Hatimaye baba mzazi wa Rais Joseph Kabila amejulikana


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Siyo Laurent Desire Kabila
Adrien Christofer Kanambe, baba yake Rais Joseph Kabila

Ule msemo kwamba ukweli daima unashinda, sasa umekamilika. Mtu anaweza kudanganya kwa muda mfupi ila si mara zote; na mdomo wa kweli utathibitishwa milele, bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

Ule uongo ulioimbwa na kuwa pambio ndani na nje ya DR Congo, eti hayati Laurent Kabila ndiye baba mzazi wa Rais Joseph Kabila sasa umefikia tamati. Hatimaye baba mzazi halisi wa Rais Joseph amefahamika rasmi.

Ni muda mrefu sasa, takribani miaka kumi na moja, Wakongomani wamekuwa wakisema kwamba, Rais Joseph Kabila si Mkongomani bali ni raia wa Rwanda wa kabila la Kitusi – kwa baba na mama.

Walisema nchi yao imevamiwa na kutawaliwa na Mnyarwanda Mtusi wa Rwanda. Lakini madai yao mara zote yalipuuzwa na nchi ambazo hazitaki ukweli huu ufahamike kwa kuwa zinanufaika na uongo huu.

Nchi hizo zimekuwa mstari wa mbele kupotosha ukweli kuhusu uhalali wa Kikongomani wa Joseph Kabila. Kuna madai kuwa nchi hizo pia ziko tayari “hata kuangamiza yeyote atakayesema ukweli kuhusu Joseph Kabila.”
Kuna msemo uendao hivi: Kutokutaka kujua jambo fulani ni huzuni kubwa na ni msiba mwingine.

Mtu anaweza kukataa kuamini jambo fulani kwa makusudi huku akijua jambo hilo lina ukweli. Ila kwa sababu, ama ya ushabiki au maslahi aliyonayo kwa jambo hilo, atalitetea kwa nguvu zote; hata kama ni uovu, alimradi lisifahamike na kupoteza maslahi aliyonayo kwa jambo hilo.

Lakini ifikapo siku kwa jambo hilo kuwa dhahiri, hakuna awezaye kuzuia ukweli usifahamike. Hapo ndipo panapotokea kizungumkuti, kwamba ukweli sasa ni lazima ujulikane.

Haya ndiyo yametokea kwa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Sasa yamefumuka madai mazito kwamba alijipachika baba wa bandia na mama wa bandia ili aitawale Kongo.

Madai yanakwenda mbali. Kwamba kwa kufanya hivyo, amevunja sheria za nchi hiyo na Ibara ya 72(i) ya Katiba ya Kongo.

Gazeti la Oeil du Patriote, yaani Jicho la Mzalendo ambalo hutolewa mjini Paris, Ufaransa, limegundua picha ya baba yake mzazi wa Rais Joseph Kabila.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, baba yake mzazi anaitwa Adrien Christofer Kanambe. Mama yake halisi anaitwa Macelina. Sasa jina la Joseph Kabila lilitokea wapi?

Kuna taarifa kuwa jina hilo lilizuka wakati wa vita vilivyoongozwa na umoja wa kidemokrasia (AFDL) wa kukomboa Kongo chini ya Laurent Kabila; akitokea Rwanda. Kabila na wenzake walikuwa wamedhamiria kumng’oa Rais Mobutu Sese Seko.

Hii ilikuwa baada ya kuuteka mji wa Kisangani. Inaelezwa kuwa baada ya ushindi huo mwaka 1996, ndipo Joseph alishauriwa kubadili majina yake ya mwanzo.

Kuna madai kuwa wazo la kubadili majina lilitoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda, kupitia kwa mkuu wake wa majeshi wakati huo hadi sasa, James Kabarebe ambaye alikuwa mwalimu na mwelekezaji mkuu wa Joseph.

Akiwa msukaji mkubwa wa “mipango ya Watusi kutaka kuikalia Kongo,” Kagame anadaiwa kushauri Joseph aachane na majina yake halali ya Hypolite Christofer Kanambe; na badala yake ajiite Joseph Kabila.

Picha ya pamoja na Adrien Christofer Kanambe, baba yake mzazi na viongozi wa Jeshi la Ukombozi wa Congo (CNL) ilipigwa manamo miaka ya 1964 katika mji wa Albertville, Kalemie katika mkoa wa Katanga.

Kutoka kushoto kwenda kulia ni Jean Sebastien Ramadhani, Laurent Desire Kabila, Gaston Soumialot na Adrien Christofer Kanambe.

Kwa mujibu wa shirika la Sipa Press, picha ya Adrien Christofer Kanambe ni ya kweli na kwa sasa iko kwenye “Facebook.”
Utafiti wa kina uliofanywa na Oeil de Patriote, uliwezesha kujua ni mazingira yapi ya kihistoria yalisababisha viongozi hawa wa CNL (Conseil National de Liberation) wakawa kwenye picha ya pamoja na Adrien Christofer Kanambe.

Matokeo sahihi ya utafiti yalitokana na kugundulika kwa nyaraka za siri za chama cha PRP – Part de la Revolution du Peuple kilichoundwa na Laurent Kabila tarehe 24 Oktoba 1967 ambako inaelezwa kuwa Adrien Christofer Kanambe alikuwa mshirika wake wa karibu.

Adrien Christofer Kanambe, baba yake Rais Joseph Kabila alitokea wapi? Ni mtu wa namna gani? Mazingira yapi yalimtoa Rwanda na kujikuta yuko Kongo akishirikiana na akina Laurent Kabila katika mapambano ya ukombozi wa Kongo?

Kwanza, Adrien Christofer Kanambe ni miongozi mwa wakimbizi wa Kitusi walioikimbia Rwanda miaka ya 1958 baada ya Gregoire Kahibanda, Muhutu kuipindua nchi hiyo na kuitawala.

Mamia kwa maelfu ya Watusi walikimbilia Kongo na kuweka ngome Mashariki mwa nchi hiyo. Wengine walikwenda Uganda, Burundi na Tanzania. Hawa ndio leo wanajiita Wanyamulenge wa Congo.

Hii ndio sababu Wakongomani wanasema Nchi za Maziwa Makuu za Afrika ya Kati na Afrika Mashariki zilizopokea wimbi la Watusi miaka ya 1950 na 1960, zikae chonjo; kwani yanayofanyika Congo leo yatawakumba pia.

Tarehe 26-27/05/1964, usiku wa manane, mji wa Kalemie ulitekwa na watu watatu waliojiita Les Trio - Kabila, Kabuto na Masengo, ambao walisaidiwa na majeshi ya serikali yaliyoasi.

Baada ya Laurent Kabila na wenzie wawili, Kabulo na Masengo kuuteka mji wa Kalemie tarehe 26 hadi 27/05/1964, walikosa msaada wa kijeshi waliotarajia kutoka kwa Gaston Soumialot aliyekuwa mkuu wa operesheni ya CNL.

Tarehe 28/05/1964 majeshi ya serikali – Armée National Congolais (ANC) yakiongozwa na Mobutu yaliuvamia mji wa Kalemie na kuutwaa tena.

Les Trio – Kabila, Kabulo, Masengo – walihamishia kamati zao za kimapinduzi katika milima ya Kankomba na kuanzisha operesheni ya kuwakamata viongozi wote wa serikali katika mkoa wa Katanga ya Kasikazini.

Bwana Jonson Sendwe aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kalimie pamoja na Meja Ndala waliangukia mikononi mwa akina Kabila na kuuliwa.

Tarehe 19 Juni 1964 majeshi ya Gaston Soumialot ya Simba-Mulele yaliuvamia mji wa Kalemie na kuutwaa tena upya toka mikononi mwa akina Mobutu.

Tarehe 31Juni 1964, Gaston Soumialot kiongozi wa CNL alisaini mkataba wa kijeshi na chama cha Kitusi cha UNAR – Union National Rwandaise, chama cha upinzani kilichoundwa na wakimbizi wa Kitusi waliokimbilia Congo miaka ya 1958.

Hawa waliweka ngome yao Kivu ya Kusini wakiongozwa na François Rukeva, Mnyarwanda Mtusi. Lengo ni kujiimarisha nchini Congo na kurudi kwao Rwanda, kupindua serikali ya Gregoire Kahibanda, Muhutu.

Mkataba wa kijeshi kati ya Gaston Soumialot na François Rukeva – kiongozi wa chama cha Kitusi cha UNAR – ni sawa na ule wa Yoweri Museveni na akina Paul Kagame nchini Uganda wenye sharti la: “Tutakusaidia kutwaa madaraka, nawe utatusaidia baadaye.”

Gaston Soumialot  wa CNL na François Rukeva wa UNAR, baada ya kusaini mkabata wa kumng’oa Rais Kasavubu (1960 – 61) na akina Mobutu, kwa upande mmoja; na Rais Gregoire Kahibanda kwa upande mwingine; ndipo akateuliwa Adrien Christofer Kanambe kuwa mwakilishi wa chama cha Kitusi, UNAR kwenye muungano wa CNL.

Tarehe 31 Julai 1964, Adrien Kristofer Kanambe (baba mzazi wa Joseph Kabila), alipigwa picha ya pamoja na viongozi wa CNL alipokuwa akitambulishwa kwa raia wa mji wa Kalemie kama mwakilishi wa UNAR kwenye muungano na CNL.

Adrien Christofer Kanambe na baadhi ya askari wa Kitusi walibaki katika medani ya Kivu ya Kusini pamoja na majeshi ya CNL hadi walipofika akina Che Guevara, Aprili 1965.

Ujio wa Che Guevara na wenzake ambao walipitia Tanzania, ulilenga kusaidia wafuasi wa Patrice Lumumba waliokuwa wakipambana na majeshi ya kibeberu nchini Congo.

Adrien Christofer Kanambe na askari wake waliungana kwa pamoja na majeshi ya CNL-SIMBA –MULELE na yale ya Cuba yakiongozwa na Che Guevara kwenye mapambano ya ukombozi Mashariki mwa Kongo hadi Februari 1966.

Mapambano ya kumng’oa Mobutu hayakuzaa matunda baada ya Laurent Kabila kutoelewana na kiongozi wake Gaston Soumialot kwenye uwanja wa mapambano.

Hapa ndipo Che Guevara aliamua kuondoka na askari wake akaelekea Bolivia kusaidia raia wa nchi hiyo waliokuwa kwenye mapambano ya kuikomboa nchi yao kutoka makucha ya ubeberu.

Tarehe 24 Oktoba 1967, kwenye kijiji cha Makanga-Tubaone, Laurent Kabila aliunda chama chake cha PRP (Parti de la Revolution du People). Alimteua Adrien Christofer Kanambe kuwa mjumbe wa  Kamati Kuu ya chama chake, mkuu wa majeshi yake na mjumbe wa kudumu wa chombo cha ushauri cha kijeshi.

Wakati huo Gaston Soupialot ameachana na akina Laurent Kabila, muungano wa CNL na UNAR umetoweka, Adrien Christofer Kanambe hakuweza kurudi tena kwenye muungano. Akaamua kuambatana na Laurent Kabila.

Mwaka 1984 majeshi ya Laurent Kabila yakiongozwa na akina Adrien Christofer Kanambe, Kaliste Majaliwa na Jenerali Sylivester Lweca, walivamia mji wa Moba, lakini walivurumishwa na majeshi ya Mobutu. Mwaka 1985 walivamia tena Moba na kwa mara nyingine kuvurumishwa na Mobutu.

Wakati huo, Adrien Christofer Kanambe alikuwa na mke wake aitwaye Macelina Kanambe, mama yake mzazi Hypolite Adrien Christofer Kanambe ambaye ndiye Joseph Kabila wa sasa.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Laurent Kabila na mkewe Sifa Mahanya ni wazazi wa bandia wa Rais Joseph Kabila.

Adrien Christofer Kanambe na wenzake, alihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi ya PRP – chama cha kijeshi cha Laurent Kabila. Walituhumiwa usaliti kwenye vita vya Moba ambako, chini ya Kanambe, majeshi yake yalipigwa mara mbili.

Baada ya kifo chake, Laurent Kabila alimchukua mke wa Kanambe, Macelina pamoja na watoto wake wawili – Hypolite na dada yake (jina halijapatikana) – akawabeba na kuwabwaga kitongoji cha Msasani, jijini Dar es Salaam. Laurent Kabila akamtwaa Macelina kama mke wake.

Kuna sababu gani ya dunia kutojua ukweli huu, kwamba mtu wa taifa jingine; uraia mwingine kabisa, anaweza kuwa rais wa nchi nyingine? Joseph Kabila.

0
Your rating: None Average: 3.8 (9 votes)