Hivi tunajifunzaje kujihami?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 07 April 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TANZANIA haijasalimika na mtikisiko wa sekta ya fedha unaodhoofisha mtandao wa uzalishaji Marekani, Ulaya na Asia.

Japo wataalamu wa kiserikali petu wanatumia lugha tamtam na ngumu kuonyesha nchi haijaathirika kutokana na tatizo hilo, hali halisi inaonyesha vinginevyo.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari, anasema nchi ina akiba ya fedha inayotosha kununua bidhaa nje kwa miezi mitano ijayo kuanzia mwezi huu.

Lakini taarifa ya Benki Kuu (BoT) iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumatatu, inaonyesha matatizo. Kwanza wataalamu wake wanasema thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka. Pili, mapato yamepungua kulinganisha na kipindi cha Julai-Desemba 2008.

Ila Benki inakiri kiwango cha nakisi katika urari wa biashara na huduma kati yetu na nje kimeongezeka, mizani ikitulalia. Ina maana tumenunua zaidi bidhaa nje kuliko tulivyouza.

Wanasema nakisi iliyopo ni Dola 20 milioni katika mwaka unaoishia Februari 2009. Katika kipindi kama hicho 2008, palikuwa na ongezeko la ziada la Dola 30.4 milioni kwa kulinganisha na kipindi cha 2007.

Hapa panahitaji utambuzi: bidhaa za Tanzania hazikununuliwa kwa wingi kikawaida, badala yake tulinunua kwa wingi za nje. Na moja ya sababu kubwa hapa, ni kushuka kwa bei ya mazao ya kilimo na maliasili katika masoko ya nje.

Tatizo hili ni matokeo ya athari za mtikisiko wa kifedha uliokumba nchi zilizoendelea kiviwanda. Wanunuzi wamepungua kununua kwa sababu hawana uwezo waliokuwa nao awali katika kuzalisha viwandani. Hawana fedha ya kutosheleza kama ilivyokuwa.

Mkanganyiko uliopo ni pale wataalamu wa serikali wanapokataa kueleza hatua gani zinachukuliwa ili kuzuia taifa na janga kubwa la kuguswa na mtikisiko wa kifedha duniani.

Hatujasikia hatua hizi kwa wataalamu wa BoT wala Wizara ya Fedha na Uchumi. Tutaamini hata Rais hajafahamishwa; vinginevyo angeshaanza kuzieleza. Hakuzieleza alipohutubia taifa wiki iliyopita.

Wataalam wanasubiri nini wakati huu ndio muda kwao kuchemsha bongo ili kuhami uchumi. Hapa ndipo utaalamu wao unapohitajika. Wakatae kuja kulaumiwa kwa kutoshauri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: