Hesabu za waliopiga kura haziingii akilini


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MWALIMU wangu wa Hisabati alinifundisha ukweli mmoja. Kwamba hesabu ikifuata kanuni zake, haiwezi kutoa jawabu tofauti hata kama zimefanywa kijijini Msalato au Washington, Marekani.

Mtoto wa shule ya Msingi Mtakuja akijumlisha 49 na 51 atapata 100. Mtoto wa Shule ya Msingi Beijing huko China akijumlisha 51 na 49 naye atapata 100.

Unapokutana na hesabu ambazo zinatoa jawabu tofauti, basi aidha swali haliko wazi, ama kanuni zimekosewa.

Katika uchaguzi mkuu uliomalizika hesabu za waliojitokeza kupiga kura haziingii akilini. Zimegoma. Hazitaki. Haijulikani tatizo liko wapi na nani alaumiwe?

Hesabu za waliojiandikisha unapolinganisha na waliojitokeza kupiga kura, inaonekana kuna tatizo kubwa ambalo halijapatiwa ufumbuzi.

Kwa mfano, katika uchaguzi wa mwaka 2005 wananchi waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16,407,318. Waliopiga kura walikuwa 11,365,477 – sawa na asilimia 69.3 ya waliojiandikisha.

Waliojiandikisha katika uchaguzi wa mwaka huu, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni watu 20,137,303. Lakini waliopiga kura ni watu 8,398,394. Hii ni sawa na asilimia 42.64.

Asilimia hii ni muhimu katika maudhui yake, kwa sababu yawezekana watu wengi hawajaelewa uzito wa asilimia hii 42.64.

Kuanzia 26 Aprili 1964 zilipoungana Tanganyika na Zanzibar hadi leo hii, tumekuwa na chaguzi kuu 10 ambazo zimekuwa zikifanyika kila baada ya miaka mitano.

Tangu wakati huo hadi mwaka 1990 uchaguzi ulikuwa ni chini ya mfumo wa vyama vingi. Waliojitokeza kupiga kura na waliojiandikisha ilikuwa hivi:

Mwaka 1965 waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 77.1 ya walioandikishwa. Mwaka 1970 walikuwa asilimia 72.2, mwaka 1975 waliopiga kura walikuwa asilimia 81.7.

Mwaka 1980 waliojitokeza walikuwa asilimia 75 ya waliojiandikisha, 1985 asilimia 75 ya waliojiandikisha na 1990 asilimia 74.4.

Kuanzia 1995 hadi leo hii, chaguzi nne zimefanyika katika mfumo wa vyama vingi. Idadi ya waliopiga kura kulinganisha na wale waliojiandikisha ni kama ifuatavyo:

Mwaka 1995 waliojiandikisha walikuwa asilimia 76.7 ya wale waliojiandikisha, mwaka 2000 asilimia 84.4, mwaka 2005 asilimia 72.4 na 2010 asilimia 42.64.

Katika kipindi chote hicho, hatujawahi kuwa chini ya asilimia 70 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Iwapo mwaka huu, asilimia 70 waliojiandikisha wangejitokeza kupiga kura kama baadhi yetu tulivyotarajia, basi watu 14. 09 wangejitokeza kupiga kura.

Lakini waliojitokeza kati ya watu milioni 20 ni watu 8 milioni nane na ushei tu. Hivyo zaidi ya watu milioni 11 hawakupiga kura!

Kwanini watu wengi hawakujitokeza kupiga kura? Nimejaribu kuwa mkarimu kwa kusema:

Wanafunzi wa vyuo vikuu wote ambao hata mmoja hakupiga kura ni 1 milioni. Ukiwaondoa unabakia na watu 19 milioni.

Watu ambao kutokana na shughuli zao hawakuweza kubadili ratiba zao na kwenda vituoni kupiga kura ni 2 milioni. Ukiwatoa unabaki na watu 18 milioni.

Walioamua kutopiga kura kwa sababu ya siasa chafu za mwaka huu, tukadirie kuwa 4 milioni. Ukitoa wanabaki 14 milioni.

Ambao hawakupiga kura kutokana na sababu ambazo zilitokea vituoni, nao tuwakadirie kuwa 2 milioni. Tukifanya hivyo, watabaki 12 milioni.

Tuwatoea watu 8 milioni ambao hawakupiga kura kwa sababu mbalimbali. Hata kwa hesabu hiyo, bado tungebakiwa na watu 12 milioni ambao wangejitokeza kupiga kura. Hawa ni sawa na asilimia 60 ya waliojiandikisha.

Lakini bado tumebaki na asilimia 42 tu! Je, sababu ni nini? Tujiulize swali hili kwa namna nyingine.

Mwaka 2005 rais Jakaya Kikwete akionekana kukubalika, alishinda kwa kupata kura 9,123,952.

Mwaka 2010 Kikwete amepata kura 5,276,827. Tofauti ya kura hizo ni kura 3,847,125 – karibu watu milioni nne.

Hii ina maana watu 3.8 milioni ambao waliomchagua Kikwete mwaka 2005 hawakumchagua mwaka huu au hawakupiga kura kabisa. Je, sababu ni nini?

Tunaweza kuangalia kwa mwanga mwingine. Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakijitapa kuwa chama chao kina mtaji wa watu 5 milioni.

Tukubaliane nao. Lakini kama hivyo ndivyo, ina maana kwamba Kikwete amepigiwa kura na wanachama wake pekee?

Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa alipata kura 2.2 milioni. Hii ni zaidi ya kura 463,325 alizopata aliyekuwa mgombea urais wa chama cha NCCR- Mageuzi, Augustine Mrema mwaka 1995.

Uchaguzi wa mwaka 1995, Mrema alipata kura 1.8 milioni au ni zaidi ya kura 944,816 alizopata Profesa Ibrahim Lipumba mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, Lipumba alipata kura 1.3 milioni.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Profesa Lipumba amepata kura 695,667 akiwa ametupwa kwa kura zaidi ya 1,576,274 na Dk. Slaa.

Hapa kuna somo jingine. Hapa kuna kitu muhimu cha kuangaliza ili kuweza kuzielewa kura milioni tano alizopata Kikwete.

Kutokana na mahusiano ya karibu kati ya vyama vya CUF na CCM inaaminika kuwa kuna kundi kubwa limehama kutoka kwa Lipumba kwenda kwa Kikwete.

Yumkini kundi hili litakuwa limehama kutoka katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.

Ukichua hesabu za uchaguzi wa 2000 na 2005, haraka utaona kuwa CCM kimefanya vizuri kwenye mikoa hiyo ambayo Lipumba alifanya vizuri katika chaguzi za 2000 na 2005.

Tunaweza hata kujua ni kiasi gani cha kura za Lipumba zilizoenda kwa Kikwete.

Kwa mfano, mwaka 2000 Lipumba alipata kura 1,329,077 na mwaka 2005 alipata kura 1,327,125.

Tofauti kati ya miaka hiyo mitano ni watu 1,952. Kati ya miaka hiyo mitano Prof. Lipumba alikosa karibu kura 2000 tu za idadi ya watu waliomchagua mwaka 2000.

Hii ina maana kuwa Prof. Lipumba alikuwa na kundi kubwa la watu ambao wamekuwa watii kwake. Lakini mwaka huu, ameishia kupata kura 695,667!

Hili ni punguzo la watu 631,458 kutoka mwaka 2005.

Tukitoa kura hizo za mwaka 2005 zikaenda kwa Kikwete, tunapata kura 4,645,369 ambapo bado Kikwete angeshinda kwa kura chache ya asilimia 55.3. 

Sijui kulikuwa na tatizo gani kuacha ushindi huu uje. Sielewi kwanini mkurugenzi wa uchaguzi, Rajavu Kilavu ambaye aliahidi matokeo ya urais yangetangazwa siku moja baada ya kupiga kura?

Kauli ya Kilavu ilikuja baada ya Machi mwaka huu kuahidi matokeo ya urais kutangazwa pamoja na yale ya wabunge na madiwani katika majimbo ya uchaguzi.

Matokeo yake, matokeo ya urais yalitangazwa karibu siku tatu baada ya uchaguzi na katika maeneo mengine inasemekana hayajatangazwa mpaka sasa.

Hapa imenibidi nijiulize: Yawezekana kura zilizokwenda kwa aliyetangazwa mshindi zilikuwa ndogo kuliko asilimia 55.3 iliyotangazwa?

Ili kujua matokeo halisi ni muhimu kwa wasimamizi wote wa uchaguzi kuweka nakala ya fomu zilizosainiwa na vyama siku ya kutangazwa matokeo hadharani ili jumla yake iweze kujumlishwa na watu huru.

Kwa vile rais keshapatikana na hakuna cha kubadili hilo, hilo litasaidia kuondoa wingu la uchaguzi wa rais mwaka huu.

Lakini itakuwaje kama baada ya kuondoa wingu likasababisha mafuriko kutoka na hesabu kutoingia akilini?

Kuna hili pia. Watu 4 milioni sijui kwanini hawakupiga kura au kura zao hazikuhesabiwa? Wataalamu tupeni majibu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: