Hata Kikwete angehamia CHADEMA


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

RAIS Jakaya Kikwete amekuwa akijitolea mfano kila anapozungumzia suala la baadhi ya wagombea nafasi za urais, ubunge na udiwani majina yao kukatwa. Anasema wanatakiwa wavumilivu kama yeye.

Kwanza alijitolea mfano katika mkutano mkuu wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini Dodoma baada ya kumteua na kumpitisha Dk Ali Mohamed Shein kuwa mgombea urais Zanzibar.

Pili alipochukua fomu ya kugombea urais mwaka huu na mara ya tatu alipozungumza na wafuasi wake katika ofisi ndogo za CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, baada ya kurejesha fomu.

Rais Kikwete anasema mwaka 1995 alipowania nafasi ya urais, Benjamin Mkapa ndiye aliteuliwa lakini yeye hakukata tamaa. Alisubiri hadi mwaka 2005 akashinda.

Vijana na hata watu ambao hawakumbuki kilichotokea wakati ule, ni rahisi kuamini maneno ya rais Kikwete na hivyo kuwaona wanaondoka CCM kuwa wasaliti na waroho wa madaraka.

Katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mwaka 1995, walijitokeza wagombea wengi. Miongoni mwao, ni Joseph Warioba, Mark Bomani, Cleopa Msuya, John Malecela, Edward Lowassa, Jakaya Kikwete na Kighoma Ali Malima.

Wengine ni Benjamin Mkapa, Horace Kolimba, Rose Lugendo, Pius Msekwa, Tuntemeke Sanga, Njelu Kasaka na Fred Rutakyamirwa.

Hata kabla ya uteuzi, Mwalimu Julius Nyerere ‘aliwaengua’ wawili, Kolimba na Malecela kwa madai walishindwa kumsaidia Rais Ali Hassan Mwinyi. Aliwatungia kitabu kilichoitwa “Hatima ya Tanzania na Uongozi Wetu.”

Siku chache kabla ya mkutano mkuu wa CCM, Kikwete aliitisha mkutano na waandishi wa habari akamlalamikia aliyekuwa Katibu Mkuu, Lawrence Gama, kwa upendeleo. Hicho kilichochea wapinzani kumwinda.

Baada ya kupiga kura, Kikwete aliongoza kwa kura 534 akifuatiwa na Mkapa aliyepata kura 459 halafu Msuya aliyepata kura 336. Kwa kuwa kanuni inataka mshindi apate zaidi ya asilimia hamsini yaani asilimia 50+, Kikwete hakuwa mshindi.

Katika kura za marudio, Mkapa alipata kura 686 na Kikwete kura 639. Hivyo, hakukuwa na uchakachuaji wa kura kumpata Mkapa kama Kikwete anavyotaka watu waamini.

Habari zikavuma Kolimba kutaka kuhamia upinzani baada ya kuikosoa CCM kuwa imekosa dira. Profesa Malima akahamia NRA, Sanga alitishia kuanzisha chama na Kikwete alishawishiwa ahame upinzani lakini ilidaiwa kuwa alitoa ahadi ya kuingia upinzani baada ya kumalizika mkutano wa uchaguzi.

Taarifa zinasema, kuelekea mwaka 2005, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiilifanya mazungumzo ya siri na Kikwete na inadaiwa ‘aliahidi’ kujiunga nao kama jina lake lingekatwa na vikao vya uteuzi.

Ikumbukwe, hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kingekuwepo chama makini angeihama CCM. Mwalimu alifurahishwa kiasi na CHADEMA, lakini asingejiunga na chama kilichoasisiwa na Edwin Mtei waziri aliyemtimua kazi kwa ‘kosa’ la kukubali kupunguza thamani ya shilingi ili kufufua uchumi.

Uchakachuaji matokeo umekuwa chanzo cha chuki kwa muda mrefu ndani ya CCM. Mathalani, mwaka 1995 Dk. Willibrod Slaa alishinda kura za maoni katika Jimbo la Karatu, lakini wakamwengua bila sababu za msingi. Nafasi yake akapewa Matteo Qaresi.

Wananchi wakamwambia Dk Slaa ahame; tangu mwaka huo CCM ni chama cha upinzani Karatu. Safari hii, Kikwete amesimamia mchakato uliowaengua washindi kadhaa.

Kwa nini walioonewa wasioondoke kama walivyofanya Kasaka na Malima? Kwani maisha yako CCM tu?

Hivi wana-CCM si miongoni mwa makundi makubwa ya watu wanaolilia maisha bora lakini hawayaoni?

Hivi si hao wote wanalia na ufisadi unaolelewa ndani ya CCM?

Kikwete aseme kweli. Wakati alishindwa katika kura za marudio, yeye amewaengua washindi halali kwa madai hawana mvuto na wengine eti si uraia.

Mshindi Jimbo la Nzega, Hussein Bashe, ametangazwa si raia, wa pili, mbunge aliyemaliza muda wake, Lucas Selleli anaambiwa amekosa mvuto; amechukuliwa wa tatu.

Wenye tuhuma chafu za kuuza viungo vya binadamu (albino) wamepitishwa, walionaswa na Takukuru kwa tuhuma za rushwa wamo, lakini NEC imemshupalia Frederick Mwakalebela.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: