Historia ya utumwa mgodi wa North Mara


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Gumzo

EMONGO au Chimongo, kwa kabila la Wakurya, ni aina ya wadudu wanaovamia na kula mazao yaliyoko ghalani au yaliyorundikwa mahali kwa nia ya kuyahifadhi.

Neno hilo ndilo chimbuko la jina Nyamongo, eneo maarufu kwa madini ya dhahabu, katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Bali katika mazingira ya leo, chimongo ni makampuni “yanayotafuna” madini na kujineemsha, huku yakiacha wananchi wakiwa hohehahe.

Chimongo wa kisasa ni kampuni ya East Africa Gold Mines (EAGM) iliyotangulia kuchimba madini katika eneo hili; halafu Placer Dome na sasa Barrick Goldmine.

Awali eneo hilo walikuwa wanaishi Wakurya wa ukoo wa Wakenye. Inasimuliwa kuwa mzee mmoja aliyeishi hapa alikuwa na mabinti ambao Wakurya wa ukoo wa Waracha waliamini kuwa wakiwaoa hupata bahati.

Ikawa hivyo. Waracha walioa mabinti wa mzee huyo wa Kikenye ambaye baadaye alihama eneo hilo kupisha wakwe zake. Baadaye kabisa wakazi wa eneo hilo wakaja kugundua hazina kubwa ya dhahabu chini ya ardhi yao.

Walianza kuchimba dhahabu. Walitumia vijiti, majembe, sululu na chochote chenye ncha; walipata dhabu na mamilioni ya shilingi. Hapo ndipo uchimbaji ulipogeuka kazi ya kila siku na kuchukua nafasi ya kilimo.

Bali leo wachimbaji wa asili wametupwa nje ya ardhi na utajiri wao. Wanatakiwa kuwa watazamaji tu. Mbele yao kuna uzio unaowatenga na kampuni ya uchimbaji madini.

Nyamongo walipoteza dhahabu yao mwaka 1995 wakati viongozi wa vijiji vitano katika kata tano za eneo hili, walipoiuzia EAGM hekta 671, yakiwemo makazi, mashamba na machimbo ya Nyabirama na Nyabigena.

Jay Taylor, Rais na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Placer Dome iliyorithi EAGM, anasema kampuni ilimilikishwa eneo la kilomita za mraba 423 chini ya mkataba maalum.

Lakini mwenyekiti wa kitongoji cha Mjini Kati Nyangoto, Juma Marura anasema, “Hakuna mkataba; kama wamiliki wa sasa, Barrick wanadai kuna mkataba, basi watuonyeshe muhtasari wa kikao kilichoridhia sisi kuingia nao mkataba.”

Mratibu wa Sheria na Haki za Binadamu Tarime (Shehabita), Bonny Matto anasema orodha za waliohudhuria mikutano ya hadhara ya kawaida, “ndizo zilitumiwa kama vikao vya walioridhia mkataba.”

Hivyo ndivyo makampuni ya kigeni, kwa msaada wa viongozi wa serikali, yalivyonyang’anya Wanyamongo ardhi na dhahabu yao.

Juma Marura anakumbuka ziara ya Rais Jakaya Kikwete mgodini hapo mwaka jana. “Alikuja hapa na kuzungumza na mwekezaji. Baadaye akatuambia atasaidia kuwepo mazungumzo ili tusiuawe na askari wa mgodini; tuletewe maji safi, tupate umeme na fidia ifanyike kisheria,” anaeleza.

“Lakini siku hiyo hiyo alipoondoka rais, askari wa mgodini waliua mwananchi mmoja aitwaye Mussa Werema Nyahiri. Na hadi leo hakuna maji safi wala umeme; na sumu itokanayo na kemikali za mgodini, bado inatiririkia kwenye makazi ya wananchi,” anasimulia Marura.

Hata hivyo, Marura anasema heri Kikwete kuliko Mkapa (Benjamin, rais mstaafu). “Mkapa alitoka mgodini akiwa amefunga vioo vya giza. Hakutusikiliza kabisa.”

Kitanzi cha Wanyamongo ni barua iliyoandikwa na kusainiwa usiku na viongozi 15 mjini Musoma, tarehe 22 Julai 1995.

Siku mbili baadaye (24 Julai 1995), viongozi haohao walitia saini “makubaliano” ya kuwa na ubia na EAGM bila kushirikisha wenye migodi midogo na wenye nyumba, mashamba na mali nyingine katika eneo karibu na mgodi.

Ilikuwa baada ya kuona wameingia katika kashfa, viongozi hao – watatu kutoka kila kijiji (katika vijiji vitano), walianza kuitisha mikutano kuhalalisha uporaji. Mkutano wa kwanza ulifanyika Agosti 1995.

Barua iliyoidhinisha uporaji (ya 22 Julai) na ambayo iliandikwa kwa Kiingereza na kupelekwa kwa aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Jackson Makweta, ndiyo inatumika kama “mkataba.”

Barua hiyo inasema, pamoja na mambo mengine, kuwa “…kampuni ya East Africa Gold Mine ina utaalamu wa kutosha na raslimali fedha kuendelea kuchimba na kufanya utafiti katika eneo tulilomilikishwa.

“Tumeshuhudia EAGM ikiajiri vijana wengi kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi … Tuna imani kubwa ubia wetu na EAGM utatufikisha katika kilele cha mafanikio ambacho tuna shauku nacho sana,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Katika barua hiyo ya “kuomba utumwa,” viongozi waliandika, “Kwa hiyo, tunawasilisha maombi ya leseni ya uchimbaji wa pamoja kama hatua ya kwanza ya maendeleo.”

Ni maoni ya wengi waliohojiwa kwamba barua hiyo iliyoandikwa katika Kiingereza safi, ilitungwa na Wizira ya Maji, Nishati na Madini, au ofisi ya EAGM.

Waliouza “nchi ya Nyamongo” – watu na utajiri wao, ni mwenyekiti David Sasi, afisa mtendaji Marwa John na mwakilishi Ibrahim C. Sererya; wote kutoka kijiji cha Genkuru kata ya Gorong’a.

Kutoka Kerende, kata ya Nyamwaga ni mwenyekiti Gideon Jackob Magaga, afisa mtendaji Polycap Joseph Range na mwakilishi Mussa Ibrahim Mangure; wakati kutoka kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga walikuwa mwenyekiti John Joseph Mugini, afisa mtendaji Protas Marwa Mwita na mwakilishi Aloyce Chacha.

Kutoka kijiji cha Kewanja, kata ya Kemambo watia saini ya “utumwa” walikuwa mwenyekiti Robert Mwita Mititi, afisa mtendaji John Matera Mang’era na mwakilishi Joseph Marwa Marwa.

Kutoka kijiji cha Nyangoto kata ya Matongo-Nyangoto walikuwa mwenyekiti Charles B. Machage, afisa mtendaji Dickson Ntora Mwita na mwakilishi Ihande Maki.

Huu ndio ulikuwa mwanzo wa “emongo” – EAGM, kumeng’enya wapendavyo madini ambayo wananchi walipewa na Mwenyezi Mungu.

Lakini waliomkaribisha “emongo” wa kigeni wameanza mbinu mpya ya kijisafisha kwa kutumia wananchi.

Kwa mfano, viongozi hao wanatumia muhtasari wa mkutano wa 11 Agosti 1995, siku 19 baada ya “mkataba wa utumwa” – kama unavyoitwa hapa – kuwa ndio chanzo na idhini ya kuingia mkataba na EAGM. Hili tayari wananchi wameling’amua.

Mkutano huo wa hadhara uliitishwa na mwenyekiti wa kijiji cha Kewanja kata ya Kemambo, Robert Mwita Mititi na ofisa mtendaji, John Matera Mang’era.

Kwa mujibu wa muhtasari wa mkutano wa hadhara, wananchi waliridhia ubia na EAGM kwa kuwa wenye mashimo (migodi midogo iyaliyochimbwa kwa mikono) wangelipwa Sh. 12,000 kama fidia kwa kila mita moja ya shimo.

Aidha, muhtasari unasema wananchi walitaka “…wakati mkataba huu utakaposainiwa (hawakuambiwa hilo lilikuwa limetekelezwa), kijiji kipate mwanasheria wa serikali atakayepitia kifungu hadi kifungu kuona iwapo unalenga kunufaisha wananchi wa Kewanja…ndipo mkataba uanze kutumika na si vinginevyo.”

Hiyo ilikuwa ghiliba. Migodi yao midogomidogo tayari iliishakwenda kwa “mwekezaji” tangu 24 Julai kutokana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuridhia eneo kuchukuliwa na EAGM kwa madai ya ubia.

Kampeni za kufanya wananchi wahalalishe kilichokwishatendeka ziliendelea katika kijiji cha Nyangoto (31 Agosti 1995) na baadaye katika vijiji vingine.

Kama ilivyofanyika katika vijiji vingine, mkutano wa Nyangoto ulimalizika kwa wananchi na wenye mashimo yaliyo karibu na mgodi kukubali “mkataba wa ubia na EAGM na kuanzisha mgodi katika machimbo ya Nyabigena.”

Taarifa ya kikao inasema mkutano ulikubali, pamoja na mambo mengine, kampuni iendeleze shule ya sekondari Nyamongo hadi kidato cha V na VI, ijenge shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Nyarero, ichimbe lambo na ifanye fidia kwa wenye mashimo kuwa Sh. 5,000 kwa mita (siyo Sh. 12,000).

Hata hivyo, kampuni ilikataa kufanya mambo matatu: kulipa asilimia 25 ya pato lake badala ya asilimia moja katika mfuko wa dhamana ya elimu, kujenga chuo cha maendeleo ya kina mama na kusomesha yatima.

Wakati EAGM ikijadiliana na viongozi wa vijiji, tayari ilikwishanunua eneo la mgodi lililokuwa chini ya raia wa asili ya kiasia (Mhindi) aliyefahamika kwa jina moja la Kumar.

Kumar alikumbwa na maradhi. Akarudi India. Akaacha mgodi mikononi mwa Enock Isack aliyekuwa mtu wake wa karibu kibiashara. Taarifa zinasema Isack alimwomba nduguye Josephat Isack.

Ni Josephat aliyeuza mgodi na eneo hilo la
mu-asia kwa EAGM na kupewa nafasi ya juu ya uongozi mgodini, fursa anayodaiwa kutumia kushawishi wananchi kuachia mali zao kwa matarajio ya wao kupewa ajira.

Pamoja na wananchi wengi kumkatalia Josephat baadaye walikuja kushangaa walipoona wanafukuzwa kwenye maeneo yao kwa madai kuwa ni “mali ya mgodi.”

Lugha ya Kiingereza ilikuwa nyenzo kuu katika kuandaa na kusaini nyaraka za mazungumzo kati ya EAGM na viongozi wa vijiji. Ingawa kulikuwa na tafsiri ya Kiswahili, ukichunguza utaona kuwa nyaraka za Kiingereza zinatofautiana na zile za Kiswahili.

Uchunguzi unaonyesha wakati katika Kiingereza malipo ya Sh. 12,000 ni kwa futi moja katika mwamba wenye madini; katika nyaraka za Kiswahili malipo hayo yanasomeka Sh. 12,000 kwa mita moja.

Aidha, kampuni ilifikia kukubali malipo ya Sh. 150,000 kwa ukubwa huohuo badala ya Sh. 12,000, lakini nyaraka za Kiswahili ziko kimya kuhusu hilo.

Katika baadhi ya nyaraka za Kiingereza, Wanyamongo wanaonekana kujifunga kupokea fidia ya hata Sh. 5,000 kwa mita moja.

Kabla ya kujitoa, EAGM ambayo ilitambuliwa pia kwa Kiswahili kama Afrika Mashariki Gold Mine (AMGM), ilifanya kazi kwa ubia na kampuni ya Placer Dome ya Canada ambayo nayo ilikuja kuacha mzigo wa matatizo kwa Barrick, pia ya Canada.

Kwa hiyo, madhira yaliyokuwa yatatuliwe na EAGM au Placer Dome sasa yameiangukia Barrick inayoshutumiwa kwa kuvujisha maji yenye sumu kwenye vyanzo vya maji – visima, mto Timbo na mto Tigithe kabla ya kuingia Mto Mara na kwenda Ziwa Viktoria.

Baada ya Barrick kuelemewa na madai ya fidia ya mashamba yaliyoporwa, mashimo ya madini, visima, nyumba zilizobomolewa na tishio la ghasia, mwaka 2008 ilikubali kukutana na wananchi.

Pande mbili hizo ziliunda kamati ndogo ya wanasheria iliyopitia upya hicho kinachodaiwa kuwa “mkataba” kati yake na vijiji.

Taarifa ya kamati ndogo ya maridhiano ya kupitia mikataba ya uchimbaji madini kati ya vijiji vitano vya Genkuru, Kewanja, Kerende, Nyangoto na Nyamwaga iliyotolewa 21 Oktoba 2008 ilifichua mambo kadhaa na ikatoa mapendekezo.

Kamati inaonyesha, katika taarifa yake, kwamba “mikataba ya vijiji na kampuni yote inafanana.”

Kwamba “kuna mikataba ya Kiswahili ambayo inatambua ununuzi na malipo ya ubia. Mikataba hiyo ni tafsiri ya mikataba ya Kiingereza ambayo haina neno ubia; badala yake kuna neno royalty (mrabaha).

Kwa ufupi, “mikataba” iliyoandikwa kwa Kiingereza, inatambua ununuzi na malipo ya mrabaha, wakati mikataba ya Kiswahili inatambua ubia.

Vilevile, kamati hiyo iligundua tofauti kubwa kati ya mikataba na viambatisho vyake vyote kwamba wananchi hawakuelezwa/hawakuelewa vizuri maana ya kile kilichokuwa kinafanyika.

Kwa kuwa ilionekana wazi kuna kasoro katika “mikataba” hiyo, kamati ndogo iliyokuwa na wanasheria wa kampuni ya Barrick na wanavijiji ilipendekeza, “Vijiji na Barrick kwa pamoja, kwa kutumia kamati za maridhiano, tufanye kwa pamoja marekebisho ya maandishi kwenye ‘mkataba’ wa vijiji na kampuni wa 24 Agosti 1995.”

Pendekezo hilo halijafanyiwa kazi kama ilivyo kwa pendekezo la fedha zote zinazotolewa na kampuni kwenda kwenye vijiji kupitia akaunti ya kijiji ili kuwepo kumbukumbu vijijjini na kutangazwa kwa jamii kwa kila mmoja kujua.

Hakuna ushirikishwaji wa wataalamu kutambua thamani ya fedha kwa miundombinu; hakuna ufuatiliaji wa miradi ya vijiji; hakuna mkaguzi wa mapato na matumizi.

Kampuni haijajenga miradi ya maji au kushirikisha serikali za vijiji katika hilo, wala haiongei na jamii vijijini.

Barrick imegoma kutekeleza mapendekezo haya na mengine mengi, ambayo kimsingi yalipaswa kutatuliwa hata kabla maeneo ya wananchi kuchukuliwa.

Wanyamongo ambao waliacha kilimo ili wachimbe madini, sasa hawana ardhi wala dhahabu. Vyote viliuzwa na wawakilishi wa utawala, tena kinyemela.

Swali ni: Nani atarejesha haki za Wanyamongo – kuwashirikisha katika uvunaji au hata mafao yatokanayo na uvunaji dhahabu katika maeneo yao ya asili?

0
No votes yet