana kitambulisho, hatapata kuandikishwa. Asipopata kuandikishwa, hatapata kupiga kura.

Kitambulisho cha Mzanzibari kimekuwa dili. Baada ya kuanza kama maskhara, ingawa kilipingwa kwa nguvu nyingi kwa kuhofiwa kitatumika vibaya, tulipo kishathibitika kuwa kililetwa kwa dhamira mbaya hasa. Ukweli unaonekana.

Kimeshasababisha maelfu ya watu kunyimwa haki yao ya msingi ya kuingia katika daftari la wapiga kura. Hawa wamekalia kuti kavu kwani nafasi kwao kuingia ni sawa na mbuni kupita kwenye tundu la sindano. Labda ipite kudra ya Mwenyezi Mungu kabla ya Oktoba mwakani.

Ikija kudra hiyo basi ndipo ukweli utapodhihiri na uongo utapojitenga. Hapo ndipo mbivu itapoliwa na mbichi itaposubiriwa iwive ili nayo iliwe kwa wakati muafaka. Ni wakati huu nyuso za wakubwa zitakaposinyaa kwa aibu.

Watatahayari maana yale waliyoyapanga kutokea ili kujinufaisha nafsi zao, yatakuwa yametenguka. Ushetani waliolenga kuufanikisha utakuwa umekomeshwa. Wamenyamazishwa. Na hii si wao tu, bali hata mawakala wao wanaojitahidi kutetea wanachokifanya.

Uandikishaji utakapoingia majimbo ya wajanja na “wasemaji ovyo isivyomithilika” watunza takwimu za kupika wanaoishi kwa kujisuta, wataumbuka na kubaki kushangaa. Labda watatamani ardhi ipasuke wajifiche. Labda wataamua kuhama nchi. Sijui.

Tushaona uandikishaji ulivyoleta aibu kwa wakubwa katika majimbo ya Kaskazini Unguja. Tushajionea namna mikakati ya kuvuruga uchaguzi inavyoandaliwa. Tushafahamu kumbe bado wakubwa hawajaamini kuwa siku hazigandi.

Ukweli ni kwamba umma umeelewa dhamira hasa za viongozi wa CCM katika kuitisha uchaguzi. Kumbe ni kiinimacho na jambo la kudanganya ulimwengu. Masikini roho zao hawajui kwamba uchaguzi huru na wa haki si matamshi bali matendo.

Masikini roho zao hawajui kuwa hawana wafichacho. Kila kitu kipo kweupeni zama hizi. Hawajui kuwa ndani ya ofisi za umma wanazotumia kufanikisha udanganyifu wamo watu wema kwa Wazanzibari wenzao na nchi yao waipendayo kama mboni za macho yao.

Masikini roho zao viongozi hawa wahafidhina hawajui kwamba kwa sasa wanapuruziwa tu kamba kwani iko siku kila kitu kitabadilika na mambo yatageuka nyuma mbele, na wao watasaga mawe kama alivyofanya firauni na wenzake.

Hata kama si kesho na keshokutwa, hakuna chenye mwanzo kikakosa mwisho. Nasema hakuna kinachodumu milele iwapo binadamu mwenyewe ataukata na kurudi alikotoka. Basi mambo yatabadilika tu Inshaallah.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: