Hillary, Obama sasa jino kwa jino


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 April 2008

Printer-friendly version
Obama na Clinton

KINYANG'ANYIRO cha kuwania uteuzi wa mgombea urais kupitia Chama cha Democratic, sasa ni dhahiri kimepamba moto.

Wanasiasa wawili mashuhuri, Barack Obama na Hillary Clinton, wanazidi kukabana koo kila mmoja akitaka kumpiku mwenzake katika kusaka nafasi hiyo.

Lakini ni Obama anayeonekana kunufaika zaidi. Kwa sasa amebuni mbinu nyingine kwa lengo la kummaliza mshindani wake.

Anatumia ufundi mkubwa kujieleza kama alivyofanya katika mji wa Pennsylvania, alipotumia nafasi hiyo kumsambaratisha Hillary.

Akifanya kile ambacho washabiki wanataka, Obama alitumia kila fursa aliyoipata kujijenga na kuhakikisha mshindani wake hawezi tena kujipa matumaini. Hatua kwa hatua, alihakikisha Hilarry anatokomea kisiasa.

Hatua hiyo imemfanya kujiongezea nafasi zaidi za kushinda katika hatua hii ya awali. Lakini ushindi wake utatokana na kile wengi wanachokiita, "kufanya vizuri katika hatua inayofuata."

"Hadi sasa anaongoza. Lakini hii haijamhakikishia nafasi ya moja kwa moja ya ushindi," anasema mmoja wa wanaomuunga mkono.

Anasema, "mchuano bado ni mkali maana mpaka sasa, kura zinaonyesha kwamba Clinton anaweza pia kufanya vizuri, iwapo Obama atachemsha huko mbele."

Obama kuweza kuhimili vishindo vya Hillary, ni ishara njema. "Amejitahidi kwa kusema kile wanachotaka kukisikia Wamarekani wengi," anasema mwanamama mmoja wa Pennsylvania. "Kama Clinton anataka kushinda, lazima afanye kazi ya ziada."

Akitamba anasema, "Hakuna atakayemzuia Obama kuwa mgombea. Tayari tumemaliza kazi ya kumshughulikia Hillary katika miji mbalimbali. Na leo tumemmaliza hapa Pennsylvania."

Anasema mbinu aliyotumia Obama katika duru hiyo ya kampeni, imezidi kumuongezea wafuasi; hata wa maafisa wa chama cha Democratic wanaojulikana kama superdelegates wameendelea kumuunga mkono.

"Hawa ni watu muhimu sana katika kampeni za Democratic. Kuzidi kuvuna wafuasi kutoka kundi hili, hakika kunaonyesha wazi kwamba Hillary amemalizika," anasema.

Kwa ujumla, kampeni za 21 Aprili zilikuwa za kushambuliana; wakati Obama akimponda Hillary, naye pia akirushiwa makombora.

Kwa upande wake, Hillary alilishambulia bango jipya la kampeni la Obama linalotangaza mpango wake mpya wa afya alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara jijini New York.

Hillary akawataka wapiga kura kumpuuza Obama na kumchagua yeye kwamba ana uwezo wa kukabiliana na matatizo mazito yanayolikabili taifa.

"Nataka kila mmoja afikiri kwa kina, acheni kuchukulia mambo kirahisi rahisi mpeni mtu anayeweza kushughulika na masuala mazito ya kitaifa," anasema Hillary kumaanisha kwamba ni hodari zaidi ya Obama.

"Badala ya kujadili atakavyokabili matatizo na changamoto zinazowakabili Wamarekani, yeye anakuwa mstari wa mbele kunishambulia."

Hillary aliwataka kufikiria tishio linalokuja la kutokuwepo uwiano wa kibiashara baina ya China na Mashariki ya Kati, pamoja na ongezeko la mzigo wa madeni.

"Sitaki tu kuzungumza kauli za kiujumla jumla kwa ajili ya kufurahisha Wamarekani, nataka kila mmoja atafakari kwa kina masuala haya," anasema Hillary.

"Naweza nisiwe na uhakika zaidi, lakini nitawaelezeni chochote ninachokifikiri kinafaa na nitawaeleza wapi ninaposimamia," alisema.

"Huyu mwanamama anayebadilika badilika misimamo katika masuala muhimu kama biashara au hata kuhusu vita hawezi kufaa kwa siasa tulizonazo sasa? anapobanwa katika masuala ya msingi, anaruka. Hiyo ndiyo staili ya Washington unaweza kusema jambo fulani hapa na ukazungumza jambo jingine kwingine, mimi siko hivyo," alisema akimponda Hillary.

0
No votes yet