Hatua ya Marando sahihi


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version

UCHAGUZI mdogo wa jimbo la Tarime umeanza kuonyesha athari zake katika siasa za upinzani. Tayari mtafaruku umeukumba uongozi wa chama cha upinzani nchini cha NCCR Mageuzi.

Mwanasiasa maarufu wa chama hicho ambaye pia ni mmoja wa waasisi wake, na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mabere Marando, alitoa maoni yake wiki iliyopita kuwa chama chake hakikupasa kusimamisha mgombea Tarime.

Kwa kauli hiyo, tayari imeeleweka kuwa hakushirikishwa, kama mmoja wa viongozi wa chama na mwasisi, katika mchakato wa kuteua mgombea wa chama hicho.  

Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua kwa nini hakwenda Tarime kumpigia debe mgombea wa chama chake, Marando alitoa sababu mbili kuu.

Kwanza, kwamba hakwenda Tarime kwa sababu NCCR-Mageuzi haina ufuasi mkubwa katika jimbo hilo ukilinganisha na Chadema au CCM.

Pili, kwamba ili kuhakikisha upinzani unanyakua tena jimbo hilo, chama chake kilipaswa kuweka nguvu zake kwa mgombea wa Chadema.

Hayo ni maoni ya Marando kama mtu yeyote ambavyo angetoa maoni. Lakini kauli yake imepingwa na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, George Kahangwa.

Kahangwa amefika mbali na kusema Marando ni msaliti wa chama chake; kwa kuwa katoa maoni yake kuhusu hali ya kisiasa Tarime.
 
Ni dhahiri kwamba “ushirikiano” baina ya vyama vinne vya upinzani – Chadema, NCCR, CUF na TLP uliobuniwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita sasa, umekufa.

Kufa kwa ushirikiano huo kulianza kuonekana baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime (Chadema), Chacha Wangwe katika ajali ya gari Kongwa, mkoani Dodoma.

Kifo cha ushirikiano wa vyama vinne ni msiba mkubwa sana kwa wapinzani na wananchi kwa ujumla. Kushindwa kwa vyama hivyo kushirikiana kunaweza kurahisisha jimbo hilo kuchukuliwa na chama tawala.

Na chama tawala hakihitaji jimbo hilo kwa shughuli yoyote ile, bali kudhihirisha ubabe wake; kutishia vyama vingine kuwa kina nguvu na kueneza propaganda zake kuwa bado kinakubalika.

Aidha, kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime – Cahcha Wangwe – na hatimaye uchaguzi, hivi sasa vinatumiwa na chama tawala kama jukwaa la kutetea mafisadi – kukataa kuwafungulia mashitaka.

Lakini si mara ya kwanza kwa NCCR, chini ya uenyekiti wa James Mbatia, kuchukua hatua zinazonufaisha CCM.

Chini ya Mbatia, NCCR imewahi kuingia katika uchaguzi mdogo kisiwani Pemba, mwaka 2003. Badala ya chama hicho kujikita jimbo la Kigoma Kusini ambako mbunge wao pekee alikuwa anajaribu kurudi bungeni, wao wakakimbilia Pemba.

Huko Pemba, NCCR haikuwa na ufuasi wowote. Ilikuwa ni kufyatua risasi gizani bila kujua kama utaua mkeo, mumeo, mtoto wako, baba mkwe, rafiki au jirani.

Ufyatuaji wa aina hii huwa umelenga kukidhi hamu ya kufyatua na matakwa ya waliokupa bunduki na risasi.

Kilichotokea ni kwamba, nguvu ambazo zingetumika kurejesha Kifu Gulamhussein Kifu wa Kigoma bungeni, ziliishia kwenye mwamba wa Pemba. NCCR ilishindwa Pemba na Kigoma.
 
Historia inaendelea kurekodi kwamba ni Mbatia wa NCCR aliyeweka pingamizi kwa wagombea watano wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao hatimaye walienguliwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa maelezo kuwa wamekosa sifa.

Kuondolewa kwa wagombea wa CUF, dakika za mwisho, kulisababisha kinyang’anyiro kubakia baina ya wagombea wa CCM, NCCR ambayo ilikuwa haina ufuasi Pemba na vyama vingine vidogo.

Hapa, historia iliandikwa pia, kwamba CCM ambayo ni mshindani mkuu wa CUF kisiwani Pemba, haikuweka pingamizi; pingamizi liliwekwa na NCCR isiyokuwa na wafuasi wa maana Pemba.

Hatua hii ilineemesha CCM na kunawirisha unafiki kwamba kwa CCM kutoweka pingamizi, basi ilikuwa inaendeleza moyo wa muwafaka kati yake na CUF.

Matokeo ya hatua ya NCCR yalinufaisha CCM na wengi wakajenga hisia kwamba Mbatia alikuwa akitekeleza mradi wa CCM Pemba; hata kama yeye binafsi na wenzake walikuwa hawaamini hivyo.

Aidha, katika mikutano yake ya kampeni, Mbatia alikuwa akitamka waziwazi kuwa kule Pemba viongozi wa CUF ni wakorofi, wanawanyima wananchi wengine uhuru wa kidemokrasia kwa kukataa kwao chama kingine kisijikite kule.

Katika kampeni, NCCR ilidanganyika kutokana na wingi wa wananchi wa Pemba waliokuwa wanahudhuria mikutano na kudhani kuwa watapata angalau mbunge mmoja au wawili.

Ni katika uchaguzi huo wa Pemba ulipatikana msamiati mpya katika siasa unaoendelea kujulikana kama “kura za maruhani.” Hizi ni kura ambazo wananchi waliamua kuwapigia wale ambao majina yao yalikuwa yamekatwa na tume ya uchaguzi.

Leo yametokea Tarime. Ni kweli kwamba NCCR ina wenyeviti wa vitongoji wengi kuliko Chadema, lakini ni wenyeviti haohao waliompigia kura mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri ya Tarime kutoka Chadema ambaye ndiye anagombea ubunge sasa.

Hata hivyo, ukweli wa kauli ya Marando kwamba chama hicho hakina mizizi ya kushinda uchaguzi tofauti na Chadema itaonekana muda si mrefu.

Marando hakusema NCCR itashindwa. Alichosema ni kwamba upepo wa sasa na kina cha uelewa, vinaelekea zaidi Chadema kuliko NCCR na kwamba vyama hivi viwili, vingekuwa pamoja, matokeo yangekuwa bora zaidi kwa upinzani.

Kwamba hakwenda Tarime ili asiharibu kura za Chadema kwa upande mmoja na kura za NCCR kwa upande mwingine, bado ni hatua ya kuwezesha kimojawapo kuimarika zaidi na kupata ushind dhidi ya chama tawala.

Lakini kama vyama hivyo vingeshirikiana uwanjani Tarime, Yusufu Mkamba, Katibu Mkuu wa CCM na Mkamu Mwenyekiti Pius Msekwa, wangekuwa wamerejea Dodoma zamani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: