Hoja ya Rostam Bungeni hii


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuzungumza mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kutoa maelezo na vielelezo kuthibitisha hoja nilizotoa katika mchango wangu wa maandishi nilioutoa katika kikao kilichopita cha Bunge wakati wa mjadala wa Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi "Richmond Development Company LLC" ya Houston, Texas Marekani mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, wakati akifungua mjadala wa hoja hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Teule, Mheshimiwa Dr. Harrison Mwakyembe, siyo tu alinitaka nithibitishe hoja yangu kwamba Kamati Teule hiyo ilikuwa inaendelea kumalizia kazi zake hadi wiki ya kwanza ya kikao kilichopita cha Bunge lakini pia aligusia maeneo kadhaa ya ripoti ambayo yananihusu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu nitoe maelezo ya kina pamoja na ushahidi wa vielelezo kuhusiana na masuala hayo yote aliyoyazungumzia Mheshimiwa Mwakyembe ili Bunge hili na Watanzania kwa ujumla waujue ukweli, tena ukweli kamili kuhusiana na suala hili.

Mheshimiwa Spika, nianze na hoja ya hati ya wito wa kunitaka nifike mbele ya Kamati Teule kutoa ushahidi.

Ni lazima nikiri nimesikitishwa sana ingawa sikushangazwa na maelezo marefu ya Mheshimimiwa Mwakyembe aliyoyatoa kueleza jinsi hati ya wito ilivyofikishwa nyumbani kwangu Oysterbay na kupokewa kwa dispatch na mtu aliyedaiwa kuwa ni ndugu yangu.

Sikuona umuhimu wala haja ya maelezo hayo kwa sababu katika mchango wangu wa maandishi nilioutoa katika mjadala ule, hakuna sehemu yoyote niliyosema kuwa hati ya kiapo haikufikishwa nyumbani kwangu tarehe waliyoitaja.

Kwa hivyo, ule utungo mrefu wa kufikia kulieleza Bunge lako kwamba Kamati Teule ina hata hati ya kiapo ya mtumishi wa Bunge aliyefikisha summons (wito) hiyo nyumbani kwangu ilikuwa na muendelezo tu wa kipaji cha usanii cha Mheshimiwa Mwakyembe.

Mheshimiwa Spika, nilichosema mimi, na ambacho Mheshimiwa Mwakyembe amekikariri vizuri katika maelezo yake, ni kuwa hati hiyo iliandikwa tarehe 24 Desemba, 2007 ikinitaka nifike mbele ya Kamati Teule tarehe 27 Desemba, 2007 na kwamba mazingira ya tarehe hizo ni magumu kwa barua kuwafikia walengwa kabla ya sikukuu kupita.

Mheshimiwa Spika, kupokelewa hati ya wito nyumbani kwangu ni suala moja na hati kunifikia mimi ni suala jengine.

Sidhani kama Mheshimiwa Mwakyembe anapofikishiwa barua nyumbani kwake wakati yeye akiwa nje ya nchi, basi wanafamilia yake husafiri kumfuata aliko ili kumfikishia barua hiyo kwa hivyo, wala haikuwa ajabu kama Kamati Teule ilivyotaka ionekane kwa mimi kupokea barua hiyo baada ya kurejea kutoka safari yangu nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika mchango wangu wa maandishi, mimi nilikuwa nje ya nchi kuanzia tarehe 17 Desemba, 2007 hadi 3 Januari, 2008. Nawasilisha kwako nakala ya photocopy ya Paspoti yangu ikiwa na mihuri ya Idara ya Uhamiaji inayoonyesha kutoka na kurejea kwangu hapa nchini kama kielelezo kinachothibitisha maelezo yangu hayo.

Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza kuwa Kamati haikuwa na nia ya kweli na ya dhati ya kutaka maelezo yangu maana kama ingetaka kufanya hivyo, ingeniita katika siku yoyote kabla ya Desemba 24, 2007. Lakini kwa kusubiri siku 7 tu kabla ya kumalizika kwa muda ambao walipaswa wawe wamekamilisha kazi yao, tena ikiwa ni kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo familia nyingi zisizo na kazi za serikali huchukua likizo, kunaonyesha wazi kuwa kulikuwa na malengo ya kutaka kuchafuana tu kwa kujua kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kutopatikana yule anayehitajika kutoa ushahidi. Iwapo Mheshimiwa Mwakyembe hapendi kuona nina siku za mapumziko, ni bahati mbaya sana kuwa mimi sina cha kumsaidia katika hilo.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema kwamba kama Kamati Teule ilikuwa na nia ya dhati ya kutaka maelezo yangu basi wangeweza kufanya hivyo hata baada ya mimi kurejea kwa sababu kama nitakavyothibitisha kwa ushahidi Kamati iliendelea na kazi hadi baada ya Desemba 31, 2007.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuliingilia hilo, napenda pia nieleze ukweli kuhusu hoja nyingine ambazo Mheshimiwa Mwakyembe alijaribu kuzipotosha akitumia usanii wake wa kuwasilisha na kujibu hoja. Nianze na ile inayohusu kuitafutia Richmond kampuni ya ushauri ya uandishi wa habari (G&S Media Consultancy) ili Richmond iandikwe vizuri na vyombo vya habari Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hoja hii inaonekana imeibuliwa kutokana na ushahidi wa Ndugu Salva Rweyemamu alioutoa mbele ya Kamati Teule. Nimepata nafasi ya kupitia Hansard za Bunge zinazohusu shughuli za Kamati Teule na nilichokiona ni kuwa Ndugu Salva Rweyemamu mwenyewe hakuwa na uhakika wa kile alichokisema pale alipoulizwa juu ya nani aliyemtambulisha kwa kampuni ya Richmond na yeye akajibu, "Nadhani ni rafiki yangu Rostam Aziz".

Mheshimiwa Spika, ni juu ya Ndugu Salva mwenyewe kuweka sawa kumbukumbu zake na kujua kwa uhakika ni nani aliyemtambulisha na Richmond badala ya kusema "anadhani". Inawezekana kama binadamu alichanganya mambo kwani mimi sikuwahi kumtambulisha kwa Richmond, maana mimi mwenyewe siwajui hao akina Richmond hata niweze kuwatambulisha kwa mtu mwingine. Mimi nilimtambulisha Ndugu Salva kwa kampuni ya FFT inayoshughulika na utoaji wa mizigo bandarini (clearing and forwarding) ambayo ndiyo ninayoitumia katika shughuli za kibiashara za kampuni zangu ili kuweza kujitangaza yaani kufanya promotion. Kuthibitisha hilo, nawasilisha mbele ya Bunge lako hati ya kiapo, affidavit ya Ndugu Hassan Dhala, mmiliki wa kampuni ya FFT, ambayo imesainiwa na kamishna wa viapo inayobainisha ukweli huu.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo mheshimiwa Mwakyembe katika maelezo yake alisema Kamati Teule ilitaka nieleze ni ile inayohusu uhusiano kati ya kampuni yangu ya Caspian na kampuni ya Dowans. Kamati Teule imehoji kwanini barua pepe na anuani ya posta ya kampuni yangu ya Caspian pia ilitumiwa na Dowans na kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Caspian wanadaiwa, naomba nirejee wanadaiwa, kuifanyia kazi pia Dowans.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuzijibu hoja hizo, napenda nimfahamishe mheshimiwa Mwakyembe kuwa mimi, tofauti na labda alivyo yeye, sina wapambe eti wa kunisimulia yaliyoandikwa katika Ripoti ya Kamati Teule aliyoiongoza. Nataka nimhakikishie kuwa nimesoma ukarusa hadi ukurasa wa ripoti waliyoiandaa pamoja na kwamba haikuwa kazi nyepesi ukitilia maanani kwamba ripoti hiyo imepotosha na kupindisha mno hoja zinazohusu masuala ya fedha, uchumi na biashara.

Mheshimiwa Spika, hakuna hata mfanyakazi mmoja wa Caspian anayeifanyia kazi Dowans. Isipokuwa narejea tena maelezo niliyoyatoa katika mchango wangu kwamba watumishi wa kampuni yangu wanaweza kushirikiana na kampuni yoyoye ambayo kampuni yetu ina nia ya kufanya nayo biashara. Na hilo lilifanyika kama ambavyo pia ni kweli kuwa kampuni ya Caspian ambayo mimi ni Mwenyekiti wake iliruhusu Dowans kutumia anuani ya posta na barua pepe yake kwa sababu tulikuwa tunatarajia kupata kazi ya ukandarasi wa ujenzi kutoka kwao, ambayo ndiyo biashara kuu ya kampuni ya Caspian.

Mheshimiwa Spika, hiki si kioja kama ambavyo Mheshimiwa Mwakyembe na Kamati Teule alitaka ionekane. Ni taratibu za kawaida kabisa katika shughuli za biashara kuwa na kitu kinachoitwa "hospitality arrangement" yaani kupeana fursa za kutumia baadhi ya huduma baina ya kampuni zinazokusudia kufanya biashara au kupeana kazi. Hili linaweza likaonekana ni jambo kubwa la kuzua maswali kwa watu wasio na uelewa wa uendeshaji biashara lakini ni jambo la kawaida kabisa katika ulimwengu wa ushindani wa kibiashara ambapo kila kampuni inatafuta kandarasi kutoka kwa mwenzake.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyoeleza kampuni yangu ya Caspian ni kampuni ya kandarasi ambayo huwa inatafuta kazi kwa kampuni nyingine zenye shughuli hizo. Caspian iliwasilisha zabuni ya kufanya kazi ya kandarasi ya ujenzi kwa ajili ya uwekaji wa mtambo wa General Electric 40MW LM6000 Gas Lurbine kwa Dowans ambayo hatukufanikiwa kuipata. Hata hivyo, tuliomba kazi nyingine ndogo ya kandarasi ya ujenzi wa ukuta wa uzio ambayo tulifanikiwa kuipata.

Nawasilisha mbele ya Bunge lako nakala za barua mbili kutoka Dowans kwenda kwa Caspian kuthibitisha haya, moja ya tarehe 10 Machi, 2007 ikitueleza kutofanikiwa kupata kazi tuliyoomba awali, na ya pili ya tarehe 25 Oktoba, 2007 ikitufahamisha kuwa zabuni yetu imefaulu.

Mheshimiwa Spika, aina ya kazi za ujenzi ambazo kutoka kwa Dowans tuna ujuzi nazo na tumejijengea jina zuri kwa jinsi tunavyozifanya. Tumewahi kufanya kazi kama hizo kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kampuni ya WARTSILA ya Finland baada ya kushinda zabuni ya kimataifa. Nawasilisha kwako Mheshimiwa Spika, nakala za barua mbili (ya kwanza ya tarehe 31 Machi, 2008) kutoka kwa WARTSILA kwenda kwa Caspian kuthibitisha ukweli huu.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa ya Bunge lako tukufu, WARTSILA ni kampuni iliyosifiwa na Kamati Teule kwamba mradi wake ni wa kuigwa katika uzalishaji wa umeme hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo mahusiano ya kikazi kati ya Dowans na Caspian ambayo ni ya kawaida kabisa, yaliyofuata taratibu zote na yaliyofanyika kwa uwazi. Ni mahusiano ambayo kama Kamati Teule ingetaka kuyajua ingeweza kufanya hivyo. Hata hivyo, Kamati Teule iliamua kukwepa wajibu wa kuujua ukweli huu na badala yake ikaamua kuibua maswali yaliyoandaliwa kwa usanii mkubwa ili yatimize lengo lililokusudiwa la kutuchafulia majina baadhi yetu na pengine hata kuhujumu sifa njema za biashara tunazofanya.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuweka kumbukumbu sawa kuhusiana na hoja hizo zilizoibuliwa na Mheshimiwa Mwakyembe, sasa nijielekeze katika hoja ya msingi ambayo ndiyo hasa niliyotakiwa niithibitishe. Hii ni ile inayohusu hoja yangu kwamba Kamati Teule iliyochunguza mkataba wa Richmond iliendelea na kazi zake hata baada ya muda wa siku 45, yaani baada ya tarehe 31 Desemba, 2007, na mpaka wiki moja kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge na hivyo kama ilikuwa na nia thabiti ya kuupata ukweli kutoka kwangu ingeweza kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimesikitishwa ingawa sikushangazwa na kitendo cha Mhe. Mwakyembe kujikakamua katika ukumbi mtukufu wa Bunge lako kwamba eti madai hayo ni uongo.

Mheshimiwa Spika, nina ushahidi wa hoja hiyo kwamba kamati iliendelea na kazi zake hadi baada ya muda iliyopangiwa kumalizika. Ushahidi huo nauwakilisha hapa mbele ya Bunge lako ili lione ni nani kati yangu na Mhe. Mwakyembe anayesema kweli.

Mheshimiwa Spika, sisi wengine hatuna kawaida ya kuja na mbwembwe nyingi za kujisifu hata kama ni kwa gharama ya kulipotosha Taifa na kuwapotosha wananchi. Tuna asili na rekodi ya kusema kweli, tena kweli tupu. Tunaamini katika kutenda na kutendewa uadilifu. Kwa hivyo, kila tunachokisema na kukitenda kina misingi yake. Leo hii, nimeona niwasaidie watanzania kupitia Bunge lako tukufu kuujua ukweli kamili ambao umejaribiwa kufichwa sana kwa malengo wanayoyajua wajumbe wa Kamati Teule.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: