Hoja za Msekwa kuhusu katiba ni dhaifu


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

Ni vizuri tujitahidi kutenganisha watekelezaji na Katiba. Katiba inaweka tu vyombo vinavyoingiza watekelezaji hao…Hilo la kutenganisha kati ya watendaji waliowekwa na katiba hiyo na katiba yenyewe - Pius Msekwa.

NAAM! Hizi ni zama mpya. Ni zama ambazo hata wakongwe wa siasa wanaanza kuchanganya maneno na hata fikra zao zinaonekana zimechanganyikiwa; kiasi cha kutufanya wengine tuanze kujiuliza hawa watu wameweza vipi kuongoza taifa hadi hivi leo?

Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amefanya makosa makubwa ambayo ni muhimu yasahihishwe. Yakibaki kama yalivyo, yatarudisha taifa kwenye matatizo yale yale ambayo tunataka kuondokana nayo.

Kwa waliofuatilia mjadala wa Katiba Mpya uliorushwa na kituo cha televisheni (ITV) mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo Msekwa alikuwa ndiye mzungumzaji mkuu, watakubaliana nami kuwa Msekwa Msekwa ameeneza fikra potofu juu ya katiba na utawala.

Mwanzoni nilifikiria amezungumza vibaya, lakini mara kwa mara alikuwa anarudia kauli moja ambayo kama ndio msimamo wake tangu miaka ya sitini, basi naweza kusema kuwa sasa naelewa kwanini taifa hili lina matatizo mengi ya Kikatiba!

Maana kama yeye ni miongoni mwa watu walioshiriki katika kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na Katiba ya Tanganyika na baadaye ya Muungano, basi ndugu zangu, kweli CCM iko matatani.

Mara kadhaa Msekwa aliasa wananchi kuwa “katiba inaweka vyombo tu, lakini watendaji wakitenda kinyume na katiba hiyo siyo kosa la katiba. Ni kosa la watendaji.”

Alirudia kauli hiyo mara kwa mara kiasi cha kufanya umma uamini kuwa Msekwa amefungwa katika fikra za miaka ya sitini ambapo aliiona katiba kama mashine tu.

Kosa la kwanza alilolifanya Msekwa, ni kutoelewa uhusiano wa katiba na watawala. Kwamba katiba ni uanisho wa mpango na mfumo wa mahusiano kati ya watawala na watawaliwa.

Wengi wanasema ni “mkataba wa kijamii.” Ni roho inayoshikilia jamii hiyo (nchi) pamoja kwa kuweka bayana yale ambayo watawala wanaweza kufanya na yale ambayo hawawezi.

Katiba haiweki tu vyombo, halafu ikakalia kimya kazi ya vyombo hivyo.

Haiwezi kuwa kama fundi ambaye analeta kitu ambacho anasema “mashine ya kusaga.” Ikaonekana hivyo hata katika maandishi yake. Lakini ukweli wa mashine hauji katika kusoma kile ambacho mashine inaweza kufanya. Njia pekee ya kujua kama kweli hii ni mashine ya kusaga, ni kuweka nafaka na kuiwasha kuthibitisha kuwa inaweza kufanya kazi hiyo.

Katiba ni zaidi ya mashine, ni mfumo mzima wa mahusiano kati ya wananchi na viongozi, kati ya viongozi na viongozi,  kati ya wananchi na wananchi na kati ya vyombo mbalimbali vya nchi na serikali.

Hivyo basi, kimsingi katiba inatakiwa iainishe bayana mamlaka ya kila mmoja na iseme kisipofanywa au kikifanywa hiki  kinatokea nini? Haiwezekani katiba ikaweka vyombo tu, kisha ikae kimya kuhusu yule aliyeteuliwa anapovurunda!

Ndio maana katiba imeweka hata utaratibu wa kumuondoa madarakani rais, waziri mkuu na wengineo. Kwa hiyo, hatuwezi kutenganisha katiba na watendaji wanaotokana na katiba hiyo.

Kosa la pili kubwa ambalo Msekwa alilifanya, ni kushindwa kuelezea uhusiano wa katiba na sheria za nchi. Mara kwa mara tunawasikia watu wanasema, “Katiba ndio sheria mama,” wakimaanisha kwamba sheria nyingine zote zinatokana na katiba.

Sasa sheria za nchi zinazotungwa na Bunge ni lazima ziendane na katiba. Sheria yoyote inayopingana na katiba, ni batili. 

Kwa maneno mengine, katiba ni lazima iwe juu ya nini kinaweza kufanywa au sheria gani inaweza kutungwa, kwani ikikaa kimya watu wanaweza kujiandikia sheria zenye madudu kama tulizo nazo leo.

Nitatoa mfano kwa kutumia katiba ya Marekani. Mabadiliko ya kwanza ya katiba ya Marekani yalikataza Bunge la nchi hiyo kutunga sheria yoyote itakayerasimisha dini fulani kukataza watu wasifuate dini nyingine. 

Kutokana na kipengele hicho, Wamarekani hawana dini rasmi na hawawezi kuja na sheria inayoonesha kwa namna yoyote upendeleo wa dini fulani. Kwa hiyo, kile ambacho katiba inakataza hakifanywi.

Kumbe basi sheria zinazosimamia watendaji mbalimbali zitafanya kile ambacho katiba inataka au haitaki.

Kwa mfano, katiba inasema kutakuwa na tume ya uchaguzi itakayoongozwa na mtu mwenye sifa ya ujaji atakayeteuliwa na rais. Lakini katiba ikisema kutakuwa na tume ya uchaguzi ambaye mkuu wake atakuwa ni jaji atakayeteuliwa na rais na kuidhinishwa na Bunge, ndivyo itakavyokuwa.

Kosa la tatu la Msekwa kwenye hoja yake linatokana na kile alichokisema kuwa sababu ambazo zinaweza kusababisha watu kutaka kuwa na katiba mpya. Alitoa sababu mbili ya kwanza alisema pale ambapo utawala unabadilishwa na pili tawala zinapounganishwa.

Wafalme wanaitwa “sovereign” kwa maana ya kwamba asili a madaraka yote katika nchi yanatoka kwa mfalme; na jamii zinazoamini utawala wa Mungu wanaamini kuwa Mungu ndiye Asili Kamili ya Madaraka (Absolute Sovereign). 

Sababu mbili za kubadilisha katiba zinazungumzia - asili ya madaraka zinapobadilishwa (kutoka kwa mfalme kwenda kwa jamhuri) au pale nchi mbili zenye madaraka kamili ya kujitawala zinapoungana.

Lakini kuna sababu ya tatu ambayo inayoweza sababisha kuandikwa kwa katiba mpya na ambayo ninaamini inatosha wananchi kuisimamia.

Katiba ya sasa inasema wazi katika ibara ya 18.1 (a) kuwa “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.”

Katiba inatambuwa kuwa wananchi ndio msingi mzima wa madaraka yote; kwa maneno mengine asili ya madaraka katika taifa letu, iko mikononi mwa wananchi. 

Hii ina maana gani? Kwamba wananchi wakiamua kubadilisha katiba yao hawahitaji kibali cha rais au serikali. Wao ndiyo asili ya madaraka na hivyo lolote wanaloamua hakuna wa kubadilisha.

Hii ndiyo sababu ya wananchi kukataa kukiachia chama kimoja kuamua hatima ya taifa. Lakini kuna hili pia. Msekwa ameshindwa kuonesha uzito wa haja ya kuwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mimi na wengine ambao tunaamini kuwa katiba inahitajika kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ujao, tunajua kuwa taifa haliwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa salama kwa kutumia katiba ya sasa.

Kama kwa miaka hamsini iliyopita tumekuwa na katiba ya sasa na ikiwa na mabadiliko mengi na malalamiko lukuki kwanini tuanze nusu karne ijayo na katiba hii hii?

Kama Rais Jakaya Kikwete anadhani kuna zawadi anaweza kuliachia taifa hili, basi zawadi iliyobora ni katiba nzuri na yenye kuona mbali.

Hivyo, basi leo hii hatuna tena mjadala wa Katiba Mpya. Hilo tumeshalimaliza. Mjadala uliyopo ni jinsi gani tuandike katiba hiyo, tuweke muda gani wa kukamilisha na kwa hatua gani na vipi.

Jambo kubwa la msingi kuanzia sasa, ni kuweka mfumo utakaohakikisha tunakuwa na katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu ujao, nikiamini kuwa kura ya maoni ya Katiba Mpya ipigwe kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014.

Hiyo itasaidia kuona Katiba Mpya ikianza kufanya kazi mapema wakati huo. Katika hili, sikubaliani na wanaosema ati tusiharakishe kuwa na katiba Mpya. Hatufanyi haraka, lakini hatutakiwi kuchelewa.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: