Hivi ndivyo TFF inavyodidimiza soka


Salim Said Salim's picture

Na Salim Said Salim - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Michezo
Leodgard Tenga, Rais wa TFF

KWA muda mrefu Watanzania wamekuwa wakisononeshwa na kutofanya vizuri kwa timu yao ya taifa ya kandanda, Taifa Stars, katika medani ya kimataifa.

Pamekuwa na mlolongo wa sababu na visingizio kwa timu hii kutofanya vizuri. Huyu anasema hili na yule anasema lile.
Wapo wanaofikiria ni uteuzi mbaya wa wachezaji, wapo wanaodhani ni maandalizi duni na wapo wenye mawazo kuwa timu hii bado haijapata mwalimu mzuri anayeweza kufichua vipaji na kuvinoa ili baadaye Tanzania iweze kung’ara katika soka la kimataifa.
Lakini lipo kundi linalojenga dhana kuwa wachezaji wanajali zaidi klabu zao kuliko timu ya taifa kwa sababu klabu zinajali zaidi maslahi na maisha yao kuliko ilivyo kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).
Hili la mwisho, kama utalifanyia tathmini, utaliona halina ubishi na lipo wazi. Sio haki na unaweza kusema kuwalaumu wachezaji kwamba wanatoa umuhimu mkubwa kwa klabu zao kuliko timu ya taifa ni kuwaonea. Ni desturi ya bunaadamu mwenye akili timamu kumjali mtu anayemthamini na kwa maana hiyo wachezaji wetu hawana makosa.
Hii inatokana na kuona wenzao waliowatangulia kuchezea timu ya taifa hawathaminiwi na TFF wanaonekana kama vinyago. Bado ninakumbuka namna ambavyo hali hii ilivyomtibua Waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni na Michezo, hayati Daudi Mwakawago na kuamua kuunda tume ya uchunguzi na kutoa mapendekezo yake.
Nilibahatika kuwa mmoja wa wajumbe watano wa tume hiyo iliyoongozwa na Balozi Makame Rashid karibu miaka 30 sasa na mimi nilichaguliwa kuandika ripoti iliyowasilishwa kwa waziri baada ya kupitiwa na wajumbe wenzangu kwa kuzingatia mawazo na ushauri tulioupata. Tulitembea karibu nchi nzima kukutana na wachezaji, viongozi wa klabu, wanasiasa na mashabiki.
Miongoni mwa mapendekezo yetu ni kwa wachezaji wa zamani, sio tu kuona wanakumbukwa na kuheshimiwa, bali pia waone mchango wao kwa timu ya taifa unathaminiwa.
Tulipendekeza wachezaji walioitumikia timu ya taifa kwa miaka mitano wapatiwe vitambulisho maalum vya kuwawezesha kuingia mpirani bila ya malipo. Wale waliochezea zaidi ya miaka mitano na kuendelea, wawe na vitambulisho vinavyowawezesha kufuatana na mtu mmoja kama mgeni wake.
Kwa wale ambao watakuwa wamechezea Taifa Stars kwa miaka 10 na zaidi na ambao hata wakati mmoja hawatimii wachezaji 30 wakiwa wametawanyika sehemu mbalimbali za nchi yetu wawe na kitambulisho cha kufuatana na mtu mmoja na kuweza kukaa jukwaa kuu (VIP).
Vilevile watu wapatiwe kitu kama posho maalum ya angalau nusu ya mshahara wa kima cha chini kwa serikali, kila mwezi.
Kwa bahati mbaya, mapendekezo yale hayakufanyiwa kazi na Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) wala Chama cha Soka Tanzania (FAT) na sasa TFF. Nilidhani TFF mpya ambayo viongozi wake wengi ni wachezaji wa zamani watawakumbuka wenzao. Nilifarijika niliposikia mwaka jana TFF imewakumbuka (na mimi walinikumbuka kama mwandishi mkongwe wa michezo katika mkusanyiko ule wa Agosti mwaka jana).
Nilifurahi sana kuwaona baadhi ya hawa wazee, wakiwemo wale tulioonana mara ya mwisho zaidi ya miaka 30 iliyopita. Baadhi yao walikuwa wamechoka kimaisha kutokana na hali ngumu ya maisha kule wanakoishi.
Wapo waliokuwa wanasaidiwa kutembea kwa magongo na wapo ambao wanachechemea kwa kuvunjika miguu wakati wakivaa jezi za Taifa Stars. Baada ya sifa nyingi za kuelezea mchango wao kwa taifa hili wazee hawa walitunukiwa suti ya michezo, jozi ya viatu na cheti cha shukrani.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Mkuu wa zamani marehemu mzee Rashidi Kawawa ambaye naye alikumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa michezo nchini waliieleza TFF kwamba kwa hili hawakukosea waliposema mkono mtupu haulambwi.
Nilipomsalimu mzee Kawawa na kumkumbusha baadhi ya mambo kwa sekunde chache nilipokuwa naye aliniambia, “Waambie… mcheza kwao hutunzwa. Na sio kwa maneno tu”.
Hapo tena TFF iliagizwa kuwapatia wazee wale bahasha ya angalau wale waliokuja Dar es Salaam kutoka mikoani na kandambili zilizochoka waweze kununua kandambili mpya na kupunguza msururu wa shida wanazopambana nazo.
Lakini kinachoonekana ni kwa TFF kutojali na kutoheshimu maagizo ya Waziri Mkuu na marehemu mzee Kawawa. Sasa imeshapita miezi sita, TFF inaonekana wazi kuwa haijali hata ahadi ile waliyoitoa viongozi wake kwa wachezaji baada ya kupewa maelekezo na waziri mkuu ambaye alisema ofisi yake ilikuwa tayari kusaidia kama TFF itakwama.
Kwa kweli uongozi wa hivi sasa wa TFF unao uwezo mkubwa wa kifedha ukilinganisha na uongozi wa zamani ukianzia na ule wa Katibu mkuu, marehemu Kitwana Ibrahim, baada ya uhuru.
Kinachosikitisha ni kwamba kilichofanywa na TFF kwa kuwakusanya wachezaji, waamuzi na walimu wa soka wa zamani Dar es Salaam kwa sherehe maalum, ilikuwa kama kuwadanganya wale wazee, wachezaji wa kandanda wa siku hizi na mashabiki kuona inajali kumbe ni kinyume chake.
Kitendo cha TFF kuwapa ahadi hawa wazee na kuitupa mbali na hata baadhi ya viongozi wake kukasirika wanapokumbushwa sio mchezo mzuri wa kimaisha.
Katika mchezo wa kandanda mchezaji akicheza vibaya, yaani kinyume na sheria za kandanda, hupuliziwa filimbi na kupokewa adhabu au hata kadi nyekundu ya kutakiwa atoke nje ya uwanja. Sasa kwa mwnenedo wa TFF kuwadharau wazee waliolitumikia taifa hili katika medani ya soka miaka iliopita nami nimeamua kupuliza tarumbeta na kumwambia Rais wa TFF, Leodegar Tenga na wenzake, kwamba wamecheza rafu na wanastahiki kupewa adhabu.
Kama TFF ilikuwa haitaki kuwapa chochote wazee wale basi isingewaahidi. Kitendo cha kumtoa mzee wa miaka 80 kutoka Bukoba au Lindi akiwa hana hata Sh. 10,000 mfukoni na nguo yake inahitaji sabuni ili ifuliwe na kumpa cheti kama njia ya kumthamini ni sawa sawa na kuchezea maisha ya watu.
Huwezi kumwambia mtu mwenye njaa ashibe kwa kunusa harufu ya pilau au mtori. Mwenye njaa hahitaji harufu ya chakula… anachotaka ni chakula ambacho kama hakitampa shibe kitampunguzia njaa aliyokuwa nayo.
Ni vizuri kwa viongozi wa TFF wakajifunza kuwa wakweli na kuelewa kwamba kutumiza ahadi ni wajibu na ndio uungwana. Ni kwa kuwathamini wachezaji wa zamani tu ndio vijana wa leo watapata moyo wa kupernda kuchezea Taifa Stars na kujitolea kwa moyo wao wote kuituimikia.
Ni kwa viongozi wa hivi sasa wa TFF kwanza kuonyesha njia iliyo sahih ya kupita na ndio baadaye tutegemee wachezaji wetu vijana kupita njia huo kwa kuamini ni nzuri na salama. Tuthamini wachezaji wetu wa zamani kwa vitendo na sio maneno matupu na ujanja ujanja.
Njia moja ya kuonyesha kuwathamini na kuwaheshumu walioichezea timu ya soka ya taifa miaka iliopita ni kwa kuukubali ukweli kuwa mkono mtupu haulambwi. Kama huo mkono hauna kitu basi TFF isiuonyooshe kwa mwenye njaa.

0
No votes yet