Hata mimi nisingejiuzulu ng’o uwaziri


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WAZIRI mmoja wa zamani aliwahi kusema eti shilingi bilioni moja ni vijisenti! Waziri huyo wa zamani alikuwa akizungumzia pesa iliyokutwa kwenye akaunti yake iliyopo kwenye benki moja ya ughaibuni baada ya kutuhumiwa kuhusika na rushwa ya rada.

Kwa sisi ambao tuliwahi kusikia kwamba kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, kulikuwepo wengine ambao suti zao zilikuwa zikifuliwa Uingereza na kwingineko Ulaya, hatukushangaa shilingi bilioni moja kuonekana kwa mwenzetu ni vijisenti tu.

Kulingana na habari hizo ni kwamba, kulikuwapo waziri au mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Mkapa, ambao wao walivaa suti hapa Tanzania mara moja na kuzirundika nyumbani na baadaye zilikunjwa na kusafirishwa kwa DHL hadi London kwa ajili ya kufuliwa na dobi Mzungu!

Kauli ya Mzee wa Vijisenti iliwakera sana wananchi nao wakamlalamikia wakitaka ajiuzulu lakini ilikuwa vigumu kwa vile hakutaka kusikia habari ya kujiuzulu. Hata hivyo, kibano kiliongezeka siku baada ya siku hadi Rais Jakaya Kikwete akamwondoa alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Kilichotokea wiki iliyopita ni ukweli kwamba si mbunge wa Bariadi Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge, pekee aliye katika kundi la wakubwa na wanene serikalini, wanaoona na kudhani kuwa mamilioni ya shilingi ni vijisenti tu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, ni miongoni mwa vigogo wa serikali wanaodhani dola milioni nne yaani karibu shilingi milioni saba za Tanzania ni vijisenti tu.

Kwa wale waliomsikia Naibu Waziri Malima akihojiwa na waandishi wa habari hawawezi kuwa hawakusikia alisema nini alipotakiwa kueleza kama alikuwa na maana gani kuranda Morogoro na mapesa mengi, bunduki na bastola.

Hoja hii isifanye wasomaji wakadhani kuwa mie ni sadist mtu mwenye roho mbaya ninayeshangilia au kufurahia masahibu yaliyompata Waziri Malima mkoani Morogoro ambako wiki iliyopita alipatwa na mkasa wa kuporwa karibu kila kitu katika hoteli aliyofikia tunayoambiwa ni ya kitalii.

Hata hivyo, pamoja na uporaji huo, mporaji au waporaji hawakuchukua silaha za moto alizokuwa nazo Waziri Malima yaani bunduki moja na bastola moja. Kwa ujumla Malima alikuwa na bunduki hizo na pesa taslimu dola za Marekani 4,000, shilingi za Tanzania 1.5 milioni, laptop tatu aina ya DELL na vitu vingine vyote vikifanya jumla ya vitu alivyoibiwa kuwa na thamani ya shilingi 23 milioni.

Kufuatia wizi au uporaji huo maneno mengi yalijitokeza kuhusu nini hasa kilikuwa lengo la wezi au mwizi aliyemwibia Waziri Malima. Kweli wezi waliokubuhu wangeacha bastola? Wezi waliobobea wangeacha bunduki? Jibu ni hapana.

Kama si wezi waliomwibia Mheshimiwa wetu je ni akina nani hao? Majibu yameandikwa mengi kwenye mitandao. Jibu moja lililoshika kasi ni kuwa mwizi alikuwa mmoja tu na kwamba alikuwa mwanamke. Hatuna haja ya kujua mwanamke huyo alifuata nini kwenye chumba cha mtoto wa Kiislam.

Kwa hiyo, mwanamke huyo alipoondoka hakuona haja ya kuacha vijisenti vya Mheshimiwa ndiyo maana akaacha bunduki na bastola kwa vile yeye hakufuata silaha wala kompyuta chumbani kwa Naibu Waziri. Haya si lazima yawe kweli lakini yaweza kuwa kweli pia.

Somo tulilojifunza kutokana na masahibu yaliyomkuta muungwana yule kule Morogoro si kwamba anatembea na bunduki na bastola kujilinda asinyang’anywe vijisenti anavyotembea navyo bali kiwango cha ukwasi wa mawaziri wetu wa serikali ya CCM.

Na huyu ni Naibu Waziri tu! Je mawaziri wanatembea na dola ngapi? Shilingi za Kitanzania ngapi? Na bunduki na bastola ngapi?

Wananchi tungependa kujua kuwa kama Naibu Waziri katika serikali ya CCM anapokuwa ziarani anakuwa na bunduki moja, bastola moja, dola elfu nne na shilingi kibao, je, waziri kamili anaranda na vijienti kiasi gani na silaha ngapi? Kumbe ndiyo maana Chenge akasema ana vijisenti tu !

Sasa siri imetoka hadharani kwamba kumbe mawaziri wetu wana fedha kibao na wanapofanya ziara mikoani wanakuwa na fedha nyingi zikiwamo za kigeni dola za Marekani, yen za Japan, paundi za Uingereza, euro ya Ulaya na fedha za madafu kama shilingi ya Tanzania inavyoitwa mitaani.

Mkasa wa Waziri Malima umeweka hadharani sababu ya mawaziri wa CCM kugoma kujiuzulu hata pale wanapokuwa hawatakiwi na wadau wengine wa wizara na sekta wanazosimamia serikalini. Na hapa niseme wazi kuwa siwalaumu kwa hilo.

Hata mimi nisingependa kuacha nafasi inayonipa fursa ya kupata fedha nyingi na kutembea mikoani na mabunduki na bastola, pesa za kigeni na shilingi za Kitanzania. Kama dola elfu nne ni vijisenti kwake Naibu Waziri Malima, je kwenye akaunti yake CRDB, NBC na BOA kuna dola na shilingi ngapi?

Kwa nini mimi nijiuzulu nikose nafasi ya kuranda na fedha mikoani? Kumbe sasa tumefahamu kwa nini Waziri wa Afya, Haji Mponda na Naibu wake Lucy Nkya wamekataa katakata kujiuzulu pamoja na kelele zote zilizopigwa na wananchi na madaktari. Hawataki kuachia mapesa na bunduki za kujihami.

Nami nawaunga mkono maana ni mjinga pekee atakayekubali kujiuzulu na kuachana na fursa ya kuranda na shangingi mikoani, dola elfu nne mkobani na shilingi lukuki kwenye mfuko wa suruali. Bila kusahau bunduki begani na bastola kiunoni! Mungu akupe nini, akupe kidonda?

Na kwa mtindo huu watakufa au kuuliwa watu wengi Songea na hakuna mtu, si Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wala Mkuu wa Wilaya atakayejiuzulu. Ajiuzulu ili iweje wakati hatuna utamaduni wa kujiuzulu na kupoteza haki ya kuranda na vijisenti mkobani, shilingi mfukoni, bunduki begani na bastola kiunoni kama alivyokutwa Malima ?

Waandamanaji watafyekwa kwa risasi Arusha wakiwamo makanika wanaotengeneza magari Sakina na Wakenya wanaofua nguo walikofikia na bado hakuna atakayejiuzulu. Ya nini kujiuzulu wakati si tabia wala desturi yetu kujiuzulu ?

Polisi wataua watu wengi migodini, watakimbia na majeneza na kuyabwaga barabarani huko Nyamongo na hakuna atakayejiuzulu kwa sababu kufanya hivyo ni kujikosesha haki ya mapesa ya kigeni na shilingi na haki ya kulala hotelini umezungukwa na wale uwapendao kwa gharama ya walipa kodi.

Kwa mtindo huu, Walahi wa bilahi hata mimi sasa napenda kuwa waziri. Bahati mbaya mtu wa kuniteua hayupo kwa sababu nalalamikiwa eti mie mshambenga na mnoko.

0
No votes yet