Hivi ndivyo walivyo viongozi wetu


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

KITU pekee ambacho viongozi wetu wanajivunia na kujidai kuwa wameifanyia nchi yetu ni kudumisha amani. Wanatamba kuwa nchi yetu ni kisiwa cha amani.

Eti wao ndio walioilinda na kudumisha amani katika nchi hii.

Kinachoshangaza ni kwamba wao wakitembea katika nchi hii iliyojaa amani na utulivu wanajilinda kwa silaha za kivita. Bastola moja haitoshi. Katika hali kama hii kuna amani gani na utulivu upi?

Polisi mmoja alitinga katika ukumbi wa disko akiwa na bunduki ya kivita SMG. Habari zilipoenea alifutwa kazi. Lakini kiongozi aliyetinga hotelini na bunduki ya kivita SMG, bastola mbili, licha ya habari zake kuenea kila sehemu ya nchi hii, hajachukuliwa hatua yoyote.

Hivi ndivyo walivyo viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuficha na kulinda uhalifu wao.

Wananchi wanaambiwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, lakini wataamini vipi ikiwa hapa panaonyesha ubaguzi? Sheria lazima ikate kama msumeno. Kama ilikata kwa polisi aliyetinga disko na bunduki ya kivita basi vivyohivyo makali ya upande wa pili yamkate Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima aliyetinga hotelini na bunduki ya kivita. Kinyume cha hapo itakuwa haina maana yoyote kudai kuwa nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria.

Polisi alikuwa na kosa moja tu la kuingia ukumbini na SMG lakini alikuwa nayo kihalali. Naibu Waziri alikuwa na makosa yote. Aliingia hotelini na SMG. Alijimilikisha silaha ya kivita kinyume cha sheria na aliiacha silaha ya kivita mahali pa wazi ambapo ingeweza kuchukuliwa na mhalifu yeyote na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi wasio na hatia.

Tunauliza, aliyekuwa anakaimu ukamanda wa mkoa wa Morogoro Hamisi Seleman alipomkuta Adam Malima na SMG kinyume cha sheria, kwanini hakumkamata? Akiwa ndiye mkuu wa upelelezi mkoa wa Morogoro hajui kuwa raia harusiwi kuwa na silaha ya kivita? Hakujua kuwa kuziweka silaha zile mahali pa wazi ni kosa pia?

Anapoibuka Adolphina Chialo kamanda wa mkoa wa Morogoro na kusema Naibu Waziri hakuwa na SMG anadhani anamdanganya nani? Polisi wachache waovu wanalichafua jeshi zima la polisi. Lakini hawa ndio viongozi wetu!

Polisi alifutwa kazi bila kuchelewa na silaha yake ikarudishwa katika chumba cha kuhifadhia silaha. Kwa Naibu Waziri mpaka sasa hakijaeleweka kitu.

Kumiliki silaha nzito kama hiyo tena kinyume cha sheria hakiwezi kutafsiriwa vinginevyo bali ni ama ujambazi wa kufanya wewe mwenyewe au kukodishia watu wakafanye. Wote huo ni uhalifu mkubwa.

Kiongozi kushiriki katika uhalifu wa kiwango cha juu kama huo ni hatari kubwa kwa Taifa. Hii imezua maneno mengi na mijadala miongoni mwa jamii. Wananchi wanataka wafafanuliwe maana yake mambo haya.

Charles kutoka Kahama katika ujumbe wake aliandika, “Iliwahi kuripotiwa na gazeti moja kuwa Naibu Waziri Adam Malima alikwenda nchini Afrika kusini kinyemela akitumia jina bandia, hudhani kwamba hata Morogoro alikuwapo kinyemela bila serikali anayoitumikia kujua?”

Mwingine akaandika, “Umeyasikia ya Naibu Waziri wetu Malima? Anasafiri na bunduki na bastola kama anaenda Somalia. Au alisikia Morogoro kuna vita? USD 4,000, shilingi milioni moja na nusu, ilhali analipiwa kila kitu! Laptop tatu, Masanduku matatu eti ya nguo, alikuwa anatarajia kukaa Morogoro kwa miezi mingapi?”

Naibu Waziri kisiasa ni kiongozi wa juu ngazi ya nne ukimwacha Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu. Kwa nchi zilizo na utawala wa sheria, na hata zilizo na utawala usiozingatia sheria hii ni kashfa nzito. Palipo na uongozi unaozingatia sheria huyu angekwishajiondoa mwenyewe katika uongozi au angekuwa amekwisha ondolewa na kiongozi wake.

Huyu ni mteule wa Rais. Kwasababu zimeanza kusikika habari za kuipora nchi madini na yeye ni Naibu waziri wa madini hayo, ni vema aliyemteua akawafafanulia wananchi ni nini kilichomsibu mteule wake. Tusiwape wananchi hofu kuwa huja wanaongozwa na viongozi wanaoipora nchi yao.

Serikali ya awamu ya nne imekuja na utamaduni wa viongozi kung’ang’ania kubaki katika uongozi hata pale wanapokuwa wamepoteza sifa. Huko ni kuonyesha kama vile wapo madarakani kwa maslahi binafsi. Serikali imepoteza mvuto. Uhalali wa serikali yoyote ni katika kulinda maslahi ya watu wake, maslahi ya Taifa. Ikishapoteza sifa hiyo inapoteza palepale na sifa ya uhalali wakuwepo madarakani.

Tunayo mifano mingi ya viongozi waliopoteza sifa na sasa wameng’ang’ania kubaki madarakani. Viongozi kama hao wamepoteza heshima yao yote mbele ya jamii!

Madaktari walipoamua kurejea kazini kwa sababu tu ya kumwamini Rais na kwamba wamempa muda ayatatue matatizo yao, ina maana hiyo siyo tiba hata kidogo ya mgomo wa madaktari.

Jiulize, daktari gani amerudi kazini kwa moyo mweupe? Ni lipi alilolitekeleza Rais kati ya madai yao yote? Sasa wanatoa tiba wakiwa na vinyongo ndani ya mioyo yao. Wanatibu kwa matumaini! Furaha ya kazi yao iko wapi? Tija itapatikana vipi.

Anayedhani kuwa huo ndiyo mwisho wa mgomo wa madaktari atakuwa anaona kwa makengeza. Mioyo yao imepondeka nayo imejaa huzuni hasa ikizingatiwa kwamba sasa wanalazimika kufanya kazi chini ya uongozi wa mawaziri wasiowataka na wanaojihami kwa silaha nzito kwa vile hakuna amani. Hivi hili nalo lilihitaji kuaminiwa kweli! Ni la kusema nipeni muda hili! Lakini hawa ndiyo viongozi wetu!

Katika hali hii  wengi watalazimika kumwamini Sheikh mkuu wa mkoa wa Dodoma, Alhaji Rajab Mustafa wa Masjid Alifarouk Islamic aliyekaimu Msikiti mkuu wa Gadaffi Dodoma, alipozungumzia madhara ya kuwa na viongozi wasiomwogopa Mungu.

Alisema; “Uhai wa Watanzania unapotezwa na viongozi waliomsahau Mungu na wasiokuwa na chembe ya utu wa ubinadamu ndani yao.

“Mgomo wa madaktari nchi nzima serikali imeonyesha dharau, kebehi na unafiki mkubwa kwa kuwapuuza wanataaluma hao nyeti. Watanzania tuna kiu ya kumpata kiongozi makini na shupavu jasiri kama Edward Moringe Sokoine kwa sasa, ” alifafanua alipotoa mawaidha katika swala ya Ijumaa wiki iliyopita.

Bado tunao viongozi wa dini walio makini na wenye kumwelekea Mwenyezi Mungu katika mawaidha yao.

Haujapita muda mrefu toka Taifa lishuhudie mnyukano mkali kati ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda, Waziri mkuu Mizengo Pinda na Ofisi ya Rais kuhusu nyongeza ya posho za wabunge. Wakati Ofisi ya Rais inasema Rais hakusaini kuidhinisha nyongeza ya posho za wabunge, Spika na waziri mkuu walisema amesaini. Spika alienda mbali zaidi kwa kusema, “Siyo kwamba zitaanza kutolewa, tuliishaanza kulipa.”

Ilipodhihirika kuwa Rais hakuwa amesaini nyongeza hiyo jambo hilo likaachwa life kimyakimya. Kumsingizia Rais wa nchi hadharani ni utovu wa nidhamu. Hata hivyo hakuna aliyewajibika, wala aliyewajibishwa. Pia hakuna aliyewajibisha. Hawa ndio viongozi wetu!

0713334239
0
No votes yet