Hata mawaziri hawaamini Polisi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

JE, umewahi kujiuliza Jeshi la Polisi haliaminiki kiasi gani na kwa nini? Je, unajua kwamba hata mawaziri wa serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawana imani na Jeshi la Polisi?

Hebu tutazame pamoja kauli za Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe tangu akiwa mbunge tu wa Kyela hadi baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri wa ujenzi.

Tangu Februari 2008, alipowasilisha bungeni ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kampuni ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura, Dk. Mwakyembe pamoja na wabunge waliojitokeza kuwa wapambanaji wa ufisadi, walitoa taarifa kwamba wanatishiwa maisha yao.

Mpaka leo, pamoja na Jeshi la Polisi kupewa namba za simu zilizotumika kutishia uhai, tuhuma hazikufanyiwa kazi, hivyo hakuna aliyenaswa.

Mei, 2009 Dk. Mwakyembe alipopata ajali baada ya gari lake kupinduka eneo la Ihemi mkoani Iringa, polisi walichunguza tukio lile na kutoa ripoti ya ajali ile katika kipindi kifupi.

Dk. Mwakyembe kwanza aliipinga ripoti ile ya polisi na pili akawashangaa kuvunja rekodi kwa kutumia muda mfupi sana kukamilisha kazi ya uchunguzi wa ajali ile. Hakika ripoti ile ilifutwa na haikutolewa nyingine.

Mapema mwaka jana Dk. Mwakyembe alitoa tuhuma nzito dhidi ya watu, aliodai walikuwa wakiifuata roho yake wakifadhiliwa na mfanyabiashara mmoja. Pamoja na tuhuma hizo kuandikwa sana katika vyombo vya habari, polisi hawakuonyesha weledi wa intelejensia na uwezo wa kufuatilia na kuchunguza.

Baadaye Dk. Mwakyembe aliteuliwa kuwa naibu waziri wa ujenzi na aliendelea kuwaambia Watanzania kuwa hana imani na Jeshi la Polisi katika kufanya uchunguzi.

Mfano, alipougua ugonjwa wa “ajabu” na kupelekwa India kwa matibabu,  Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ndiye alipita kila mahali akidai anachougua Dk. Mwakyembe kina uhusiano mkubwa na kulishwa sumu.

Ingawa tuhuma hizo nzito zingelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi haraka na kuwanasa wahalifu, lilikaa kimya. Baada ya kushutumiwa kwa ukimya huo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha (sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), akaibuka na kusema polisi “wanachunguza” suala hilo.

Siku iliyofuata Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba,  akajitokeza na kusema kwamba kadri anavyojua, na kwa mujibu wa taarifa walizopata kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu.

DCI Manumba aliwaaminisha wananchi kwa ujumla kwamba wamefanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba naibu waziri huyo hakuwa amewekewa sumu yoyote isipokuwa alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kawaida.

Lakini aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda, akajiweka kando na taarifa ya DCI Manumba akisema haijui na wala hajui mkurugenzi huyo alikopata ripoti hiyo.

Maelezo haya ya Dk. Mponda yalikuwa yanathibitisha kwamba Jeshi la Polisi limepika ripoti. Dk. Mponda akawataka wote wanaofutilia suala hilo, wamuulize DCI Manumba alikopata taarifa hizo!

Utata; Waziri Shamsi anasema polisi wanachunguza, DCI Manumba anasema wamepata ripoti ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, lakini waziri mhusika anasema hana ripoti hiyo.

Tujiulize, Jeshi la Polisi liliongopa? Kama liliongopa katika suala linalohusu afya ya naibu waziri, litaaminika vipi katika matukio yanayohusu raia wengine likiwemo la kutekwa na kuteswa karibu ya kufa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka?

Mkanganyiko wa suala hilo ulizidi pale Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), ilipojitenga na ripoti kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe.

Badala yake, Ofisi ya Rais ilizitaka wizara mbili zilizoibua mkanganyiko huo; Mambo ya Ndani ya Nchi na Afya na Ustawi wa Jamii, kukaa chini na kuondoa utata huo.

Taarifa ya Ofisi ya Rais iliyotolewa na Stephen Wassira ilimpa nguvu Dk. Mwakyembe ambaye aliandika waraka mzito akausambaza kwenye vyombo vya habari akishangaa ripoti ya polisi. Serikali haikujitokeza tena kuweka sawa suala hilo na kwa desturi, liliachwa lipeperushwe na upepo.

Halafu, Jeshi la Polisi likasema litawahoji na kuwashtaki wale wote walioeneza habari kwamba Dk. Mwakyembe alilishwa sumu. Mlengwa alikuwa Waziri Sitta ambaye hadi leo hajahojiwa wala kuchukuliwa hatua.

Wananchi wanaamini Sitta alikuwa sahihi isipokuwa Polisi walitaka kujikosha. Je, kwa faida ya nani?

Dk. Mwakyembe aliporejea nchini kutoka kwenye matibabu, akazima mjadala juu ya afya yake akisema umefungwa.

Hata hivyo, wasomaji wanaofuatilia kauli za Dk. Mwakyembe watagundua kuwa hajawahi kuwa na imani na Jeshi la Polisi siyo tu alipokuwa mbunge, bali pia alipokuwa waziri.

Kama waziri wa serikali ya CCM hana imani na Jeshi la Polisi; raia, wanasiasa wa upinzani watapata wapi imani na chombo hicho kwa usalama wao?

Kama Dk. Mwakyembe hajawahi kuridhishwa na ripoti ya uchunguzi wa polisi, wananchi wataliaminije katika kuwasaka, kuwatia mbaroni na kuwashtaki watuhumiwa wa kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka?

Kama Dk. Mwakyembe na Dk. Mponda walitilia shaka ripoti ya polisi katika sakata la ugonjwa tu, wananchi waamini vipi weledi wa Jeshi kuichunguza na kuinasa serikali ambayo ni mtuhumiwa namba wani?

Hii ndiyo sababu wanaharakati wanashinikiza iundwe tume huru ya kuchunguza kadhia nzima iliyomkuta Dk. Ulimboka – polisi hawaaminiki.

Katika utetezi wake Rais Jakaya Kikwete anasema kuwa “tumdhuru Dk. Steven Ulimboka ili serikali ipate nini?”

Ipate nini? Jibu ni ili ipate ilichopata – madaktari takriban wote wameingia woga, ‘wamesitisha’ mgomo.

Aidha, Rais Kikwete anasema serikali yake haijamtuma mtu yeyote kwenda kumteka na kumdhuru Dk. Ulimboka. Lengo la kauli hii ni kujiweka mbali na madai kwamba ofisa mmoja wa ikulu anayetumia jina la bandia la Abeid ndiye alifanikisha mpango huo.

Polisi walipokwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) kumwona “mgonjwa maiti”, Dk. Ulimboka alimtambua ofisa wa ngazi ya juu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam aliyempokonya simu na vitu vingine.

Polisi anaowaamini Rais Kikwete, ndio mwaka 2006 walimdanganya kwamba wameua majambazi wanne katika tukio la kurushiana risasi, lakini tume aliyoiunda, ilibaini vijana waliouawa walikuwa wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja wa Dar es Salaam.

Polisi anaowaamini Rais Kikwete ndio wanashindwa hadi sasa kutoa ripoti ya waliotorosha nyara za serikali kutoka hifadhi ya taifa hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro wakapakiwa kwenda Qatar.

Mtuhumiwa wa uhalifu anapokuwa ni serikali, polisi hawawezi kufanya kazi.

0789 383 979
0
Your rating: None Average: 4.5 (6 votes)