Hebu Serikali ijitambue


editor's picture

Na editor - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI haiwezi kupinga ilishindwa kusimamia vizuri Operesheni Hamisha Mifugo kwenye maeneo tengefu mwaka 2006 na hivyo kuchochea ufukara kwa mamia ya wafugaji.

Ushahidi ni vilio watoavyo wafugaji wa Kilosa, mkoani Morogoro. Kila anayebahatika kufikia mwandishi wa habari, analalamikia kuporwa mifugo wakati wa operesheni hiyo.

Kilio kama hicho kimetolewa na wafugaji wengi nchini. Kilisikika Mbarali, mkoani Mbeya; kilisikika Ludewa na Makete, wilaya za mkoani Iringa.

Kama tutambuavyo matokeo mazuri ya operesheni, ndivyo tunavyoguswa na matokeo haya mabaya.

Mifugo ni chanzo cha uhakika wa mapato ya wafugaji. Hatua ya kuwapora ni kuangamiza mapato yao.

Operesheni iliendeshwa kinyume na misingi ya haki za binadamu na utawala bora na kibaya zaidi, viongozi waandamizi serikalini wametuhumiwa kujinufaisha kutokana nayo.

Tunakumbuka serikali ilichunguza matokeo na athari za operesheni hii, iliyokuwa utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.

Lakini miaka mitatu baadaye, hakuna taarifa inayohusiana na kilichogundulika. Tunathubutu kuamini tume iliona hali halisi na inajua – maana imetajiwa na wananchi – viongozi waliovuna kibinafsi kutokana na operesheni hiyo. Hakuna aliyewajibishwa.

Hawa wamepora mali za wafugaji na kuwasababishia ufukara hadi kwa familia zao. Hapa ndipo tunaposema serikali haijawajibika ipasavyo katika uovu uliotendwa.

Hili linakera na halipendezi. Ni aibu kusikia malalamiko kama haya yakiendelea, bila ya kuwepo hatua za dhati kwa wahusika.

Haiwezekani serikali kukaa kimya wakati wananchi wanahangaika namna ya kuishi baada ya waovu kuhujumu njia yao kuu ya mapato.

Unaposikia mfugaji anaapa atampiga Mkuu wa Wilaya akimkuta, kwa kuwa amemfilisi; jua kwamba ameguswa mno.

Na huko ni kuchukua sheria mikononi ambako ni kutenda kosa la jinai. Lakini afanyeje wakati serikali anayoichangia kodi, haijamsaidia? Kwa kushindwa kumlinda pamoja na mali yake, anaamini haimjali.

Mfugaji huyu anawakilisha hisia za wafugaji wengi walioathirika na operesheni ya serikali; sema tu wao hawajabahatika kuinua sauti zao zikasikika.

Tunaogopa matokeo ya wote hawa kuonyesha hasira zao. Itoshe basi kuiamsha serikali ichukue hatua haraka kuwezesha wafugaji kulipwa haki zao, ikiwemo kuwabana viongozi waliowadhulumu.

0
No votes yet