Hivi tutalindana mpaka lini?


Rehema Kimvuli's picture

Na Rehema Kimvuli - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version

UKISIKILIZA kipindi cha bunge, wakati mwingine unatamani kufunga redio au televisheni. Utakuta mbunge huyu anamtetea yule na yule anamtetea mwingine. Muda mwingi unapotea kwa kazi moja tu: Kuteteana!

Kumekuwa na tabia ya muda mrefu sasa kwa viongozi wa serikali kupenda kulindana na kukingiana vifua katika kila kashfa zinazotokea.

Tabia hii kwa kuwa imezoeleka sasa, imekuwa ni sehemu ya serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimekuwa kikishika madaraka tangu nchi ilipopata uhuru wake mwaka 1961.

Viongozi wamekuwa hawana aibu wala woga katika kulindana kwao kiasi kwamba hawajali hata thamani ya kura zilizopigwa hata wao kuteuliwa kuwa mawaziri au wabunge.

Mara nyingi viongozi wa kisiasa hujikuta wakitoa kauli za kutetea waovu licha ya athari zake kuwa ni kuumia kwa wananchi.

Mfano mzuri ni maelezo waliyotoa wabunge Anna Abdallah, Samuel Chitalilo na Chrisant Mzindakaya hivi karibuni bungeni wakati wa mijadala ya bajeti ya serikali.

Wabunge hao walisikika wakitaka wananchi wasiamini katika tuhuma zinazotajwa dhidi ya viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Anna yeye alitoa kauli zilizoashiria kutofautiana na maelezo ya mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela aliyesema watuhumiwa wa ufisadi wa fedha za EPA washitakiwe na fedha lazima zirudishwe zote huku akitaka bunge lipewe taarifa hasa inayosema fedha zimerudishwa.

EPA ni moja ya kashfa kadhaa nzito zinazoikabili serikali kwa sasa na kulingana na taarifa mbalimbali, inasemekena wahusika wake ni pamoja na viongozi waandamizi serikalini.

Inashangaza kuona viongozi wanalindana hata kwa masuala yaliyo wazi ambayo yamekuwa yakitajwa kwa muda mrefu sasa na bado serikali haijayatolea taarifa makini au kuchukua hatua za kuyachunguza ili kupata ukweli wake.

Hata kauli aliyoitoa bungeni Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), kwamba yapo mambo waliyoyagundua katika uchunguzi wa mkataba wa Richmond lakini hawakuyaeleza katika ripoti yao kwa sababu ya kunusuru kuporomoka kwa hadhi ya serikali, inashangaza.

Hivi inakuaje wabunge waliotumwa na Bunge kuchunguza jambo zito kwa nchi watoe ripoti yenye majibu nusunusu huku wakisema wanainusuru serikali. Si ni serikali yenyewe iliyovunja taratibu hadi kusababisha kashfa hiyo?

Serikali ni taasisi inayofanya kazi kwa niaba ya wananchi kama ambavyo bunge linaundwa kikatiba kutumikia wananchi ambao walipiga kura na kuchagua wawakilishi wao ili kuisimamia serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.

Katika mazingira gani sasa hata kamati ya bunge itoe ripoti inayolinda waovu ambao wenyewe licha ya kupewa dhamana ya kuongoza vizuri, hawakuheshimu dhamana hizo?

Kitendo cha kutoa ripoti iliyoficha baadhi ya taarifa kinamaanisha kuwa Kamati ya Dk. Mwakyembe haikufanya kazi yake kikamilifu.

Na inakera kuona dosari hiyo imefanywa kwa makusudi ili kuendeleza utamaduni mbaya wa kulindana miongoni mwa viongozi wa serikali.

Leo Dk. Mwakyembe, baada ya kuona sakata la Richmond limeibuka upya bungeni, analalamika na kushauri kwa Spika kuvunjwa kanuni ili suala hilo lijadiliwe tena na kwamba amejipanga na wajumbe wenzake kuyaeleza waliyoyaficha.

Je akiyaeleza leo si yataharibu heshima ya serikali ileile waliyokuwa wameinusuru isiingie doa walipoamua kuficha baadhi ya mambo?

Hayo ndiyo matokeo ya utawala kujenga mfumo unaoruhusu kuficha mambo muhimu ya nchi japo kuyaeleza huwa kuna maslahi makubwa kwa umma.

Suala lililochunguzwa lilihusu matumizi mabaya ya madaraka na raslimali za taifa na wala hapakuwa na sababu ya msingi ya kulinda waliohusika kuhujumu.

Wanasahau kuwa Tanzania ni nchi maskini ambayo ina kundi kubwa la watu wanaoishi chini ya kipato cha dola moja kwa siku.

Ni vipi wananchi hao wanasaidiwa iwapo mfumo wa kulinda wahujumu uchumi wa nchi utaendelea? Kila siku viongozi utasikia wakisema hili na lile halikufanyika kwa sababu ya uhaba wa fedha. Fedha zipi wakati mipango ya ufisadi inazidi?

Watanzania wanazidi kufa kwa magonjwa yanayotibika, maelfu ya watoto wanakosa elimu na lishe bora huku viongozi wakiendekeza ufisadi.

Wakati umefika kwa viongozi kuamka na kusimama mbele kukomesha ufisadi. Kila anayevunja taratibu za utumishi, adhibitiwe na wahujumu washitakiwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: