Hila katika uandaaji katiba zitaligharimu taifa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

NILIPATA kusema awali na kuandika, kwamba damu iliyomwagika katika bara la Afrika baada ya ukoloni ni nyingi zaidi kuliko iliyomwagwa na wakoloni kwa ujumla wakati wa utawala wa mabavu dhidi ya mtu mweusi.

Miaka zaidi ya 50 tangu wakoloni waanze kufungasha virago katika bara hili, bado dunia inashuhudia umwagaji mkubwa wa damu usiopimika katika ardhi ya Afrika.

Mathalani, baada ya machafuko yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 na kusababisha takribani watu 1,000 kuchinjwa (samahani natumia neno baya kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kuwasilisha kimantiki mauji yale na watu wakaelewa isipokuwa ni kuonyesha ukatili huo kwa kutumia hilo neno), haikutarajiwa kwamba hali kama hii ya kumwaga damu ili kupata madaraka, bado ingevumilika katika bara hili.

Ukirejea vita vya wenyewe kwa wenywe vya Angola, Sudan, Sierra Leone, Liberia na sasa Somalia, Libya na Ivory Coast, nchi zote damu inaendelea kumwagika ili watawala wabaki madarakani ama kwa hila au kwa mabavu.

Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za bara hili ambako damu nyingi sana haijamwagwa ili watawala wasalie madarakani. Nasisitiza ‘si damu nyingi’ na sisemi ‘damu haijamwagika’ kwa sababu katika kutafuta madaraka tumeshuhudia nguvu za dola zikitumika kupita kiasi na kusababisha watu kufa, kupata vilema na hata wengine kwenda ukimbizini. Haya yametokea na wala asije akatokea mtu akaamini kwamba eti sisi ni tofauti sana na Waafrika wengine.

Ninarejea haya yote kwa sababu mchakato wa kuandika katiba mpya umeanza nchini  kwa kutayarisha muswada wa sheria ya kupitia katiba ambao unakusudia kutoa mamlaka ya kuundwa kwa tume ya kuratibu kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, kuandika ripoti na rasimu ya katiba hiyo kisha kuiwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muswada huo unawasilishwa katika mkutano wa tatu wa Bunge ulioanza jana mjini Dodoma. Baada ya serikali kutangaza muswada huo kwenye gazeti la serikali Machi 11, mwaka huu, wadau mbalimbali wameanza kujadili kwa kina muswada huo.

Jumamosi iliyopita Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) iliandaa kongamano kubwa lililowavuta pamoja wanasiasa, wanasheria, majaji wastaafu, wanaharakati, wanafunzi, wakulima na wafanyakazi, kujadili muswada huo.

Katika mjadala, ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV na Redio One, ujumbe muhumu ulitolewa.

Mengi yalizungumzwa, kuanzia muswada ulivyokwepa kujadiliwa kwa mambo ya msingi kama madaraka ya rais; ushiriki wa vyama vya siasa katika kupiga kampeni kuhusu mabadiliko ya katiba; madaraka makubwa kupita kiasi ambayo yamerundikwa kwa rais kuamua kuunda tume; kuteua wajumbe wake; kuwapa hadidu za rejea lakini pia kupokea ripoti ya tume ikishakamilisha kazi.

Ni dhahiri kwamba muswada huu umejaa hila, nia mbaya na kwa kweli mwisho wa mchakato hautasaidia Tanzania kupata katiba mpya na bora zaidi kuliko  iliyopo.

Kwa maneno mengine, muswada wa kutaka kuandikwa katiba mpya unajidhihirisha jinsi ambavyo watawala hawako tayari kufungua milango ya madaraka ili umma ushiriki kwa kina na kwa nia njema katika kutengeneza katiba nzuri na bora ambayo itasaidia kujenga taifa linalojali demokrasia na utawala bora.

Tayari joto la kisiasa limekwisha kupanda likijielekeza kwenye kitu kimoja; kwamba serikali haitaki na wala haina nia njema hata kidogo ya kusaidia taifa hili lipate katiba mpya. Ndiyo maana kwa mfano hata mwakilishi wa chama tawala aliyetumwa kutoa msimamo wa chama hicho kinachounda serikali, Prince Bagenda alisema kuwa katiba nzuri itapatikana kwa mapambano, bila shaka akikejeli wale wote waliokuwa wanadhani mchakato unaosimamiwa na serikali kwa sasa ungesaidia kupatikana kwa katiba mpya bora zaidi kuliko hii iliyopo leo.

Sote tunakumbuka kwamba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alipata kutajwa na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba ni nyota mpya ya Afrika kwa maana ya uongozi wake shupavu.

Leo wakimtazama Museveni hawathubutu hata kukumbuka kwamba walipata kumsifia. Huyu ni mtu ambaye ndani ya nafsi yake ameamua kufia madarakani. Tofauti ya Museveni na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ni umri tu, lakini nafsini mwao wanafanana katika kutamani kusalia madarakani.

Kwa Tanzania, kinachotaka kutokea ni hila, kwa maana ya kutengeneza sheria mbaya na kandamizaji ambazo tayari zipo nyingi tu ambazo zimepigiwa kelele lakini hazibadilishwi, ili kuhalalisha madai halali ya taifa hili kuwa na katiba mpya ambayo inaendana na zama za sasa na si hii ambayo kwa miaka mingi imekwisha kupitwa na wakati.

Wazungumzaji katika kongamano la kujadili muswada huo lililoandaliwa na Udasa, wakiongozwa na dhamira safi za nafsi zao, na kwa kiwango kikubwa kiu ya kuona taifa hili linaondokana na  sheria na mifumo kandamizi ili kwa pamoja taifa lipige hatua mbele katika mstari wa maendeleo, walionyesha udhaifu mwingi katika muswada huo.

Kama ilivyo ada, serikali imesonga mbele na muswada huo kama alivyonukuliwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, ambaye yeye binafsi haamini katika katiba mpya, wanauwasilisha muswada huo kama ulivyo na mapungufu yake, ingawa watasikiliza maoni ya wadau kama hayo ya wanakongamano.

Inawezekana, CCM inataka kutumia wingi wake bungeni kama ambavyo imekuwa ikiutumia mara nyingi kulazimisha kupitishwa kwa mambo ya ovyo ndani ya Bunge; hili linawezekana sana na inavyoelekea ndiyo mkao wa sasa.

Kwa kuwa hilo linawezekana kufanywa na CCM na serikali yake ili kujaribu kujenga kukubalika miongoni mwa jamii ya kimataifa kwamba wanafuata demokrasia na utawala wa sheria, ni vema pia wakajiweka tayari kwa mgogoro mkubwa wa kikatiba ambao aghalabu uzoefu katika nchi nyingi za Kiafrika matokeo yake hayajawahi kuwa mazuri kwa watawala.

Nilisema kuwa Tanzania haina tofauti sana na mataifa mengine ya Afrika ambako damu nyingi imemwagika, ila Tanzania kwa miaka mingi imefanikiwa kuzuia hayo kutokea kwa kutokuruhusu ung’ang’anizi sana katika madaraka.

Pengine busara hiyo ya kuepuka ung’ang’anizi katika madaraka safari hii ingeelekezwa kwenye kutambua jambo moja tu, kuwa katiba ni mali ya umma na ni umma tu wenye mamlaka ya kuitengeneza kwa utaratibu ambao utawahakikishia ushiriki wao kwa kiwango cha kutosheleza kiu yao. Ujanja ujanja huu safari hii utatugharimu vibaya. Hili ni angalizo muhimu kuanzia sasa na huko tunakoelekea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: