Hawa Dowans kama Bruce Lee


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KAMPUNI ya kufua umeme ya Dowans imeiweka serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye fuko. Haifurukuti.

Baada ya kushinda kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kustahili kulipwa tuzo ya Sh. 94 bilioni, msimamo wa serikali na CCM ulikuwa “Dowans lazima walipwe”.

Msimamo wa CCM ulitolewa na John Chiligati, kada aliyekuwa katibu wa Itikadi na Uenezi na ambaye sasa ni naibu katibu mkuu wa chama hicho. Kwa upande wa serikali msimamo ulitolewa na mwanasheria mkuu wa serikali, Frederick Werema.

Ilipofika Februari, tena wakati wa sherehe za kuzaliwa kwa CCM, Rais Jakaya Kikwete alijinasua akisema hawajui wamiliki wa Dowans na “ameagiza wanasheria wapambane tuzo hiyo isilipwe.”

Katika kikao cha Halmashauri Kuu (CCM-NEC) ikitumia falsafa ya kujivua gamba iliwasuta wanasiasa watatu waliopachikwa majina ya Mapacha Watatu – Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz.

CCM wakaanza kampeni ‘kiinimacho’. Rostam akaachia nyadhifa zake za kisiasa ukiwemo ubunge kwa kashfa hiyo ya Richmond/Dowans.

Serikali ikafanya ujanja: Mitambo ya Dowans wakauziwa Symbion Power ya Marekani. Ulipokaribia uchaguzi mdogo wa Igunga kujaza nafasi aliyoiacha Rostam, CCM ikampigia magoti asaidie kutetea.

Akaitwa, akapambwa kwa maneno matamu na alipoona “amesamehewa dhambi” katika namna iliyompendeza, akagharimia ndege ya kampeni.

Oktoba 2, wakazi wa Igunga wakaidhinisha kupitia boksi la kura Dk. Dalaly Peter Kafumu wa CCM ndiye mbunge wao.

Katikati ya sherehe za Igunga, Mahakama ya Kuu ikaipa tuzo Dowans kwa kutupa rufaa zote za wanaharakati wanaopinga tuzo hilo .

Mtu anayedaiwa kuwa ‘mmiliki’ wa Dowans ni Rostam Aziz. Nyaraka zilionesha ndiye alipewa “Power of Attorney” kusimamia mradi huo japokuwa Machi mwaka huu ilichezwa filamu ya ‘kininja’ akaja nchini Brigedia Jenerali mstaafu Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi akidai ndiye mmiliki halali.

Hee! Symbion Power ilifanikiwa kununua mitambo ya Dowans licha ya mahakama kuzuia upande wowote unaohusika nayo kufanya lolote bila idhini yake.

Halafu mahakama iliyozuia mazungumzo yoyote kuhusu Dowans hadi iruhusu, ilisubiri hadi ukakamilika uchaguzi mdogo wa Igunga na CCM ikaibuka kidedea ndipo ikatupa kesi ya wanaharakati ya kuzuia kampuni hiyo yenye nguvu za ajabu kulipwa tuzo lake.

Ushindi wa kisanii namna hii ni sawa na wa msanii wa filamu za zamani, Bruce Lee ambaye alikuwa na uwezo kisanii kupiga hata kuua kundi la maadui zake, mwenyewe akabaki salama, wakati mwingine bila kujeruhiwa.

Bruce Lee wa Dowans ameigaragaza TANESCO kortini na amewabwaga kisanii wanaharakati na wananchi. Mlolongo huu wote unaonesha mbali na kusikika majina ya kina Rostam na Al Adawi, kuna Bruce Lee mwingine Dowans.

Kwa nini Mahakama imefumbia macho “dharau ya mahakama” iliyofanywa na serikali? Kwa nini serikali imehusika katika mpango huu na kuipa Symbion Power mkataba?

CCM ndiyo iliagiza serikali itafute mbinu za kuondoa giza mwaka 2006. Haraka serikali ikaja na Richmond ambayo iligeuza Dowans iliyobatizwa kuwa Symbion.

Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo haikumtaja mmiliki wa Richmond wala Dowans. Rais akasema hawajui Dowans. Serikali haimjui Dowans hivyo Watanzania hawaijui Dowans. Sasa sarakasi zote hizi, tunamlipa nani? Usanii mtupu!

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)