Hofu ya mabomu yatanda Dar


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version

JESHI la Wananchi (JW) limekataa kuthibitisha kauli za wananchi kuwa bado kuna mabomu makubwa na hatari zaidi ambayo yatalipuka kwenye kambi ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam.

Akihojiwa jijini Dar es Salaam juzi Jumatatu, Mnadhimu wa JW, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo amekataa kusema lolote juu ya kuwepo mabomu hatari na milipuko mipya.

Shimbo alimwambia mwandishi wa habari hizi, “Zingatieni tangazo lililotolewa na mheshimiwa rais (Jakaya Kikwete) ambaye alitembelea eneo la tukio; mengine yatakuwa majungu.”

Alikuwa ameombwa kujibu hoja za wananchi kwamba wameambiwa kwenye maghala ya silaha kambini Gongolamboto, kuna mabomu ambayo yatalipuka si muda mrefu.

Aliulizwa pia iwapo anafahamu kuwa kuna mabomu mengine makubwa, mazito na hatari ambayo yanaweza kuteketeza eneo kubwa.

Kwanza Luteni Jenerali Shimbo alicheka, kwenye simu yake ya mkononi na hatimaye kusema, “Rais alitembelea pale kwenye tukio na kutoa tangazo rasmi. Lizingatieni hilo. Msifuate majungu.”

Shimbo hakuwa na maelezo kuhusu madai kuwa jeshi liliishaomba wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa, fedha za kugharimia uteketezaji baadhi ya mabomu kwenye kambi ya Gongolamboto.

Alisema, “Kwa hayo mimi sitakuwa na la kusema maana katika nafasi yangu kikazi, haiwezekani kutolea hayo majibu.”

Kwa staili yake ya kuongea kwa kujiamini, Shimbo alisema inafaa maswali hayo “…aulizwe waziri au katibu mkuu wa wizara ya ulinzi.”

Jitihada za kuwapata viongozi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hazikuzaa matunda. Simu (0754 995555) ya waziri Dk. Hussein Mwinyi iliita mara nyingi bila kupokewa.

Hata pale waziri alipotafutwa kupitia simu ya mezani (022 2152697), simu hiyo iliita hadi kukatika bila ya kupokewa.

Mwandishi wa MwanaHALISI ambaye, kwa siku nne mfululizo, amekuwa maeneo yanayozunguka Gongolamboto, amekuwa akiongea na wananchi juu ya mkasa wa Jumatano iliyopita ambamo watu wapatao 25 wamefariki kutokana na milipuko ya mabomu.

mwansishi amenukuu wananchi wakisema wameambiwa na askari wa jeshi hilo kwamba “kuna hatari ya mabomu mengine kulipuka hivi karibuni.”

Wananchi wanadai wameelezwa kuwa “uhai” wa mabomu yanayohofiwa kulipuka tayari umepita na yalistahili kuteketezwa.

“Sikiliza nikueleze, si jeshi wala serikali wasiojua kama kuna hatari ya mabomu kulipuka katika kambi hii,” alieleza mwananchi akinukuu mmoja wa maaskari katika eneo la Pugu Kajiungeni.

Askari ambaye hakutaka jina lake litajwe na aliyeongea mbele ya wananchi wapatao 15, alisema jeshi liliishapeleka maombi serikalini mara kadhaa kuomba fedha kwa ajili ya kuharibu mabomu kwa kuwa yameshapitwa na wakati, lakini serikali imekaa kimya.

“Hata baada ya mabomu ya Mbagala kulipuka jeshi liliandika barua nyingine kuomba fedha na idhini ya kuyaharibu haya ya hapa, kama vile ilikuwa inasubiriwa siku tu balaa litokee,” amesema.

Akiwa kama anayetetemeka na akiangalia huku na kule, askari huyo alisema, “Hata hivyo, Mungu amesaidia; moto haukufika kwenye ghala lenye mabomu mazito. Sijui ingekuwaje saa hizi.”

Abubakari Mustafa, kijana aliyesema ana umri wa miaka 34 alizomewa pale alipotaka kuelezea hali katika kambi ya Gongolamboto.

Alikuwa ameanza kusema, “Unajua pale kuna mabomu mazito, yako chini ambayo yanahitaji kupangwa kwa fokolifti. Kama serikali itaamua leo…” ndipo akazomewa na kuambiwa anyamaze kwani yeye siyo mwanajeshi.

Mwandishi, hata hivyo, alielezwa kuwa karibu familia zote za wanajeshi wanaoishi maeneo yanayozunguka kambi (Pugu Kwalala, Majohe na Kajiungeni) walihama nyumba zao mapema siku ya tukio.

Mwananchi mmoja alikubaliana maelezo hayo akisema, “Ni kweli walikuwa wanajua. Familia nzima jirani yetu waliondoka saa 11 jioni siku ya tukio (Jumatano) na hawakurudi mpaka jana Ijumaa.” Huyu ni muuza vinywaji baridi Pugu Kwalala.

Mama mmoja anayeishi Pugu Kajiungeni alisikika akisema kuwa alipigiwa simu na kaka yake ambaye ni mwanajeshi anayefanya kazi kambini Gongolamboto mchana wa siku ya tukio na kumwambia aondoshe familia kwa kuwa “jeshini hali si nzuri.”

“Unajua sikumwelewa. Nilipomuuliza kwanini anasema hivyo, alikata simu na mimi nikadharau,” anasimulia mama huyo.

Taarifa kutoka kwa wakazi wa Majohe, Chanika na Gongolamboto zinaeleza kwamba kulikuwa na sauti za milipuko tangu saa 9 mchana siku ya tukio.

“Mimi na mume wangu tulikuwa Chanika majira ya saa tisa alasiri. Tukasikia mishindo mitatu – wa kwanza tulifikiri mpira wa gari umepasuka lakini tuliposikia wa pili na wa tatu tukajua mabomu yanalipuka,” anasimulia mama wa umri wa kati.

Usiku wa tukio ulikuwa wa matukio yasiyo ya kawaida kwa wengi. Hamsini Khalfani anasimulia:

“Nilikuwa nimeshanawa kuanza kula. Nikalazimika kunyanyuka na kuchungulia nje. Ndipo nilipobaini ni milipuko ya mabomu kutokea upande wa kambi ya jeshi,” anasema.

“Hakuna aliyethubutu kula. Kuanzia hapo ikawa mshikemshike. Watu wanakimbia ovyo makundi kwa makundi. Niliwasikia baadhi ya majirani wanawaambia watoto wao waingie ndani,” anasimulia kwa uchungu.

Usiku wa tukio, eneo lote kuanzia Pugu Kwalala, Pugu Kajiungeni, Pugu Kigogo Fresh mpaka Kisarawe, kulikuwa na gari moja tu lililokuwa linabeba majeruhi kuwapeleka hospitali ya Kisarawe.

Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser (DFP 6315) ni la wizara ya mambo ya ndani lilitolewa msaada na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

Dereva wa gari hili alichukua baadhi ya watoto na kuwakimbiza Kisarawe. Watoto wengi waliumia kwa kukanyagana na wengine wazazi wao walikuwa wanawarushia ndani ya gari kama nazi.

Bahati mbaya hata mpaka sasa 7 mchana wa siku ya pili, hakukuwa na gari la serikali la kusaidia kuhudumia majeruhi kwa kuwapeleka hospitalini. Hakukuwa pia na tangazo la kutuliza watu.

“Kilichotusaidia, mimi na baadhi ya wenzangu, tulikuwa tunakimbia na wanajeshi huku wakituelekeza pa kukimbilia,” anasimulia Yusuf Mohammed, mfanyabiashara wa Pugu Kwalala.

“Wanajeshi tuliokuwa tunakimbia nao walituambia atakayesimama ndiye mwenye hatari zaidi ya kupigwa na bomu kuliko yule aliyechuchumaa na aliyechuchumaa yuko hatarini zaidi kuliko aliyelala,” alieleza Yusuf.

Kama wahenga walivyosema, “penye wengi kuna mengi.” Ingawa lilikuwa tukio la hatari sana lakini kulikuwa na vituko vya kuweza kuchekesha.

Wakati tukikimbia mabomu (Pugu Kajiungeni), nilimkuta mzee amebeba kiroba cha unga wa sembe akikimbia nacho. Nilipomwambia akitupe ili apate nguvu za kukimbia alikataa. Alianguka na kuinuka nacho.

Mtu mmoja eneo la Chanika alijikuta amevaa gagulo bila kujitambua. Haikujulikana alikuwa wapi wakati mabomu yanalipuka lakini, alionekana asubuhi akiwa katika hali hiyo.

Yusuf Mohammed, mfanyabiashara wa Pugu Kwalala anasimulia alivyoshuhudia mama mjamzito akijifungua porini na kukiacha kichanga.

“Inatia uchungu hata kusimulia. Wakati tumejificha porini, mama mmoja mjamzito alijifungua; lakini bomu lilipopiga karibu yetu, sote tukatimua mbio na mama alikiacha kichanga chake,” anasimulia kwa huzuni.

0784 447077 uclejay_jongo@yahoo.com
0
No votes yet