Haya ya Liyumba kituko!


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 February 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KUANZIA kufichuka kwa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ilioko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mradi wa umeme wa Richmond hadi ule wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT, palianza mashaka.

Namna serikali ilivyokuwa nzito katika kushughulikia ufisadi huo, yenyewe ikazidisha mashaka.

Angalau idadi fulani wanakabiliwa na mashitaka ya kuchota kifisadi mabilioni ya shilingi za EPA. Hapajaonekana uthabiti katika kudhibiti wahusika muhimu wa ufisadi katika Richmond.

Ujenzi wa majengo ya BoT umechunguzwa. Mabaya yamebainika. Angalau maofisa wawili wa Benki hii wapo mahakamani kwa sasa.

Lakini bado zimwi la mashaka katika kesi yao linazidi huku kukiwa na uchungu kwamba watuhumiwa wakuu hawajadhibitiwa.

Tusisemeje mashaka wakati Amatus Liyumba, mtuhumiwa aliyeshurutishwa kutoa hati za mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh. 55 bilioni, anatolewa rumande kwa kuwasilisha mali za thamani ya chini ya Sh. bilioni moja?

Ameachiwa kwa dhamana mchana kweupe? Sasa inakuaje umma uambiwe eti ametoroka haonekani? Hakimu anaamua kutoa waranti wakamatwe wadhamini wake.

Wadhamini wanafika mahakamani. Hakimu anasema hapana tatizo anasubiri kesi. Ndio maana hata wakili wa mtuhumiwa, Hudson Ndyusepo anashangaa kulikoni?

Si vizuri kuhoji uwezo wa hakimu anayesikiliza kesi hii na ni desturi yetu ya kitaaluma kutothubutu kuingilia uhuru wa mahakama tukiamini kila mhusika anajitahidi kufanya kazi yake vizuri.

Bado kama chombo kinachowakilisha mawazo ya umma, tuna wajibu kutafuta kujiridhisha juu ya kila tunachokiona kinazidisha kiwingu katika kushughulikia tatizo linalokua nchini petu la ufisadi.

Tunataka kujiridhisha kwani yanayoshuhudiwa na wananchi wanaofika mahakamani kila siku kufuatilia kesi hizi, pamoja na wenzao walioko mbali na nafasi ya kuwepo mahakamani, yanakirihisha.

Tunakosea nini tukisema mwenendo wa kesi na hasa namna mahakama ilivyoshughulikia suala la dhamana ya watuhumiwa, unazua hoja nyingi?

Inawezekana hata mzee Liyumba aliyefika mahakamani jana Jumanne, hajawaza hata chembe kutoroka kesi.

Pengine anataka atulie mpaka mahakama itakapompa haki ya kujieleza. Huenda anataka kuthibitisha kuna haki kweli katika mchakato wa kimahakama Tanzania?

Tunasihi kila mtu, hasahasa maofisa wa Mahakama; waendesha mashitaka, mawakili na hakimu msikiliza kesi, wafanye tu kazi yao kwa uadilifu mkubwa ili kuondoa mashaka haya!

0
No votes yet