Hatimaye Stella amfikia Waziri Mkuu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameingia kijijini Ubungo Msewe kwa kutaka ripoti kamili ya ufuatiliaji tuhuma mbalimbali zilizofikishwa kwake, MwanaHALISI imefahamishwa.

Taarifa zimeeleza kwamba Pinda amekutana na Stella Kajuna, mwanamke aliyefichua uhalifu unaofanywa katika kijiji cha Msewe, mkoani Dar es Salaam, ukidaiwa kusimamiwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.

Malalamiko ya Stella kwa Waziri Mkuu, yamejikita zaidi katika malalamiko yake ambayo anasema polisi kituo cha Mbezi kwa Yusuf hawajayashughulikia.

Moja ya malalamiko hayo ni lile linalohusu kubakwa kwa mwanafunzi wa kike wa Kidato cha Pili ambaye anadai alimlea tangu akiwa na umri wa miaka miwili.

Tayari kwa maelekezo ya waziri mkuu, suala la Stella limeanza kushughulikiwa upya. Mapema wiki iliyopita mwanamke huyo alihojiwa kwa siku mbili mfululizo na ofisi ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Stella, muimbaji maarufu wa nyimbo za injili anayejulikana zaidi kwa jina la Stella Joel, anasema Jeshi la Polisi limeshindwa kushughulikia suala hilo kwa muda mrefu.

Anasema badala yake, baadhi ya askari wamekuwa wakishirikiana na watuhumiwa kijijini Msewe kumbughudhi na hata kudiriki kumfungulia mashitaka bandia.

Malalamiko matatu ya Stella yanamhusu kijana aitwaye Alfred Laizer, anayetuhumiwa kumbaka mtoto wa Stella. Msichana huyo hivi sasa ameacha shule baada ya kuwa amewekwa kimada kwa muda mrefu.

Malalamiko ya Stella, yakiwemo lile la kushambulia na kujeruhi pamoja na kuharibu mali, yalifunguliwa kwa kumbukumbu UDSM/RB/2636 ya mwaka 2006, KMR/RB/6801 na KMR/RB/6824 za mwaka 2007.

Stella amelalamika kuwa alipigwa na askari wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu na hakuna hatua iliyochukuliwa hadi leo.

Mlalamikaji anasadikiwa kumwambia waziri mkuu kuwa mbinu zote za kuua kesi dhidi ya Laizer, zinafanywa na polisi kutokana na shinikizo la mama yake, Rose Laizer, mtumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kutokana na Stella kuendelea kufuatilia kesi zake, anadai kutungiwa kesi ya kutishia kwa maneno kuwaua Rose na mwanawe Alfred.

Kesi dhidi ya Stella ilifunguliwa na kutajwa haraka na kusababisha awekwe mababusu ya Segerea, licha ya kutimiza masharti ya kawaida ya dhamana. Alikaa mahabusi kwa siku tatu kabla ya kuachiwa.

Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa Msewe, Jafari Nyaigesha, amekuwa akitajwa kama mhimili mkuu wa uhalifu unaotendeka Msewe.

Stella ameamua kuendelea kufuatilia malalamiko yake dhidi ya Nyaigesha, kiongozi aliyeshinda uchaguzi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ameandaa malalamiko mapya dhidi ya Nyaigesha, akimwandikia Kamishna Alfred Tibaigana kutaka hatua za kisheria zichukuliwe.

Nyaigesha anatuhumiwa kukalia kesi zote za Stella na kuzitumia kwa maslahi binafsi.

Stella anadai Nyaigesha amevunja nyumba yake na baada ya kuingia, alitoka na hati za kununulia nyumba hiyo. Inadaiwa tayari ameshazigonga mihuri na saini, ishara ya kuonyesha kuwa yeye ndiye mmiliki halali.

Malalamiko ya Stella yamewahi kufikishwa Wizara ya Usalama wa Raia, chini ya Waziri Bakari Mwapachu. Wizara ilitoa maelekezo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Jinai wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCIO), kuyafuatilia, lakini Stella hajapokea taarifa yoyote zaidi.

MwanaHALISI imewahi kuonana na Kamishna Tibaigana, na kumueleza matatizo yalioko Msewe na namna Stella, aliyeyafichua anavyoandamwa.

Mkuu wa Upelelezi wa Kanda, alifuatilia malalamiko hayo kwa kuagiza apatiwe majalada ya kesi za Stella, lakini mlalamikaji huyo hajaelezwa maendeleo ya uchunguzi huo.

Gazeti hili lina vielelezo mbalimbali vya malalamiko ya Stella na wakazi wengine wa Msewe, lakini haijafahamika nini kinachokwamisha hatua zote hizo.

Kwa kuona mazingira hayo, Pinda amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kufuatilia malalamiko hayo. Naye waziri amemwelekeza Naibu wake, Balozi Khamis Kagasheki, kufuatilia suala hilo.

MwanaHALISI imeona barua ya Balozi Kagasheki akimuarifu Stella kuvuta subira wakati suala lake linafuatiliwa na ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

"Naamini haitachukua muda mrefu kutokana na kumbukumbu zetu kuonyesha (suala hili) lilishaanza kushughulikiwa," anasema katika barua ya 31 Machi 2008 yenye Kumb. Na. AB 102/349/01/27.

Kijiji cha Msewe, kinachokaliwa na wakazi wa kada tofauti, wakiwemo walimu na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kiko jimbo la Ubungo, linalowakilishwa na Charles Keenja (Mb).

Katia hatua nyingine, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Msewe, Nyaigesha, amewahi kuthibitishwa kwa tabia chafu na Baraza la Kata Ubungo, baada ya kulalamikiwa.

Malalamiko hayo yalifunguliwa na Renatus Paisi akimtuhumu Nyaigesha na Joseph Shabani kuuza kiwanja kisicho chake, 9 Februari 2002.

Mwenyekiti wa Baraza la Kata, Aureus Mbepela, katika uamuzi wake wa kurasa tano, amesema Nyaigesha ni mtu "asiyeeleweka" kutokana na kujihusisha kwa karibu na kesi ya kuuza kiwanja.

"Baraza linamwona na hatia kwa matendo na kauli alizotoa na kusababisha kiwanja husika kiuzwe bila idhini?. Baraza linapendekeza kwenye mamlaka iliyo juu ya Serikali ya Mtaa kumchukulia hatua zinazostahili," imeelezwa.

Mbali na kesi hiyo, Nyaigesha amelalamikiwa na wakazi wa Msewe kwa kuuza viwanja na mashamba, likiwemo la Christina Misana ambaye hatimaye nyumba yake ilibomolewa.

Wakati waziri mkuu ameagiza malalamiko ya Stella yafuatiliwe na polisi kwa karibu zaidi, Nyaigesha tayari anasemekana kuhojiwa na polisi pia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: