Heshima ya mwanamke kwanza, CCM baadaye


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

WANAHARAKATI wa masuala ya kijinsia, wengi wao wakiwa wanawake wanasema mwanamke ni mshirika mkuu wa mwanamume katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wanasema ndiyo maana aliumbwa baada ya ubavu wa Adamu kunyofolewa na kufinywa kiumbe kizuri Hawa. Wanasema kusudio la Mungu ni kumfanya mwanamke kuwa sawa na mwanamume kiutendaji na kifikra—siyo kuwa kiburudisho.

Udhalilishaji pekee wanaoukemea ni wa kupigwa na wanaume, kubakwa, kulazimishwa kuolewa, mirathi na kukeketwa.

Nakubaliana nao isipokuwa katika hili. Wanawake leo wote wamegeuka washangiliaji na washuhudiaji wa mfumo mpya wa udhalilishaji wa wanawake katika nyanja za siasa unaofanywa na wanaume.

Wamesahau kwamba umebuniwa mfumo mpya wa udhalilishaji unaotumika kwenye kampeni za siasa.

Kila chama cha siasa kimependekeza wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, miongoni mwao ni wanawake. Wanaume wanawapa nguvu na kusaidia washinde.

Lakini mara wakishinda, wanawake wenyewe huzua uvumi; mwanamke fulani ameshinda kwa sababu alimpa ‘nonino’ kigogo fulani na akishindwa inadaiwa ni kwa vile alimnyima nonino kigogo fulani.

Huu ni udhalilishaji unaofumbiwa macho na asasi zote zinazotetea haki na hadhi ya mwanamke na unazidi kuota mizizi.

Miaka ya mwanzoni mwa 1990 ziliibuliwa habari zilizokusudia kumchafua kiongozi mmoja kitaifa eti alimuoa mwanafunzi—hakukuwa na uthibitisho.

Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, mwanamke mmoja aliyeitwa Anjelina alitumiwa na watu waliodaiwa kuwa wapinzani wa mgombea urais, Augustine Mrema kumdhalilisha.

Mwaka 2000 kuna watu walimparamia Prof Ibrahim Lipumba eti hakuwa na mke. Aliwajibu wenye dada wampelekee wakaufyata.

Baada ya kustaafu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Omari Mahita kulikuwa na habari angewania ubunge kupitia CCM Jimbo la Morogoro Mjini.

Wapinzani wake wakafukua bomu kuwa alizaa na mtumishi wa ndani Rehema Shaaban.

Mwaka huu tunashuhudia wapinzani wa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Salaa kwamba ‘amepora’ mke wa mtu.

Sina uhakika na tukio la kiongozi mmoja wa kitaifa kumwoa mwanafunzi, lakini matukio mengine yote ni ya kweli. Kwamba ni kweli Mrema alizaa na Anjelina, kwamba ni kweli Mzee aliteleza kwa Rehema ni kweli Dk. Slaa anatarajiwa kumwoa Bi. Josephine ambaye ameachana na mumewe miaka mitatu iliyopita.

Hivi katika matukio hayo, nani anadhalilika? Nani anadhalilika mke wa mtu akifumaniwa na mume wa mtu? Kwa misingi ya usawa nitajibiwa wote.

Ikitokea mwanamume na mwanamke wamebaki uchi katika tukio la fumanizi, mashuhuda wa tukio—wanawake na wanaume—ni kweli wote watakuwa na ujasiri wa kuwatazama bila kuona aibu?

Au ni nani kati ya wawili hao atatafutiwa nguo haraka na kusitiriwa?

Kwa uzoefu wa matukio mbalimbali ya fumanizi mitaani, wanawake hujizuia kumtazama mwenzao akiwa mtupu, ndiyo maana humtafutia nguo haraka na kumsitiri.

Kama hivyo ndivyo, mwanamke ndiye anadhalilika zaidi kuliko mwanamume.

Fikiria. Anjelina alifikia hatua ya kuvua nguo akabaki uchi wa mnyama nje ya nyumba ya Mrema. Hapo nani alidhalilika? Kwa nini kumpinga Mrema iwe ni kwa gharama za ufedhuli kama huo?

Hivi kuna wanawake wangapi wamezaa nje ya ndoa zao na hatuoni wakitangazwa kwenye magazeti kama wake wa watangaza nia au wagombea?

Hivi ukosefu wa maadili ni kwa wagombea wapinzani wa kisiasa tu? Je, viongozi wa CCM hawana msururu wa vimada nchi nzima?

Je, CCM wanaturuhusu tutenge ukurasa kuanzia wiki ijayo tutaje nani alizaa na nani au mwanafunzi gani?

Tatizo hapa ni ushabiki mkubwa kwa CCM kwamba wanachofanya kila mmoja anadhani kuwa ni sahihi. Jamani, hadhi na heshima ya mwanamke kwanza, CCM baadaye.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: