Hatujafanikiwa kujisimamia


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUNAPOTAFAKARI hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika 25 Oktoba nchini kote, tunabaki kujiuliza, "Hivi kweli itafika siku tujivune mbele za watu kuwa tumefanikiwa kujisimamia?"

Hata kidogo. Hakuna palipokuwa salama. Yapo maeneo watu walihangaika kupita kiasi kabla ya kuona majina yao katika orodha ya wapiga kura. Wengine waliondoka vituoni baada ya kupoteza muda mwingi pasina kupiga kura zao.

Kuna maeneo palikuwa na upungufu au ukosefu wa kifaa hiki au kile na hivyo kuzorotesha upigaji kura.

Baadhi ya watu walilazimika kusubiri kwa muda mrefu katika msongamano kutokana na kituo cha uchaguzi kuwekwa mahali pasipo nafasi ya kutosha kukidhi idadi ya watu waliopaswa kupiga kura.

Lakini pia kuna maeneo ambayo walitokea wahuni na kupora masanduku ya kura kabla na baada ya kura kupigwa. Ripoti zimeonyesha yapo masanduku yalichomwa moto.

Isitoshe, katika baadhi ya maeneo ya nchi, matokeo ya uchaguzi yalisubiriwa kwa muda mrefu isivyo kawaida, tena bila ya kutolewa sababu ya msingi.

Cha kusikitisha ni pale inapoonekana matatizo yalikuwepo maeneo ambayo chama tawala kilikuwa kinakabiliwa na ushindani mkali kutoka vyama vya upinzani.

Kwa maneno mengine, kwa yale maeneo ambayo CCM ilikuwa ina uhakika wa ushindi, mambo yalikwenda bila matatizo yoyote.

Si kawaida kukuta popote pale wafuasi au viongozi wa CCM wamekamatwa kwa tuhuma zozote zile. Bali makundi ya Watanzania walioamua kufuata upinzani, hawajalala makwao.

Ajabu hata waliojitoma kwenye vituo na kupora masanduku hawajakamatwa. Sasa ule ukakamavu uliotangazwa na Jeshi la Polisi umeishia wapi kama masanduku yanaporwa wao wakiwa mita chache na kituo?

Tunajua hakuna mpumbavu wa kupora sanduku la kura kwenye vituo ambavyo CCM haina upinzani. Haijawahi kutokea tangu mwaka 1995.

Ndio maana tunajenga imani kuwa haya si matukio ya bahati mbaya. Ni matukio ya kupangwa vema na mapema ili kusaidia CCM.

Hapo hatujastawisha demokrasia bali tunaidhoofisha na tunajionesha kuwa hatujapea kiutu wala kustaarabika isipokuwa tunazidi kujidanganya kwamba tunakwenda sambamba na walimwengu wengine.

Hakika kwa hali hii, wala hatuna haki ya kumsikia waziri anajigamba eti “tumefanikiwa kwa asilimia karibu 100 kuendesha uchaguzi mzuri.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: