Hatma ya Warioba mikononi mwa JK


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Mashata dhidi yake yaiva
Jaji Joseph  Warioba

SERIKALI inakamilisha taratibu za kumfikisha mahakamani Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, MwanaHALISI limegundua.

Waziri mkuu huyo wa zamani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mwananchi Gold Limited (MGL) ya Dar es Salaam.

Jaji Warioba anatakiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma juu ya matumizi ya mabilioni ya shilingi ambayo kampuni yake ilichukua kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Taarifa zilizopatikana juzi usiku zilieleza kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ilikuwa tayari imewasilisha jalada la uchunguzi kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua za mwisho.

Tuhuma zinazomkabili Warioba zipo katika maeneo mawili. Kwanza, ni kama fedha zilizotoka BoT zilipitia mkondo sahihi na halali; na pili, kama fedha hizo zilitumiwa kama ilivyotarajiwa.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa MGL ilichukua dola 5,512,398.55 (sawa na Sh. 6 bilioni) kutoka BoT.

Ni upatikanaji wa sehemu ya kiasi hiki cha fedha na utata katika matumizi yake ambavyo vinaweza kumfikisha Warioba mahakamani wakati wowote kutoka sasa.

Pamoja na kuwa mwenyekiti wa bodi, Warioba pia ana hisa katika Kampuni ya Mwananchi Gold Ltd.

Hisa zake zinapitia kwenye kampuni ya familia yake inayoitwa Umoja Entertainment Limited.

Wengine wenye hisa ni Vulfrida Mahalu kupitia kampuni ya familia yao iitwayo VMB Ltd.; Yusuf Mushi kupitia kampuni ya Y.M. Limited na CCM Trust ambayo taarifa zinaonyesha kuwa inamilikiwa na Warioba na Mushi.

Makampuni haya manne ndiyo yanaunda kampuni ya Mwananchi Trust Limited yenye hisa 1,123 katika Mwananchi Gold Limited.

Kwa mujibu wa nyaraka za Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA), wenye hisa wengine katika Mwananchi Gold Limited, ni BoT yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lenye hisa 375 na Chimera Company Limited (ya raia wa Italia) yenye hisa 500.

Habari za kuaminika kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) zinasema mipango ya kumfikisha Warioba mahakamani tayari imekamilika.

Warioba ndiye aliongoza Tume ya Kuchunguza Rushwa (Tume ya Warioba), iliyoundwa na Rais Benjamin Mkapa mara baada ya kuingia madarakani Oktoba 1995.

Kampuni ya Mwananchi Gold Limited, ilianzishwa na serikali kwa lengo la kusafisha dhahabu inayochimbwa nchini.

Lengo la Serikali la kuingia ubia katika kampuni hiyo lilikuwa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo ambapo matarajio yalilenga uuzaji wa asilimia 85 ya dhahabu katika bei ya soko la dunia.

Hata hivyo, miezi miwili iliyopita, Warioba alinukuliwa akimweleza mwandani wake kuwa ana nyaraka zote zinazohusu  matumizi ya fedha zilizoingia kwenye Mwananchi Gold Limited na kwamba haki yake ya kujieleza ikizingatiwa, atajieleza “vizuri tu.”

Mapema mwaka huu, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe aliwaambia waandishi wa habari kuwa, “Kama Warioba hana kosa, hofu ya nini?”

Alikuwa akijibu madai ya Warioba kuwa anasumbuliwa sana na anatishiwa kukamatwa na kushitakiwa. Alisema, “Kama wanataka kunikamata si wanikamate?”

Lakini taarifa za kuaminika zinasema Chikawe “alimuuma sikio” raia mmoja wa Tanzania anayeishi nje ya nchi akisema, “Lazima Warioba atafikishwa mahakamani.”

Aidha, Jaji Warioba alipoulizwa juzi Jumatatu, kuhusu hatua ya kufikishwa mahakamani wakati wowote sasa alisema, “Ah, sijui wanataka nini, maana mambo haya nimeshaeleza na naona kama yameisha.”

Naye DPP, Eliezer Feleshi alipoulizwa na gazeti hili kuhusu taarifa hizi, aliuliza haraka, “Wewe amekwambia nani haya?”

Alipoambiwa ni taarifa kutoka vyanzo vya habari vya gazeti, alisema yeye yuko safarini na kuongeza, “Basi nitafute keshokutwa Jumatano (leo).”

Ofisa mmoja mwandamizi wa TAKUKURU ameithibitishia MwanaHALISI  kwamba kesi ya Mwananchi Gold Limited ipo mbioni kukamilika.

Naye Msemaji wa Wizara ya Sheria na Katiba, Omega Ngolle alipoulizwa juu ya mipango ya kumfikisha Warioba mahakamani, alisema yupo nje ya ofisi kikazi.

“Nipo Shinyanga kikazi; mafaili yapo ofisini. Haya mambo ya lini Warioba atafikishwa mahakamani, siwezi kuyajua ndugu yangu. Nakuomba uwasiliane na DPP Feleshi, atakueleza,” alisema Ngolle.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Edward Hosea, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: