Hapa wanachezea akili za watu


Edson S. Kamukara's picture

Na Edson S. Kamukara - Imechapwa 08 April 2008

Printer-friendly version

NI dhahiri tumesikia mengi kuhusu ubadhirifu wa mali ya umma na hasa mwishoni mwa mwaka jana ulipoibuka msamiati mpya wa ufisadi.

Lakini haijaeleweka hasa lini Watanzania wataondokana na kizunguzungu kinachowapata cha kuendelea kusikia visa vya mafisadi. Hawajui watafungwa jela au mali zao zitafilisiwa na taifa.

Tulipokuwa 30 Desemba, 2005, wakati akilihutubia bunge jipya kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete aliahidi atapambana na rushwa kwa nguvu zote bila ya kumuonea mtu haya.

Kauli yake ilitafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni simulizi kwa kuwa hata mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, aliwahi kuiita serikali yake ni ya zama za uwazi na ukweli, ingawa mpaka anaondoka Ikulu, mengi alikuwa hajayaweka wazi.

Usiri wa mambo hayo ilikuwa kitendawili kikubwa ambacho ni Mkapa mwenyewe, na wasaidizi wake wachache na matajiri walioneemeka, walifahamu majibu yake.

Rais Kikwete alikuwa na mahali pazuri pa kuanzia kutokana na ushahidi kwamba Watanzania wamekuwa na ujasiri wa kutaja waziwazi wanaowadhani wanufaikaji wakubwa wa raslimali za taifa.

Alipokuwa ziarani mkoani Iringa, Rais aliwahi kusema anawafahamu wala rushwa ila "amewapa muda wajirekebishe," ingawa hakueleza muda huo ungekwisha lini ili awashike makoo.

Yapo maswali yanaulizwa leo: mafisadi hao wamejirekebisha au wamezidisha visa vya kutafuna nchi? Kama hawakujirekebisha, wangalipo au wamekimbia nchi? Na je, waliopo bado nchini wamechukuliwa hatua makini?

Kinachoonekana ni kupewa pole kwa wale wachache wanaolazimika kuachia ngazi ikielezwa kuwa hiyo ni "ajali ya kisiasa" wavumilie.

Serikali inachezea akili za watu katika namna ya kushughulikia kikamilifu mafisadi. Haiwezekani na wala haijapata kutokea popote duniani mtu aibie wananchi Sh. 133 bilioni kwa mwaka mmoja tena katika kitengo kimoja tu katika Benki Kuu yenye vitengo chungu nzima, halafu aachiwe.

Inashangaza wanatengeneza mipango ya malipo hewa ya Sh. 152 bilioni kwa siku na serikali inakaa kimya ikitazama. Ama kweli, hii ni serikali ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

Tuliambiwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Ballali amepoteza mabilioni kwa kusabilia mafisadi waingie na nyaraka bandia na kuchota fedha. Kilichofuatia tukaambiwa anatibiwa Marekani.

Akavuliwa ugavana hukohuko na baadaye tukatangaziwa kuwa amevuliwa hadhi ya diplomasia katika pasipoti yake, uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Marekani.

Kichekesho, mpaka leo hatujaelezwa hatima ya bwana fedha huyu ikoje. Hakuna ofisa wa serikali anayewajibika kufahamisha wananchi taarifa za Dk. Ballali.

Wala wananchi hawajaelezwa kama fedha zile alichukua binafsi au kutokana na maelekezo ya viongozi wakuu anaowajua. Hicho kingali kizungumkuti.

Hayo yamekuja wakati mafisadi wametengeneza mkataba mbaya wa kuwapa kazi wasiyoiweza kampuni ya Richmond ambao mpaka wanauza kazi hiyo kwa watu wengine, walishindwa kutimiza hata asilimia 30 ya mkataba. Hawakufua umeme hata nusu ya megawati 100 zilizohitajika.

Kimya kinapozidi katika masuala muhimu kama haya, maana yake Watanzania wanalazimishwa kusahau matatizo ya nchi yao, badala yake waelekeze nguvu katika kutatua matatizo ya maisha waliyonayo.

Kweli, wanaishi na kulala huku wamejifunika mablanketi kusubiri asubuhi ili watoke kuhangaikia mlo wa siku. Hawana nguvu za kusimama kidete kuwatunga shemere mafisadi ili warudishe fedha za umma na washitakiwe mahakamani.

Fedha hizi zilivyo nyingi, pindi zikirudishwa zitasaidia ununuzi wa vitabu shuleni, utengenezaji madawati ili watoto wachoke kukaa chini mavumbini, tutapeleka maji na umeme vijijini ili kupunguza mzigo wa mama kuendelea kupikia kuni na kuepusha macho yao kuzidi kuwa mekundu.

Tungenunua dawa za hospitalini kwa fedha hizi na tukaongeza nguvu katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wasiofikia umri wa miaka mitano, kuimarisha utafiti dhidi ya ongezeko la malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Wakati tunalia na mafisadi, viongozi hawasemi huu utajiri wanaomiliki katika kipindi kifupi cha miaka miwili ya uongozi, wameupata wapi?

Tatizo la Watanzania ni kucheka mno na viongozi waovu. Wakipita majimboni hiyo mwaka mara moja (maana wengine hawajapita majimboni tangu uchaguzi) wakishatoa visenti vyepesi basi hakuna kama wao. Wanaondoka bila ya kuulizwa.

Tena huja na wake na watoto zao majimboni huku wakitanua kwa magari ya kifahari. Wanasahau kuwa watoto wa wanyonge vijijini wanalala kwa mlo mmoja kwa siku, huku wakienda shule na njaa wakiwa miguu chini.

Inawezekana mafisadi wameachwa makusudi watese maana viongozi tuliowapa dhamana ya kusimamia mali zetu wamechoka kuzilinda na kwa kuona hazina wenyewe, wanajinufaisha na watoto wao.

Wahenga hunena; "mdharau mwiba mguu huota tende," na kumbe hata katika taifa letu, kunafanywa mzaha unaotoa mwanya maalum wa mafisadi kulindwa kama ni watu wema kwa taifa.

Rais Kikwete bado una kazi ya kutekeleza ahadi kuhusu wala rushwa. Amuru wakamatwe haraka badala ya kuwachelewesha ili wafilisiwe mali walizochuma na kushitakiwa. Mbona walalahoi hukamatwa bila ya makosa?

0
No votes yet