Harufu ya mauaji ya kimbari yanukia Zanzibar


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version
Zanzibar

NIMESHINDWA kujizuia kuandika makala juu ya yanayotokea Zanzibar, hivyo najitupa uwanjani. Hata hivyo nitajitahidi kuchagua maneno ya kutumia kwa kuwa wapo watu hodari wa kupandikiza hisia kwa jamii ili kujenga uhalali wa malengo yao binafsi.

Katika makala haya sitataja jina la mtu, nitachambua tu juu ya kinachoendelea Zanzibar. Kwamba sasa vurugu zimeibuka na kuwa ni shughuli halali ya kuupinga Muungano.

Baada ya matukio ya Jumamosi, Jumapili na Jumatatu wiki mbili zilizopita, sura mpya ya mahusiano ya kijamii Zanzibar imejifunua kwa uwazi.

Wapo wanaoficha na kufunika ukweli kwamba shida ya Zanzibar kwa sasa siyo kitu kingine chochote bali ni ile mbegu ya ubaguzi inayozidi kuota mizizi na sasa inaimarika.

Watu wamejiuliza maswali mengi, kwamba kama tatizo ni Muungano, inakuwaje vurugu zinaelekezwa kwenye makanisa na baa? Je, makanisa na baa ni kitambulisho cha Muungano?

Lakini lingine ni suala la kutaka kuwasadikisha watu kuwa kuna kikundi kimoja ndani ya jamii na dini yao wanaodhani kwamba wao ndiyo wazawa wa Zanzibar, kwa hiyo wengine wote ni wa kuja na hawana nafasi wala uhalali wa kuwa visiwani humo, labda hata imani zao ni haramu visiwani humo.

Nitatalii mambo haya; mosi, kuhusishwa kwa dini yaani Ukristo na Muungano na kujumuishwa kwa baa kama suala la Muungano, na pili imani kwamba kuna Wabara waliopo Zanzibar ambao ni kero kwa wanaojiona kuwa ni Wazanzibari halisi.

Dunia inakumbuka mauaji ya kimbari kuwahi kufanywa na utawala wa Kinazi wa Adolf Hitler wa Ujerumani. Hitler aliwaaminisha Wajerumani kwamba kiini cha matatizo yao ni Wayahudi hivyo wakawaua Wayahudi kwa mamilioni.

Taarifa zinasema kwamba kiasi cha Wayahudi milioni tano walilipuliwa kwenye matanuru. Hii ilikuwa kazi ya mikono ya Hitler. Kati ya mwaka 1933-1945, alitekeleza ushenzi usioelezeka dhidi ya ubinadamu.

Mwaka 1994 majirani zetu Rwanda,  kwa siku mia tu, Wahutu wenye msimamo mkali waliwaua kinyama mno Watutsi katika mauaji yaliyotanda nchi nzima.

Walitumia silaha za jadi kuendesha ushenzi huo chini ya uratibu wa watawala wa wakati huo. Huu ni ushenzi wa karibuni kabisa kuwahi kufanywa dhidi ya ubinadamu ambao sisi Watanzania siyo tu kwamba tulisimuliwa au kusikia, ila tulishuhudia miili ya watu waliokatwakatwa vibaya ikielea kwenye mto Rusumo hadi kuingia Ziwa Victoria.

Nimekumbusha mauaji ya kimbari kwa vile anayepanga uhalifu dhidi ya binadamu mwenzake lazima afanye mambo mawili; moja atengeneze utambulisho wa kubaguana, pili utambulisho huo aufungamanishe na shida za jamii kwa wakati huo.

Kwa Zanzibar kinachoonekana shida kwa wanaojiita watetezi wa uhuru wa Zanzibar ni Muungano; huu unatajwa kuwa kiini cha shida zote za Zanzibar, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa hiyo, lazima ung’oke.

Katika harakati hizo, Muungano unafungamanishwa na Ukristo. Kwa nini Muungano unaunganishwa na Ukristo na mambo ya Wabara, ni vigumu kuelewa, ila itoshe tu kusema kwa wanaoamini kuwa wao ni Wazanzibari halisi wanaamini kwamba Muungano umechimbuka ndani ya Ukristo.

Inawezekana wenye fahamu hizi wanazikita zaidi kwa kumtazama mmoja wa waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere, lakini kwa hila za wapinga Muungano na kinyongo kilichopitiliza  hawakumbuki kuwa alikuwako pia muasisi mwenza, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Kwa nia ya kufitinisha umma wa Watanzania hususan Wazanzibari, basi kila lililo baya kuhusu Muungano linabebeshwa na kuvalishwa joho la Ukristo.

Kwao Ukristo ni Bara hawakumbuki kabisa kuwa kuna Waislamu kwa mamilioni wamejaa Bara, kuanzia pwani hadi ncha za mwisho za nchi.

Baa zinafungamanishwa na Bara, ni kazi ya Wabara kutengeneza na kuuza pombe, ni kazi ya Wabara kunywa pombe; kwa maana hiyo kila kwenye baa ni shughuli ya Wabara, kwa hiyo ni shughuli ya wenye Muungano hivyo ni vema na ni haki kuvamia, kupora na kuchoma moto. Teketeza!

Wanaoendesha dhana hii kama ilivyo ya udini, hawana fahamu kwamba hoteli zote kubwa zilizoenea ufukweni mwa visiwa hivyo, zikivutia watalii na kila aina ya wageni kutoka kokote duniani, pamoja na mambo mengine kuna bia na kila aina ya kilevi.

Hoteli hizi si misikiti wala makanisa. Ni vitega uchumi vya mabilioni, ni vitega uchumi vya kimataifa, lakini kwa kuwa siyo za Wabara (nyingi za Wazungu) kwa wahafidhina hawa siyo kitu, siyo Muungano, na ndiyo maana hazikuchomwa moto.

Suala la pili katika kadhia hii ni kuonekana kwa Wabara kama kero, kwa wanaojiona kuwa ni Wazanzibari halisi. Hawa wanaonekana hivyo kwa sababu fikra za waendesha kampeni hizi, ambazo hakika zina kila dalili ya kupanda mbegu ya ubaguzi na kujenga mwelekeo wa mauaji ya kimbari, wanaona na kuwafikiria Wabara kama ndio wafia Muungano; wanawaona Wabara kuwa wanaupenda zaidi Muungano kwa madai wananufaika.

Baada ya kuzungumzia habari ya ufungamanisho wa Muungano na makanisa, baa na Wabara kuufia Muungano, nitajielekeza kwa kifupi juu ya suala la kampeni zinazoendeshwa dhidi ya Muungano kwa kutumia jukwaa la dini.

Miongoni mwa mambo ambayo hadi sasa yanasumbua akili yangu siyo suala la kukataliwa au kukubaliwa kwa Muungano ndani ya jamii, bali ni kuona jukwaa la dini linatumika kama njia ya kutekeleza malengo hayo.

Kwamba dini inaendesha harakati hizo tena hadharani na kwa mbwembwe, wakati inajulikana kabisa suala hilo ni la kisiasa.

Ingelikuwa ni chama cha kisiasa kinaendesha harakati hizi ingeweza kueleweka, lakini dini? Inakuwa shida kidogo kupata mantiki.

Jambo hili sasa linafungua ukurasa mpya juu ya utii wa sheria. Ni kweli kuna uhuru wa maoni kwa mujibu wa katiba, lakini pia kuna uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa katiba.  Dini kutumika kama jukwaa la kisiasa nchi inaelekezwa kwenye maangamizo.

Harakati hizi za dini kuvaa joho la siasa ni maandalizi ya maangamizi. Najua wapo watakaokerwa na ukweli huu, lakini naomba jamii ijiulize hivi kama kuna viongozi wa dini wanatamani sana kupiga siasa kwa nini wasijiunge kwenye vyama  vya siasa kueneza sera za kujitenga kuliko kutumia jukwaa la dini ambalo ni nyeti sana kuendeleza mapambano ya kudai uhuru?

Mwisho niseme tu pamoja na kuwa muumini wa uhuru wa kujieleza na kuitaka dola kuheshimu uhuru huo, nashindwa kujizuia kusema kuwa serikali ya Zanzibar na hata ile ya Muungano katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa legelege sana, hazichukui hatua kuzuia maafa kutokea mpaka ama yawe yametokea au ziwe zimesukumwa na jamii kuchukua hatua.

Tunaambiwa chokochoko zinazoendelea Zanzibar za kudai kuvunjwa kwa Muungano ili Zanzibar ipate uhuru wake hazikuanza jana wala juzi. Vuguvugu hili limekuwako kwa muda mrefu sana, hata kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; lakini kwa wanasiasa wa kizazi cha sasa wanapenda kupongezwa na kufurahisha watu tu, hakuna mwenye ubavu wa kuchukua hatua; mikakati ya kuvunja nchi mapande mapande inafanywa hadharani, lakini watawala wala hawasumbuki.

Kwa waliosoma habari za mauaji ya kimbari kuna taarifa zinazoitwa vielelezo vya awali vya mipango ya mauaji ya kimbari (early warning for genocide); watawala na vyombo vya dola hasa vya usalama vimepewa wajibu wa kukusanya taarifa mapema na kutambua kuwa jamii inanyemelewa na janga husika ili kuchukua hatua stahiki kuepusha balaa hilo.

Nina hakika Zanzibar kuna kusinzia kwingi, nina hakika ndani ya watawala wamo wanaosadia maandalizi hayo. Katika hali kama hii mtu anapashwa kujua wanaodai uhuru kwa mgongo wa dini na wanaachwa tu wanalitakia taifa hili mwisho mbaya. Tafakari.

0
No votes yet