Historia kuzibeba, kuziangusha Simba, Yanga SC


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia 14 hadi 28 Julai 2012.

Mashindano hayo makubwa, katika ukanda wa Afrika Mashariki hushirikisha klabu bingwa kutoka nchi wanachama wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) lakini Tanzania itawakilishwa na klabu tatu.

Katika michuano hiyo Tanzania itawakilishwa na nchi nne, tatu kutoka Bara na moja Zanzibar. Klabu kutoka Bara ni mabingwa wa soka nchini, Simba; washindi wa pili, Azam, na mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga, wakati kutoka Zanzibar ni Mafunzo.

Ratiba ya michuano hiyo imetolewa na klabu 11 kutoka nchi wanachama wa Cecafa. Siku hiyo ya ufunguzi kutakuwa na mechi mbili ya kwanza itakuwa kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini halafu Yanga na Atletico ya Burundi.

Kundi A litakuwa na timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya DR Congo na Ports ya Djibouti. Katika Kundi B kutakuwa na Azam, Mafunzo na Tusker ya Kenya  wakati Kundi C litakuwa na klabu za Yanga, APR, Wau Salaam  na Atletico.

Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili.

El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika nchini kwa mwaka wa pili mfululizo.

Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh kati ya 13-15 Julai mwaka huu itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Bingwa wa michuano hiyo atapata dola 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000.

Gumzo la wadau wa soka nchini ni kuhusu uwezo wa klabu hizo nne kulibakiza kombe hilo tena mwaka huu.

Wale wanaotazama wachezaji waliosajiliwa na klabu hizo msimu huu, hasa Simba na Yanga wanatamba kuwa kombe halitaondoka.

Pia wanaotazama historia ya michuano hiyo ikifanyika nchini, nao wanatamba kwamba kombe litabaki nchini hivyo kutwaa tuzo ya mshindi wa kwanza na huenda ya pili kama ilivyokuwa mwaka jana.

Jangwani wanajipa moyo zaidi na kinachowapa imani hiyo ni ushindi wa mabao 2-1 ambayo Yanga ilipata katika mechi ya kirafiki dhidi ya Express ya Uganda. Simba wamejishika pumzi baada ya kutoka sare mara mbili na klabu hiyo, japo imepata matokeo mazuri katika ziara yake ya kutembeza kombe Kanda ya Ziwa.

Uwezo wa Azam FC katika michuano hii haujulikani, lakini wanaweza kushtua klabu kongwe kama ambavyo ilifanya iliposhiriki kwa mara ya kwanza na kutwaa taji la Kombe la Mapinduzi.

Japo Azam imejitokeza kuwa tishio hata kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Bara, macho na masikio ya wadau wa soka yako kwa klabu za Simba na Yanga.

Simba wanategemea historia zaidi kwamba inaposhiriki michuano inayofanyika nchini – Bara au Visiwani – ina bahati ya kutwaa kombe hilo. Simba ilitwaa kombe hilo ilipofanyika Bara 1974, 1991, 1992 (Zanzibar), 1995 na 1996. Mwaka 2002 Simba ilitwaa pia kombe mjini Zanzibar.

Simba haina rekodi ya kutwaa kombe hilo nje ya Bara na Zanzibar wakati Yanga imekuwa na bahati mara mbili mjini Kampala, mara moja Zanzibar na mara moja Dar es Salaam.

Yanga imebahatika kutwaa kombe hilo mwaka 1975 mjini Zanzibar; mwaka 1993 na 1999 Kampala, na 2011 Bara.

Hata hivyo, michuano hiyo ilipofanyika nchini mara mbili na mara moja Zanzibar kati ya mwaka 1976 na 1990, kombe hilo lilinyakuliwa na klabu nyingine. Kwa hiyo, michuano kufanyika nchini si tiketi ya kulibakiza.

Mwaka 1977 Simba ilitolewa na Luo Union ya Kenya hatua ya nusu fainali Dar, na mwaka 1986 Yanga ilifungwa kwa mikwaju ya penalti na El Marreikh ya Sudan.

Aidha, mwaka 1998 Rayon Sports ya Rwanda iliiacha Mlandege ikiwayawaya kwa kichapo cha mabao 2-1 mjini Zanzibar na kuondoka na kombe.

Mwaka 2005 Simba ilifungashwa mapema; mwaka 2006 Yanga ililala mapema lakini Moro United ilitolewa katika fainali na Polisi ya Uganda; mwaka 2008 Simba na Yanga ziliacha kombe likatoka.

Viongozi wa klabu zote nne Azam FC, Mafunzo, Simba na Yanga wajue  mafanikio yako katika mazoezi na mbinu za mchezo siyo historia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: