Hatuna mapatano na "wafalme"


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Tafakuri

YETU ni Jamhuri. Yaani nchi ambayo inaongozwa kwa misingi ya Katiba inayotokana na wananchi wenyewe na ambayo msingi wake siyo utawala wa kifalme (urithi) au wa kidini (Mungu).

Nchi ambayo ni jamhuri viongozi wake wanachaguliwa na wananchi na wanatokana na wananchi hao tena kwa njia ya kura au njia nyingine ambayo imekubalika katika nchi hiyo.

Katika nchi ambayo ni jamhuri kiongozi wa juu kabisa wa nchi anatokana na mfumo wa kura za raia wa nchi hiyo.

Hivyo, sifa kubwa ya jamhuri, hasa ile ya kidemokrasia, ni kuwa ni utawala wa watu, unaotokana na watu, na kwa ajili ya watu wenyewe.

Kwa maneno mengine, katika nchi ambayo ni jamhuri hakuna kiongozi ambaye anatambulika kama kiongozi kwa sababu ya urithi, nasaba, au amri ya Mungu!

Katika jamhuri hakuna viongozi ambao ni “chaguo la Mungu.” Viongozi wote ni chaguo la wananchi wanaowaongoza. Katika jamhuri basi, viongozi wanatoka kwa watu wenyewe na ni watu hao ndio wanawaweka viongozi wao madarakani.

Kwa maneno mengine, katika jamhuri viongozi hawatoki mbinguni au jehanamu. Wanatoka katikati yetu, ni raia wenzetu.Kwa msingi huo basi, viongozi hao ni taswira halisi ya sisi wenyewe tuliowaweka madarakani.

Naamini ukiwaangalia viongozi basi unaweza kujua wale wanaoongozwa walivyo, na kinyume chake pia ni kweli; yaani ukiwaangalia wale wanaoongozwa vivyo hivyo ndivyo walivyo viongozi wao.

Ninachosema ni kuwa mwaka huu 2009, ambao tayari tumeuanza na matukio mbalimbali, tujitazame upya na kama taifa. Ni wajibu wetu tuamue kuvunja mahusiano ya kitaswira na watawala wetu.

Sisi wananchi tubadilike na tuwe vingine ili mtu akiwaona watawala wetu asituone sisi ndani yao. Hivyo, tuwatangazie mapema watawala wetu kuwa hatuna mapatano na wale wote wanaotutawala kama wafalme.

Nimepata nafasi ya kuzungumza na viongozi mbalimbali (mawaziri, wabunge, na wengine). Jambo moja ambalo nimeligundua katika miaka hii mitatu ya harakati za mapambano ya kifikra ni kuwa kuna viongozi ambao wanaamini kabisa kuwa wao ni kama wafalme fulani hivi.

Kuna viongozi ambao nilipozungumza nao walikuwa na hasira za aina fulani kuwa kwanini wanahojiwa; wako tayari kuzusha zogo na kutaka kupigana.

Mara kadhaa baadhi yao wamekuwa kwenye kujihami zaidi kiasi kwamba huwa najiuliza, hivi walipokubali kuwa viongozi walifikiri wamekubali kuwa watoto wa mfalme? Leo hii hata watoto wa wafalme wanawajibishwa na wananchi wenzao.

Siku chache tu zilizopita tulisikia kisa cha Prince Harry (mtoto wa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Uingereza, Prince Charles), alivyolazimika kuomba radhi baada ya kusikika kwenye video aliyorekodi akiita jina la kumdhalilisha mmoja wa maafisa wenzake jeshini.

Imebidi Prince Harry atoe tamko la kuomba radhi kwa kauli aliyoitoa. Sasa kama mwana wa mfalme anaweza kulazimishwa kuomba radhi na kufuta kauli yake, kwa nini hawa tuliowapigia kura wafikiri kwamba wana uwezo wa mwisho juu ya maslahi yetu kama raia?

Ni kwa sababu hiyo tunatangaza tena, na sauti yetu isikie kama radi katika usiku wa gharika, kuwa kama miaka miwili iliyopita walifikiri tunawakaanga kwenye moto walikuwa sahihi.

Hata hivyo, moto ule uliopita ulikuwa ni wa kuni, na ulioisha mwaka jana ulikuwa ni moto wa mafuta; mwaka huu ni moto wa gesi tukiandaa moto wa nyuklia kuelekea 2010.

Kama mwaka jana tuliwapigisha magoti watawala wetu, mwaka huu tutahakikisha wale wote wanaojifikiria ni wafalme watambae kwa magoti mbele ya wananchi wa taifa hili.

Tunachotaka hasa siyo kuwadhalilisha, siyo kuwaumbua, siyo kuwafanya waonekane duni, bali kuhakikisha wale wote walioapa kuilinda Katiba ya nchi wanafanya hivyo.

Waliopa kusimamia miradi wanafanya hivyo kwa ubora wote; wale wote walioapa kulinda amani na utulivu wanafanya na wale wote ambao walisimama kuomba kura za wananchi wa taifa hili, wanaacha kula na kulala na badala yake wanafanya kazi kuonesha kwanini wanastahili kura nyingine.

Katika hili tumedhamiria kuziteka fikra za wananchi wetu; kuwaonesha kuwa hawapaswi kamwe kuuza haki yao ya kura kwa vifulana, vi-tsheti na pilau la hapa na pale.

Tunataka wananchi wa Tanzania wawe tofauti na wale wa Kenya. Wakati Kenya walisema “kula kuleni, kura tupeni,” sisi tunataka wananchi wetu wajione ni wenye utu kweli na hadhi.

Tunataka wathubutu kusema, “Kula hatuli, kura hatuwapi mpaka kula tule wote.” Kwamba suala siyo kula tu mimi na familia yangu, au yeye bosi na wapambe wake, bali kuhakikisha hadi mtoto wa Masasi, na mama wa Maneromango naye anakula.

Hatuko tayari tena kuuza haki ya mzaliwa wa kwanza na kujiuza utu wetu kama makahaba wa kisiasa wanaopitiwa na kila mwanasiasa!

Tunataka Watanzania waamue, kwamba ni wao ndio wenye uamuzi wa mwisho wa nani anawaongoza na jinsi gani anawaongoza.

Geukia MwanaHALISI – wachapishaji wahariri na waandishi wake. Siku tisini zilizopita zilikuwa ni muda wa kwenda jangwani, muda wa kutulia na kutafakari: Je, katika taifa letu, sisi kama chombo cha habari tuna wito gani? Ilikuwa ni saa ya taamuli.

Tumekaa, tumeona, tumeamua kwamba hatutasalimisha nafsi zetu. Tutakuwa wa kweli kwa taifa letu na kwa wananchi wenzetu. Katika hili hatuna makubaliano wala mapatano na wale watutawalao kama wafalme.

Tutaendelea kuhoji; tutaendelea kukosoa, na tutaendelea kujenga hoja kuwa Tanzania inastahili viongozi bora zaidi kuliko “bora viongozi.”

Siyo tu tutajenga hoja, bali zaidi tutaweka mwanga wa viongozi hao ni wapi na wana sifa zipi; tutawamulika viongozi bora na kuwapa jukwaa; tutahakikisha kila anayesimama kuongoza anawajibishwa na wananchi anaowaongoza.

Yawezekana tukawaudhi baadhi ya watu, tukawakwaza na wengine wakaona “tunawaonea”. Kwa wote hawa tuna ujumbe mmoja tu: Watumikieni wananchi kwa haki, ukweli, uwazi, na usawa na kwa mujibu wa sheria.

Kinyume cha hapo tutazifunua rangi zenu kama mwali anavyofunuliwa na tutaweka mipango yenu hadharani na siri zenu upenuni, hadi pale mtakapotambua na kukubali kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano, na uongozi wake wastahili kuwa wa demokrasia.

0
No votes yet