Hata CCM ni ‘chama cha msimu’


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KINYANG’ANYIRO cha uchaguzi kinaendelea nchini kote. Tayari watu makini wameona sura halisi ya uchaguzi itakavyokuwa.

Katika kinyang’ayiro cha urais, ushindani uko kwa wagombea wawili – Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demekorasia na Maendeleo (CHADEMA) na Jakaya Kikwete anayewania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wengine wanasema miamba hiyo miwili – Slaa na Kikwete – inatofautiana kwa kiwango kikubwa. Bila kujali itikadi zao, wanaona kuwa huu ni uchaguzi kati ya umakini na usanii na utendaji na upigaji soga.

Ni uchaguzi kati ya mbunifu, mwadilifu na mzalendo, dhidi ya ufisadi, ukasuku na kikundi kidogo cha mtandao maslahi. Haya yanasemwa na kuonekana kwa matendo na historia za wagombea wenyewe.

Wakati hayo yanatokea katika mijadala rasmi na isiyo rasmi, Kikwete amesikika mara mbili mfululizo akiwaonya wananchi wasivichague vyama vya upinzani kwa madai kuwa ni vya “msimu.”

Kuna haja ya kuangalia kwa makini kauli hii ili wananchi wasijitumbukize katika mchezo mchafu uliowekwa na mgombea huyu anayeonekana kutojali sheria inayounda vyama vya siasa.

Kejeli hii si kwa vyama vya upinzani bali ni kejeli kwa sheria inayounda vyama hivyo. Madhara ya kukejeli sheria ya nchi ni makubwa na hasa kama kejeli hiyo inafanywa na mgombea ambaye ni rais na anagombea ili kurejea katika madaraka ya ofisi hii muhimu kwa usimamizi wa sheria za nchi.

Siyo siri kwamba Rais Kikwete ameweka historia ya kuwa rais anayekebehi utawala wa sheria kwa kudai kwake mara kwa mara kuwa anaheshimu utawala wa sheria.

Kikwete anayetakiwa kuheshimu utawala wa sheria hawezi kamwe kudai vyama vya upinzani ni vyama vya msimu wakati akijua sheria inayounda vyama hivyo ni ileile iliyounda chama chake, na kwa bahati njema, CCM ni moja ya vyama vilivyosajiliwa siku moja sambamba na vyama vingine.

Kama u-msimu wa vyama vya upinzani unatokana na kile kinachoitwa kuonekana wakati wa uchaguzi na kupotea baada ya uchaguzi, basi vyama vyote vya siasa nchini ni vya msimu.

Hii ni kwa sababu, ni wakati huu wa uchaguzi tunashuhudia kuwepo kwa vyama hivyo, kwa ilani na ahadi kemkem kwa wananchi kuwa vitafanya mema endapo vitapewa ridhaa ya kuongoza.

Kwa CCM, u-msimu wake unaonekana hata kwa njia ya kufuru ya matumizi ya fedha zisizo na maelezo, chafu na safi katika kutafuta ridhaa hiyo.

Matumizi haya ya fedha si ya kila siku, wala kila mwaka, bali tunayaona wakati wa msimu wa uchaguzi. Hivi sasa tunaona mabango ya kuinadi CCM mpaka vyooni, magerezani na hata mahakamani.

Tunashuhudia mabango na picha za wagombea wa CCM mbugani, kwenye maroli yaliyobeba magendo, vijiwe vya wauza unga, juu ya shehena za nyara za taifa na hata katika magari ya wagonjwa mahututi yakiwamo yanayotibika, lakini kwa Tanzania yameshindikana.

Kufuru hii ya mabango na picha haipo siku zote. Inapatikana wakati na msimu wa uchaguzi. Je, katika hali hii, nani ni wa msimu kati ya CCM na vyama vya mageuzi?

Tumezoea kuona kwa macho yetu kuwa baada ya kila uchaguzi CCM na vyama vingine hupotea kabisa na kutosikika.

Kwa chama dola kama CCM, ofisi zao ambazo kwa msimu huu zimegeuka kuwa vijiwe vya kugawa rushwa na takrima, baada ya uchaguzi ofisi hizo hugeuka kuwa vijiwe vya kudai na kukusanya rushwa.

Wananchi huzikimbia ofisi za CCM na hata nyingi hufungwa wakati wote au kugeuka kuwa maegesho ya magari na wizi na vipuri vya magari.

Mtu makini hawezi kusema wakati huo ambapo hutumika kuwafisidi wanachama na wananchi, CCM huwa ni chama kinachosimamia mapinduzi kama jina lake. Chama huwa hakipo, bali kundi la maslahi linalotumia jina la chama kupata maslahi binafsi.

Wakati wa uchaguzi, vyama vyote hufufuka, ikiwemo CCM. Huja kwetu na ahadi nyingi, lugha tamu na ahadi za kutupeleka peponi tukiwa hapahapa duniani.

Kama kinavyodai kuwa ni nambari wani, CCM ndicho chama kinachokuja na ahadi nyingi za msimu na za kudumu. Hufika mahali hata mgombea akawauliza wenyeji wa eneo la kampeni, “Mnataka niwaahidi nini kwenye mkutano wa leo?”

Kwa maoni yangu, kinachoitwa “vyama vya msimu,” hakuna msimu unaovuka kiwango kama huu wa kuahidi bila kudhamiria kutimiza kile unachoahidi.

Na kama hicho ndicho kipimo cha “msimu,” basi chama hiki kilichopo ikulu na viongozi wake ndicho kinachoongoza katika vyama vya msimu.

Hata haya tunaoyaona sasa wakati huu wa uchaguzi, ni kielelezo kingine kwamba CCM ni chama cha msimu.

Nani anaweza kusema kwamba chama ambacho hakina huruma, busara, kinachokumbatia rushwa, kilichojaa ubabe, kama si chama cha msimu?

Bila shaka hakuna. Ni kwa sababu, chama ambacho hakitendi kazi zake kwa msimu, hakiwezi kukubali kugeuka genge la watafutaji.

Kada mmoja maarufu na mpiga debe wa chama hiki aliwahi kuniambia. “Huu ni msimu wa mavuno kwa wajanja waliopo ndani ya CCM.”

Akasema huu ndio “msimu” wa kukamua wagombea kwa sababu baada ya uchaguzi hawataonana tena na watakaochaguliwa.

Hivyo basi, kila aliyepo ndani ya CCM hutayarisha orodha yake ya mahitaji binafsi na kuiwasilisha kwa mgombea anayeona kuwa amebahatika kukusanya fedha zaidi.

Anapanga kumalizia ujenzi wa nyumba yake, kulipiwa karo ya watoto wake kwa miaka mitano ijayo, matibabu ya wazazi wake, kusaidiwa katika kesi inayomkabili au kuahidiwa cheo baada ya uchaguzi.

Mwingine aweza kuwa na mipango ya kuhamishiwa kituo kizuri, kununuliwa gari, pikipiki, simu ya kisasa, kijiwe cha biashara, ajira ya kudumu na nyinginezo.

Haya tumeyashuhudia kwa macho yetu katika msimu huu CCM inapoongoza katika medani hii. Katika msimu huu, sheria za nchi na maadili yanayoongoza serikali hupelekwa likizo ya lazima.

Mgombea urais wa CCM aweza kumwahidi mwizi wa mali ya umma kuwa atampa cheo baada ya uchaguzi, wanaogushi na mafisadi huahidiwa nafasi kwa kukichangia chama chake.

Ushindi wa kura za maoni huwa kigezo cha kukubalika badala ya uzalendo kwa nchi, watu na mali zao. Chama kinachojinadi vitabuni kuwa mtetezi wa wanyonge, katika msimu huu hugeuka kuwa mtetezi wa matajiri na wenye mali.

Chama hiki huwageuza wananchi kuwa daraja la kuvukia kuingia katika kinga dhidi ya sheria na madai ya uadilifu. Kwamba ndani ya chama hiki cha msimu, “hakuna kinachoshindikana,” ilimradi uwe na fedha za kununua viongozi.

Kawaida watu hufikiri kabla ya kusema. Lakini Kikwete, mara nyingi, amesema kabla ya kufikiri na matokeo yake ni kusema yasiyotakika, yasiyo na kweli na mara nyingi anaongea mahali ambapo hapahitajiki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: