Hisia za ubaguzi wa rangi zakoroga Afrika Kusini


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version

WAKATI nikitoka katika ofisi za gazeti la Mail and Guardian la Afrika Kusini zilizopo katika mtaa wa Jan Smuts mjini hapa juzi, nilipanda teksi iliyokuwa ikiendeshwa na mzungu aliyejitambulisha kwa jina moja la Klaas.

Tukiwa safarini, tulikuwa na mjadala mkali uliokuwa ukihusu baadhi ya matamshi yake ambayo mimi niliyatafsiri kama ubaguzi wa rangi. Kwa maoni yake, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ndiye Mtu mweusi aliyeelimika kuliko wote ndani ya chama tawala cha African National Congress (ANC) nchini Afrika Kusini.

Anadai kwamba Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma hajaelimika kabisa. Na lawama hizo zikatupiwa pia kwa Rais wa Umoja wa Vijana wa ANC, Julius Malema.

Mimi nikapingana naye kwa hoja mbili. Kwanza nikasema suala la elimu ni pana sana. Kwamba ninawafahamu watu ndani ya ANC wenye elimu kubwa kuliko ya Thabo Mbeki kama kigezo cha mtu kuelimika ni kuingia darasani.

Lakini pia nikasema, mtu hawezi kudai kwamba babu wa mababu zetu walioishi zamani hawakuwa na elimu eti kwa vile hawakuingia darasani. Kwamba elimu si kuingia darasani pekee. Kikubwa zaidi, nikasema kama Mbeki angekuwa ameelimika, asingekataa wananchi wake wafe kwa Ukimwi huku serikali yake ikikataa wasitumie vidonge vya kurefusha maisha maarufu kwa jina la ARV’s.

Kuhusu Zuma, hoja yangu ikawa kwamba kwa vile hadi sasa hakuna tuhuma kwamba uchaguzi uliomwingiza madarakani ulichafuliwa, basi yeye ni kiongozi halali wa Afrika Kusini.

Ni kimantiki tu na hili limesemwa pengi kwamba wananchi wa eneo humchagua kiongozi wanayeona anawafaa. Kama Zuma hana elimu basi kuna mawili; ama wananchi wa Afrika Kusini kwa ujumla wao hawana elimu au wanapenda watu wasioelimika.

Ulikuwa mjadala mrefu na mkali, lakini chanzo chake kilikuwa Malema, mwanasiasa aliyezaliwa mwaka 1981 tu lakini mawimbi ya siasa zake yanaitikisa nchi hii hivi sasa.

Kwa Waafrika Kusini walio wengi, Malema ni sawa na kichaa ambaye bado anaishi katika zama za ubaguzi wa rangi. Vitendo vyake katika siku za karibuni vinathibitisha hilo.

Kwanza ni kitendo chake cha kuimba wimbo ambao ni maarufu wa “Ayasab' amagwala” yaani Waoga wanaogopa, ambao ndani yake kuna kipande kinachoimbika kama “Dubul' ibhunu” yaani ua Kaburu.

Kwa lugha ya Kiafrakana, neno Boer ambalo kwa Kiswahili linatafsirika kama kaburu lina maana ya mkulima. Kihistoria, wengi wa wazungu ma-Boer walikuwa wakulima na kwa watu weusi wa Afrika Kusini, Boer maana yake ni sawa na Kaburu kwa Mswahili.

Machi 10 mwaka huu, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Thaba Nchu, nje ya jiji la Johannesburg, Malema aliimba hadharani wimbo huo ambao umepigwa marufuku na Mahakama Kuu ya Afrika Kusini.

Wiki tatu baadaye, kiongozi wa chama cha makaburu wenye msimamo mkali, Eugene TerreBlanche, akauawa na wafanyakazi wake shambani kwake. Wazungu na makaburu wakachachamaa. Wakasema wimbo huo wa Malema umesababisha kifo cha TerreBlanche.

Lakini Malema anapinga kwamba kifo cha kaburu huyo hakina uhusiano na wimbo huo wa ANC. Anajitetea kwamba wimbo huo ulianza kuimbwa zamani na ni sehemu ya historia ya chama chake.

Wiki iliyopita Malema aliibuka tena. Alikwenda nchini Zimbabwe kwa ziara ya kichama ambako alitoa matamshi yenye utata na ambayo hayakupokewa vema nchini kwake.

Malema alidai kwamba Waafrika kwa ujumla wao wanapaswa kumuunga mkono Rais Robert Mugabe. Akamponda Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai kwamba ni kibaraka wa Wazungu.

Akaenda mbali zaidi. Akamwomba Zuma naye afanye kama Mugabe. Agawe mashamba kwa watu weusi ili amalize utegemezi wa Wazungu kwenye uzalishaji wa chakula.

Hapo sasa akawa amegusa pabaya. Hii ni kwa sababu Zuma ndiye msuluhishi wa mgogoro wa Zimbabwe na inajulikana ya kuwa Malema ni miongoni mwa viongozi wa ANC waliofanya makubwa kumwingiza madarakani.

Ilikuwapo hatari ya kuonekana kwamba alichokisema Malema kina baraka za Zuma. Na hili lingekuwa jambo la hatari kwa ustawi wa Afrika Kusini ambayo ndiyo kwanza inajiponya majeraha ya sera za ubaguzi wa rangi.

Na ikumbukwe, bado kuna wazungu ambao hawana imani na Zuma. Huyu ni mwanasiasa ambaye wakati wa kampeni za kuwania urais, alikuwa akiimba na kucheza wimbo maarufu wa zama za kibaguzi wa “Lethe Mshini Wami” yaani Niletee bunduki yangu.

Zuma ameibuka mwishoni mwa wiki iliyopita na kudai kauli za Malema hazina uhusiano wowote na kifo cha TerreBlanche kwa namna yoyote wala ANC.

Kwamba yeye na ANC kwanza hawana uhusiano na kundi lolote baina ya Mugabe na Tsvangirai na pia hawana mpango wa kugawa mashamba kwa weusi kama alivyofanya Mugabe. Zuma naye akaenda mbali zaidi.

Akasema kauli zinazotolewa na wanasiasa wa aina ya Malema ni za kuogopwa kama ukoma. Hapo Malema akawa ametoneshwa kidonda.

Kesho yake akaibuka na kueleza kushangazwa kwake na kauli ya rais wake. Akasema hata Thabo Mbeki (adui mkubwa wa Malema ndani ya ANC), hakuwahi kumsema kiongozi wa chama hicho hadharani.

Akasema utaratibu wa ANC ni kwa viongozi kusemana ndani ya vikao vya chama (kama CCM?) na si hadharani. Kwa maelezo, haamini kama ni Zuma mwenyewe aliyetoa kauli hizo. Wanasiasa! Juzi, aliibuka Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Montashe na kukandamiza kile alichokisema Zuma. Inaonekana chama tawala sasa kimechoka na Malema.

Kiongozi huyu wa Vijana wa ANC anajua kuna kundi la watu walio nyuma yake. Vijana wasio na elimu ambao hawapati fursa za kiuchumi na wameshindwa kupata maendeleo hata baada ya kwisha kwa siasa za ubaguzi.

Na kama walivyo wanasiasa wengi, Malema hazungumzi kile anachokitenda. Nitakupa mfano mmoja kueleza kwa nini naamini hili.

Alipokuwa Zimbabwe mwezi uliopita, alimlaumu Tsvangirai kwa uamuzi wa kuishi eneo la Sandton la watu wenye kipato cha hali ya juu jijini Harare.

Huo ni uasi mkubwa, kwa maoni ya Malema na kwa weusi wanaoteseka kiuchumi. Cha ajabu ni kwamba, yeye mwenyewe alikuwa akiishi Sandton katika wakati wote alipokuwa Zimbabwe!

Kilichowazi ni kwamba anataka kutumia shida za weusi kujiongezea nguvu za kisiasa. Na hata kama Zuma anakubaliana naye katika baadhi ya mambo, anafahamu hawezi kuwa mjinga.

Watu weupe ndio wanaoshikilia uchumi wa Afrika Kusini. Wao wanaweza kuamua kuiharibu nchi hiyo kiuchumi katika namna ambayo wengi wanaweza kuifikiria tu.

Waafrika (makaburu) wanaamini Afrika ndiyo kwao. Kwamba wao na watu weusi ndio pekee waliopewa ardhi ya Afrika na Mungu kwa ajili ya kuitawala. Hawaendi kokote.

Lakini vuguvugu hili la Malema na watu wa aina yake linawafanya waanze kufikiria mara mbili kuhusu mustakabali wao ndani ya nchi ambayo babu wa babu zao walizikwa.

Ni kipindi kigumu kwa Afrika Kusini. Ni kipindi ambacho Afrika kwa ujumla inatakiwa kuomba kipite haraka. Ni kipindi cha hatari.

0
No votes yet