Hatujui au tunafanya kusudi?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KATIKA vita, inafahamika kwamba yule ambaye analijua vizuri zaidi eneo ambalo inapiganwa, ndiye mwenye nafasi nzuri zaidi ya kushinda.

Na wakati majenerali wa Saddam Hussein walipokuwa wakijipanga jangwani wakati wa Vita ya Ghuba ya mwaka 1990-1991, walikuwa na uhakika wa kuyapiga majeshi ya Marekani.

Majeshi ya Irak yalikuwa yakiyafahamu zaidi mazingira ya eneo la ghuba ya uajemi kuliko Wamarekani na washirika wao katika vita hiyo.

Ndiyo maana Saddam aliitangazia dunia kwamba Marekani itakiona cha mtema kuni wakati vita ya ardhini, hususani kwenye jangwa la Arabia, itakapoanza.

Cha ajabu, ni katika vita hiyo ya jangwani, ikipachikwa jina la Operation Desert Storm, ndipo haswa majeshi ya Saddam maarufu kwa jina la Republican Guard, walipokiona cha mtema kuni.

Ndani ya saa 100 za kwanza tangu kuanza kwa vita hiyo ya jangwani, wanajeshi 100,000 wa Irak tayari walikwisha uwawa ukilinganisha na askari 148 wa Marekani.

Ndani ya saa 100 tu za kwanza, vifaru 5856 vya Irak vilikuwa vimeharibiwa.

Nini kilitokea? Je, ilikuwaje majeshi ya Marekani yakashinda katika vita hiyo ambayo iliyopiganwa katika eneo ambalo majeshi ya Irak yalipigana na majeshi ya Iran kwa miaka minane kabla?

Ndipo hapo sasa linapokuja suala la kitu kiitwacho Global Positioning System (GPS) – mfumo wa satelaiti 24 uliowekwa umbali wa maili 11,000 kutoka uso wa dunia.

Mfumo huu unatumika sana kwenye kufahamu muda na mahali alipo mtu au kitu.

Ulibuniwa mwaka 1973 na wizara ya ulinzi ya Marekani na ulitumika kwa mara ya kwanza katika vita vya Ghuba.

GPS inamwezesha mtu kufahamu kitu kilipo. Ukichanganya na “kifaa dada” kiitwacho Geographic Information System (GIS), mtu anaweza kujua kila kitu kuhusu kitafutwacho.

Kwa hiyo, kama mtu anatafuta kifaa X, GPS itamwambia mahali halisi kilipo. GIS itasema iwapo hicho kitu ni mkorosho au bwawa la maji. Na iwapo eneo hilo lina chumvi nyingi au asidi.

Kwa hiyo, wakati majeshi ya Saddam yalikuwa yamejipanga mahali yakiwasubiri Wamarekani, askari hao walikuwa wanajua wapi askari, vifaru na magari mengine ya kijeshi yalipo. Hivyo, wakashambulia kutoka mbali. Vita ikaishia hapo.

Nimetoa mfano huu kuelezea namna sayansi na teknolojia inavyochukua nafasi katika vita na uendeshaji wa majeshi katika nchi zilizoendelea katika miaka ya karibuni.

Jeshi la Marekani halijabuni GPS pekee. Limewahi kubuni vitu vingi ikiwamo simu za mkononi. Hata hizi simu za aina ya Blackberry zilizopata umaarufu mkubwa duniani kote, zimebuniwa na jeshi hilohilo.

Hapa nchini kwetu, hali ni tofauti. Wiki mbili zilizopita, vituo vya televisheni vilipambwa na kipindi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuelezea mafanikio yake katika miaka mitano ya kwanza ya utawala wa rais Jakaya Kikwete.

Tulionyeshwa mwanajeshi akivunja matofali kwa kichwa. Mwingine akipigwa na mbao hadi zinavunjika mwilini. Tukaonyeshwa pia namna wanajeshi wanavyolima na kutibia watu.

Nafikiri yote hayo ni mambo murua kabisa. Lakini katika dunia ya sasa, nilitarajia kuona kitu gani kipya kimebuniwa na jeshi letu tangu enzi zile za magari ya nyumbu. Binafsi, sikuona chochote.

Haya mambo ya kupasua matofali kwa kichwa ni vita vya kizamani sana. Haya ni mapigano ya enzi za akina Lao Zu na Achilles enzi hizo. Wakati vita inapiganwa kwa mashine. Sisi tunatumia vichwa kuvunja matofali! Tunashindwa kutumia ubongo.

Halafu kuna ile picha ya mwanajeshi ameweka mkono chini halafu gari linapita juu yake. Hizi ni picha za mambo ya kizamani. Enzi ambazo nguvu ya mwili ya mwanajeshi ilikuwa muhimu.

Leo hii, bado mwanajeshi anatakiwa kuwa fiti kimwili lakini anatakiwa kuwa fiti zaidi kiakili. Yale madege makubwa, GPS na GIS haziendeshwi na watu wanaovunja matofali kwa kichwa. Hawa wanatumia vichwa vyao kisasa.

Lakini nilisikitishwa zaidi nilipoona wanajeshi wakiimba wimbo wa kumtukuza rais Kikwete kwenye kipindi hicho. JWTZ haikuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Sote tunajua kwamba Kikwete, pamoja na Kikwete kuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu, lakini hiki ni kipindi cha kampeni. Sifa zozote kwa mgombea mmoja, hasa zikitolewa na chombo cha umma, zinaleta picha mbaya.

Hata kama kipindi chenyewe kilitokana na maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, ilikuwa wazi kwamba lengo lilikuwa kumsifu Kikwete.

Vinginevyo, hakukuwapo na sababu ya kumpa rais dakika zaidi ya 15 za kuzungumza na wanajeshi na kikundi cha kwaya kuimba nyimbo za kumsifu.

Mimi naheshimu sana JWTZ. Kimsingi naheshimu mno fani ya jeshi na wanaonijua wanafahamu fika kwamba kama nisingekuwa mwandishi wa habari, basi leo hii ningekuwa mwanajeshi.

Kwa maoni yangu, kipindi kile hakikuwa na maana nyingine yoyote zaidi ya kutuonyesha kuwa JWTZ inamuunga mkono Kikwete katika kipindi kingine cha urais..

Nataka niamini kwamba JWTZ ni jeshi letu sisi wananchi. Si jeshi la CCM, CHADEMA wala CUF. Na ningependa, kama lingetaka kufanya vipindi vizuri vya televisheni liachane na kutuonyesha mambo ya mitulinga.

Lituonyeshe namna linavyopiga hatua kutoka zama zile za kale kwenda zama za kisasa. Mambo ya kuvunja matofali kwa kichwa na kuimba “tuna imani na Kikwete” hayawezi kulisaidia jeshi, wala kusadia ujenzi wa demokrasia nchini.

0
No votes yet