Hatuna sababu ya kumpongeza Rostam


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Rostam Aziz

SIKUBALIANI na wanaopongeza uamuzi wa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kwa kujiuzulu. Nawakatalia zaidi wale wanaodai amefanya hivyo kwa maslahi ya taifa.

Wananishangaza zaidi wanaodai kuwa alichokifanya Rostam ni kitendo cha kuigwa.

Lakini wanaonishangaza zaidi ni wote ambao wanatukuza uamuzi wa Rostam kana kwamba aliitikia wito wa baadhi yetu kumtaka ajiuzulu.

Hawajasoma hotuba yake. Ni wavivu wa kusoma, wagumu kuelewa, na wepesi kusahau.

Hotuba yake ya nane, yenye maneno 3067, pamoja na mambo mengine, ilitaja maneno “Wazee wangu” mara 34; “chama chetu” mara 13; “CCM” mara 16; “Halmashauri Kuu ya Taifa” mara 4; “Kamati Kuu” mara 6; “biashara” mara 6; “taifa” mara 8; “Tanzania” mara 6.

Neno “Watanzania wenzangu” linaonekana mara 1; “wananchi” linatokea mara 4 na kati ya hizo hakuna kitu kama “wananchi wenzangu.” Neno “Wazee wetu” linatokea mara 1.

Sasa ni kitu gani kimewafanya wanaoshabikia hotuba hii waamini kuwa Rostam alijiuzulu kwa maslahi ya taifa?

Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kujiuzulu ubunge wa kuteuliwa akikataa kuburuzwa na serikali ya mkoloni wakati tunaelekea Uhuru.

Inanishangaza kuwa leo hii watu wanaojiona ni wanasiasa wameshindwa kufuata mfano wa kujiuzulu katika hali ya kupinga serikali inavyofanya mambo.

Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu na kumuachia Kawawa baada ya Uhuru kupinga sera na jinsi wakoloni walivyokuwa wakijaribu kumburuza pamoja na jitihada zake zote za kujaribu kufikia muafaka wa aina fulani.

Mwezi Julai 1957 Nyerere aliteuliwa kuwa Mbunge katika Baraza la Kutunga Sheria. Miezi michache kabla ya hapo alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara.

Tarehe 14 Desemba, 1957 aliandika barua ya kujiuzulu. Siku mbili baadaye, katika makala iliyotoka kwenye kijarida “Sauti ya TANU” alisema awali aliamini kuwa serikali ilikuwa na malengo ya kweli ya kushughulikia matatizo ya kisasa ya wakati huo.

Aligundua kuwa serikali haikuwa tayari kubadili mwelekeo katika dhamira safi. Alijua kuwa asingeweza kuendelea kuwa ndani ya Bunge lisilokuwa tayari kusikiliza hoja zake, hasa kwenye mambo ya msingi.

Aliandika hivi (tafsiri ni yangu): “Kama ningeamini kuwa jukumu langu ndani ya baraza lilikuwa kutoa na si kuchukua, bado ningejiuzulu.

“Nimeweza kutoa kila kilichokuwa kwenye uwezo wangu kukitoa, na vyote nilivyovitoa vimekataliwa. Niliingia Bungeni nikiwa na dhamira ya kutoa na kupokea. Haipo tena. Ningekuwa nawaibia wananchi, na kukiibia chama changu kama ningeendelea kubakia humo, nikipokea posho na kuhudhuria tafrija kama mbunge, watu wakiamini kuwa nilikuwa na manufaa fulani, wakati nilikuwa najua siku na manufaa yoyote. Hivyo, sikuwa na jingine isipokuwa kujiuzulu”.

Nyerere aliongozwa na kanuni; kwamba maslahi ya wananchi yako juu ya maslahi mengine. Rostam amejiuzulu kwa sababu kubwa mbili – chama chake na biashara zake.

Rostam anasema: “Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.

“Dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.”

Kwa ufupi, Rostam hakujiuizulu kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.

Kama kweli Rostam aliona kuwa anahitaji kujishughulisha na biashara zake kwanini aliamua kurudisha fomu za kugombea ubunge? Kwanini alikubali kusimama na Kikwete jukwaani na kuomba kura za wananchi ambao walimrudisha tena Bungeni kwa mara ya nne?

Vile vile, Rostam hakumwomba radhi mtu yeyote. Alizungumza kama mhanga wa siasa mbaya na chafu.

Sote tunajua jinsi alivyotumia vyombo mbalimbali vya habari kushughulikia wapinzani wa “Kikwete wake. ” Tunakumbuka kauli yake dhidi ya wale aliowaita “mafisadi nyangumi”.

Na wakati huo yeye hakuona kama hizo zilikuwa siasa uchwara. Hajatuomba radhi kwa siasa hizo alizoshiriki kuziasisi na kuziendesha.

Binafsi ninaamini, kuna hatua zaidi za kuchukuliwa:

  1. Avifunge vyombo vyake vyote alivyotumia kuwachafua watu, Rupert Murdoch mmiliki wa vyombo kadhaa vya habari vya Uingereza na Marekakani.
  2. Ajipeleke mwenyewe kwenye vyombo vya usalama na kutoa ushahidi jinsi alivyohusika na kashfa ya Kagoda na EPA kwa ujumla.
  3. CCM kimvue uanachama chini ya kanuni za maadili na katiba ya chama.

Kitu pekee ambacho naweza kumpongeza na kumshukuru Rostam kwa uamuzi wake wa kujiuzulu ni kuwa angalau sasa tumebakiwa na mtu mmoja Bungeni ambaye ana nguvu kuliko mwanasiasa mwingine yeyote nchini na ambaye natumaini naye atafuata mkumbo wa kuachia ngazi na huyo atafanya kweli kwa maslahi ya Taifa. Si Lowassa.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: