Heri kwa watakaochagua mabadiliko


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

JUMAPILI hii, wananchi wataamua nani avuke mabonde na vichaka vyenye miiba ili aingie jumba kubwa, jeupe, la zamani, lililoko kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam – Ikulu.

Mkazi wa ikulu ndiye mtawala mkuu wa nchi – rais. Kwa miaka 50 mtawala ametoka chama kilekile, cha viongozi walewale na fikra zilezile; kama bado zipo.

Katika uchaguzi huu, wananchi wanatarajiwa kuonyesha kuwa, ama wanataka mabadiliko au wanataka kubaki katika ndweo za wachovu waliotawala nchi hii kwa nusu karne sasa.

Bali Jumamosi iliyopita, Dk. Willibrod Slaa, mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliliambia taifa, kwa njia ya kujibu maswali ya wananchi kupitia kituo cha televisheni cha ITV, kuwa Tanzania bila CCM inawezekana.

Uchaguzi mkuu huu ni wa kutafuta mabadiliko. Hata CCM inajua kuwa iwapo itashinda, kama haitaleta mabadiliko, itashindwa kutawala.

Lakini wananchi wamepata fursa ya kipekee mwaka huu, kujua yote ya pande mbili: upande wa waliokuwa madarakani kwa nusu karne na wale wanaotaka kuingia ikulu. Kwa hiyo ni rahisi kuchagua.

Je, wapigakura washikilie ahadi ya yule ambaye hajawahi kuwadanganya au wakumbatie yule wa kale ambaye ahadi zake nyingi zimekuwa hewa na hasa ahadi ya “maisha bora kwa kila Mtanzania” ambayo imegeuka kuwa “maisha bora kwa kila fisadi?”

Vijiji vingi ni jahanamu. Wanaolima hawavuni. Ukame. Mafuriko. Ngedere! Wanaovuna hawauzi sokoni. Lazima uuze katika ushirika uliokumbwa na ufisadi uliolelewa na serikali.

Makazi ya wananchi wengi shamba yameendelea kuwa vibanda vilivyoezekwa kwa nyasi na kukandikwa kwa udongo – mithili ya vibanda vya muda vya wavuvi wanaosubiri mkondo wa upepo.

Vifo vya watoto na akina mama na wazee, kutokana na magonjwa yanayozuilika na kutibika, vinaendelea vijijini ambako watawala hukusanya kodi lakini hawafikishi dawa wala elimu ya kujikinga.

Wapigakura wachague yupi: Aliyetawala kwa miaka 50 na hadi leo anashindwa kuua mbu anayeendelea kueneza malaria inayoua kuliko ukimwi?

Kipindupindu kiliingia mkoani Morogoro mwaka 1978; kikakaa na kujenga maghorofa. Hadi leo kinaendelea kuua; mbele ya serikali ya chama mashuhuri kwa kupiga soga za “maendeleo.”

Chama ambacho serikali yake imeshindwa kuua mbu au kutokomeza malaria; imeshindwa kutumia maji ya mito, maziwa na bahari kuondoa janga la njaa, kitachaguliwaje?

Nani atachagua chama ambacho serikali yake inatukana na kutishia wafanyakazi; kuwanyima mishahara inayolingana na kazi zao; kukataa kulipa walimu mafao yao na kukataa kulipa wastaafu hadi wengine wamekufa kabla ya kupata haki yao?

Mzazi gani atakwenda kituoni Jumapili kuchagua chama ambacho serikali yake inashiriki kuzalisha ujinga – kwa watoto kumaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika?

Wananchi wamemsikia Dk. Slaa akiwapa mfano wa rais anayepishana na wazungu angani wakiwa wamebeba dhahabu, almasi, tanzanite na madini mengine kutoka Tanzania; wakati rais anarejea nyumbani na furushi la ahadi za kupewa nyavu za kudakia mbu.

Dhahabu ni madini yenye elementi ya kemikali na ambayo, licha kunakshia vitu mbalimbali, hutumiwa kulinda thamani ya fedha duniani. Uranium inatoa nishati ya umeme na hutumika kutenegeneza, pamoja na mambo mengine, silaha za nyuklia.

Serikali ya chama kilichotawala kwa miaka 50, inaingia mikataba mibovu ya madini ambayo inafanya taifa liambulie makombo ya makampuni ya uchimbaji – kwa kutupiwa kinachoitwa mrabaha: asilimia 3 ya mapato yao.

Hayo ni matunda ya chama ambacho kimechoka, kimedhoofika, kimechakaa na hakina uwezo tena wa kuleta mabadiliko. Nani atachagua CCM na kwa lipi?

Twende kwa mifano. Serikali imekataa kufungua vyuo, mahali pengine inadaiwa kukataa kufunga vyuo, ili wanafunzi, kwa maelfu, waweze kurejea walipojiandikishia na kufurahia haki yao ya kupiga kura.

Nani atachagua chama ambacho serikali yake inapora wanafunzi haki ya kupiga kura? Hicho ni chama cha siasa au kundi la wababe?

Mauaji ya vikongwe na albino katika mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria. Serikali ya chama tawala imekaa kimya hadi iliposutwa na kustuliwa na wananchi na jumuia ya kimataifa.

Wapigakura wanauliza: Chama ambacho serikali yake lazima ipashwe joto kama injini ya treni inayotumia kuni, kitachaguliwa na nani?

Wananchi wanaotaka mabadiliko watawezaje kuchagua chama ambacho serikali yake, baada ya kuzika walioangamia katika meli ya m.v Bukoba, “iliingia mitini” hadi wakati huu wa kutafuta kura; ambapo inakuja na ahadi ileile ya kununua meli mpya?

Chama ambacho serikali yake iliuza viwanda, makampuni na mashirika ya umma kwa “bei ya bure” kana kwamba imeshikiwa kiboko, kitachaguliwaje na wananchi wanaotaka mabadiliko? Asasi hizo zilijengwa kwa jasho na damu ya wananchi wote.

Usafiri wa reli umekufa. Kampuni ya ndege (ATCL) inapumua kwa shida. Shirika la umeme, TANESCO limeshindwa kuwa na miradi endelevu ya kuzalisha umeme. Nani atachagua chama ambacho serikali yake imesababisha yote hayo?

Serikali ya CCM imenyamazia wizi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na makampuni ya Kagoda, Meremeta, Deep Green na mengine mengi. Kimya hicho kinaondolea chama hadhi ya kuwa mpangaji tena ikulu.

Mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa, yangetumika kujenga zahanati kila kata nchini na kuweka dawa na fedha zinazosalia kumalizia malipo kwa madai ya walimu.

Nani atakubali kuchagua chama ambacho kimehifadhi, kulinda, kupakata na hata kusifia watuhumiwa wa ufisadi nchini?

Nani atachagua chama ambacho serikali yake inajua walioibia wananchi mabilioni ya shilingi; ikajua walikopitishia fedha hizo, lakini ikakaa kimya na kuwalinda?

Kama wananchi wanataka mabadiliko, watachaguaje mgombea ambaye wakati akiwa rais, alivunja katiba ya nchi kwa kufanya upendeleo – kusamehe waliokiri kuwa wezi wa mabilioni ya shilingi, huku serikali yake ikiendelea kushitaki “wezi” wa kuku?

Wanaotaka mabadiliko hawawezi kuchagua chama ambacho viongozi wake wanakataa kuona ukweli kwamba elimu na afya vinaweza kutolewa bila mwananchi kuweka tena mkono mfukoni.

Viongozi wa CCM ndio wanasema haiwezekani. Hakika wao hawawezi kwa kuwa, fedha na raslimali nyingi zinachotwa na wezi na mafisafi ambao serikali yake inalinda na kuhusudu.

Hawawezi kwa kuwa wana baraza kubwa la mawaziri ambalo ni aghali sana. Wananunua magari mengi ya kifahari na wanalipana posho zenye thamani ya kujenga shule 50 za sekondari kila mwaka.

Bali Jumapili yaja. Pasiwepo wa kunyang’anya wananchi haki yao – kwa vitisho au kwa wizi. Kwani mwizi wa kura atashindwa kutawala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: