Hapa ndipo tunapokosea katika soka


Maurice O. Gama's picture

Na Maurice O. Gama - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version

NAANDIKA makala hii kutoa mchango wangu kuhusu mjadala ulioanzishwa katika gazeti hili tarehe 22 Juni, 2011 uliokuwa na kichwa; “Tunakosea wapi katika soka?” Ufuatao ni mchango wangu.

Timu ya mpira wa miguu ni mjumuiko wa watu 11 wanaotakiwa kucheza kwa uelewano mkubwa. Watu hao wanapatikana kwa ustadi wa kila mchezaji binafsi kuumudu mpira.

Uwezo binafsi wa kumiliki mpira ukichanganya na hulka ya mchezaji ndipo hupangiwa nafasi uwanjani; kulinda goli au kushambulia mbele au kiungo katikati.

Bila kuwa na wachezaji wenye ustadi binafsi kuunda timu bora haiwezekani. Haijalishi kocha ni wa hadhi gani, miguu ya mchezaji ikiwa na kigugumizi cha kusukuma mpira hakitafanyika kitu na hasa kama timu yenyewe ni ya wakubwa.

Mchezo wa mpira wa miguu, unategemea sana miguu kutekeleza majukumu. Zipo stadi nne za msingi ambazo miguu lazima iweze kutekeleza. Kwanza ni kutoa pasi; pili ni kupokea pasi; tatu ni kuondoka na mpira, na nne kujipanga upya kupokea mpira mwingine. Mengine kama kupiga mpira kwa kichwa kupiga mashuti ni nyongeza japo yanatakiwa.

Pale mchezaji atakapoweza kutekeleza hatua hizo hapo juu kwa wepesi bila kigugumizi cha miguu ndipo tunasema mchezaji amekamilika. Baada ya hatua hii unaweza kuunda timu, vinginevyo mtacheza tu mpira kwa kubutua.

Tofauti kati ya wachezaji mahiri katika soka jana, leo na kesho inatokana na uhodari wao katika maeneo hayo manne. Hapa nyumbani wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa, kwa mtazamo wangu, ni waliochezea Yanga kabla haijavunjika.

Uthibitisho wa mapungufu katika stadi hizo nne, angalia jinsi mchezaji anavyoshindwa kutuliza mpira, anavyotoa pasi butu, anavyoshindwa kukimbia nao na hata namna ya kujipanga ili amsaidie mwenzake.

Anakimbia uwanjani bila ulazima na hajui anakimbilia nini na wapi! Mipira mingi hutoka nje ya uwanja wakati wa mechi. Mara ngapi umeshuhudia mchezaji akipiga mpira nje ya goli wakati yupo peke yake karibu au ndani ya eneo la penalti?

Mapendekezo

Kwanza, tuanze kuwanoa wachezaji wakiwa na umri kuanzia miaka 15. Wachezaji hawa wapatiwe mazoezi yanayolenga kuwapa ustadi katika maeneo hayo manne. Pili, wapatikane walimu wa kufundisha hizo stadi za mpira. Walimu wa ngazi ya kawaida wataifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Tatu, mazoezi yatengewe muda wa kutosha; saa nne asubuhi na saa nne jioni (kama ni wanafunzi saa mbili asubuhi na saa tatu hadi nne jioni.) Mazoezi ya asubuhi yawe kwenye stadi za kumiliki mpira. Wajengewe ukuta wa kujifunzia kupiga pasi na kupokea pasi na kadhalika. Mchezaji mmoja mmoja atajifunza kwa haraka zaidi kwani ukuta utamrudishia mpira kadiri anavyotaka.

Ukuta huo utumike kama mfano wa goli na ugawanywe sehemu kuu tano. Kona za chini alama 5; kona za juu alama 4; ubavuni mwa kipa alama 3, juu ya kichwa cha kipa alama 2, miguuni mwa kipa alama moja na katikati upana wa mikono na kimo cha kipa alama sifuri.

Mchezaji atatakiwa atumie huo ukuta kujifunza pia kulenga golini kwa mpira uliokufa au uliohai. Kuna ustadi wa kupiga mpira kwa kutumia sehemu za mguu na namna kiwiliwili chako kinavyo simama wakati wa kupiga mpira wenye mwelekeo. Asipo zijua hizo mbinu mchezaji utamwona anapiga mpira juu ya goli wakati yupo hatua kumi tu toka golini.

Nne, katika mazoezi haya yasiingiliwe tena na mazoezi ya viungo. Kimbia kimbia ya mazoezi haya inatosha kuukomaza mwili.

Ikumbukwe huu ni mchezo wa mpira wa miguu, kijana ajifunze kupiga mpira kwa miguu yote miwili. Muda mwingi miguu iwe na mpira. (Askari hata awe ngangari kiasi gani katika gwaride, kulenga shabaha ni lazima aimudu bunduki vema).

Mashindano sio mahala pa kujifunza stadi za mpira bali pa kukomaza. Kama mchezaji hana stadi mashindano hayatamsaidia kitu.

Sambamba na mapendekezo ya hapo juu ni kuwaandaa vijana shuleni kuanzia shule za msingi sio sekondari. Vijana mashuleni wana muda mwingi wa kujifunza na kukomaa na stadi hizo.

Mazoezi yao ya viungo yalenge jambo maalum kama ni uvumilivu, nguvu, kasi, nk. yasiwe kama ya sarakasi kupendezesha macho. Muda wa mazoezi ya viungo usiingiliane na muda wa mazoezi ya stadi za mpira.

Walimu wafundishwe na walimu wenye ujuzi mkubwa katika fani ya mchezo wa mpira. Mara moja moja makocha wanaweza kutoa kliniki kwa wachezaji moja kwa moja.

Makocha

Makocha wa bei kubwa ni wataalam wenye ujuzi wa kujenga timu sio kufindisha stadi za msingi. Pili kwa fani yake kocha ni sawa na mwashi. Mwashi hafyatui tofali bali hulitumia tofali lililotayari. Ujenzi utakuwa rahisi iwapo tofali litakuwa na umbile sahihi.

Kocha akipata wachezaji waliotimia katika maeneo manne niliyotaja anaweza kuunda timu na ikatekeleza analoagiza kwa ufanisi.

Makocha wote waliofika hapa nchini wameshindwa na wataendelea kushindwa mpaka wachezaji wenye staid nne wapatikane. Mbrazil Marcio Maximo aliwahi kulalamika kwamba anashindwa kutekeleza majukumu yake kwani wachezaji mahiri hawapo. Kocha mmoja mzalendo aliwahi pia kuuliza hivi wachezaji wetu kweli hawafundishiki?

Bahati mbaya makocha wa kwetu wanajitahidi kufundisha vema kwa yasiyo sahihi. Makocha wetu wanayajua mapungufu ya wachezaji lakini badala ya kuwapatia mafunzo katika stadi za mpira, jambo ambalo ndilo sahihi, msisitizo wa mafunzo yao ni kwenye kukimbia, kuruka na kila aina ya kwata.

Pamoja na umuhimu wake kwata sio mbadala wa stadi za mpira. Stadi kwanza, stamina husaidia. Muda mrefu na mwingi wa mazoezi mchezaji acheze na mpira, kwa kutumia miguu yote miwili.

Vilevile, mashabiki hatuwatendei haki wachezaji wetu. Kumsifia mchezaji huku ukijua hajakamilika kistadi za mpira ni kumvika kilemba cha ukoka, anajihisi staa, hamsikilizi mwalimu, na hafundishiki.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali waelekeze nguvu zao kwenye shule. Wawapatie nyenzo za kujifunzia. Klabu haziwezi kuwekeza katika kufundisha stadi za mpira kwa sababu zinaishi kwa masilahi. Maslahi ya leo sio kesho.

Mwandishi wa makala hii Maurice O. Gama (BA Educ, UDSM; MPA Lawrence, Ks, USA) ni Ofisa Tawala na Mipango wa Chuo Kikuu cha Saint Augustine SLP 674, Mtwara. Anapatikana kwa simu 0784 309 802 na imeili mauricegama@yahoo.co.uk
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)