Hoja za NECTA hazina mashiko


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako ametangaza kufutwa kwa matokeo ya wanafunzi 3,303 wa kidatu cha nne waliofanya mitihani yao ya taifa mwaka jana.

Dk. Ndalichako alisema wiki iliyopita kwamba kufutwa kwa matokeo hayo kulitokana na baadhi ya wanafunzi kukamatwa na simu, notisi, kujisajili mara mbili na kufanya mitihani kwa kutumia karatasi za majibu zenye miandiko tofauti katika somo moja.

Miongoni mwa shule ambazo zimeathirika na hatua hiyo, ni shule ya shule ya Sekondari ya Mikunguni (S0384), Hamamni (S0390), Jang’ombe, High View na Lauréate zilizopo visiwani Zanzibar.

Licha ya kushindwa kuingia katika ushindani wa nafasi 10 bora, shule hizo ambazo zilikuwa zikitamba huko nyuma, zimeishia kupata herufi (w) ikiwa na maana withdrawn yaani kufuta aukutengu matokeo kutokana na kufanya udanganyifu.

Haya ni matokeo ya kwanza mabaya zaidi katika kipindi cha miaka 35 tangu Mapinduzi ya 12 Januari 1964.

Alama hii hutumiwa sana kwenye vyuo vya elimu ya juu. Hapa aliyefichiwa matokeo huandikiwa kwa vile huwa hajakamilisha ada ya masomo au kazi za darasani.

Kwa shule za sekondari kama ilivyotokea Zanzibar itakuwa si sahihi kwani shule za serekali fedha hulipwa na serekali. NECTA hawajasema popote kama wamezuia matokeo ya shule hizo mapaka uchunguzi ukamilike.

Hata hivyo, ukiangalia kwa makini hicho kinachodaiwa kutendeka, haraka unaweza kubaini NECTA imeshindwa kueleza ukweli wa kilichofanyika.

Kwa mfano, shule ya sekondari ya Mikunguni ambayo ilikuwa bora huko nyuma, mwaka huu imeongoza kwa aibu. Kati ya wanafunzi wake 42 waliofanya mtihani wa kidato cha nne, ni wanafunzi watano tu walionekana kutokuwa na mashaka.

Mikunguni imepakana na shule mbili za Lumumba na Nyerere.

Lakini hizi “hazikutumbukia kwenye mikono ya NECTA.” Katika mazingira yoyote yale, mtihani hauwezi kuvuja Mikunguni, ukashindwa kuvuja Lumumba na Nyerere.

Aidha, kwenye shule ya Sekondari ya Jang’ombe kati ya wanafunzi 176 waliofanya mitihani, ni wanafunzi 53 tu waliosalimika. Waliobaki wote wamepigwa alama w.

Mwalimu mmoja wa shule hii amemweleza mwandishi wa makala haya, kwa sharti la kutotajwa jina kwamba hadi Jumatatu, NECTA ilikuwa haijawapa taarifa kuwa matokeo ya wanafunzi hao yamezuiwa.

Kama ilivyo kwa Mikunguni, Jang’ombe imepakana na Kidongochekundu ambayo haikukumbwa na dhahama hii; Laureate iliyopo Chukwani imepakana na High View.

Lakini Laureate, kati ya wanafunzi 48 waliofanya mitihani, ni wanafunzi wawili tu ambao NECTA imesema matokeo yao hayana mashaka.

Hawa waliosalimika wameangukia alama D na F. High View ambayo ilikuwa miongoni mwa shule bora nchini huko nyuma, kati ya wanafunzi 78 waliofanya mitihani, ni wanafunzi tisa tu waliosalimika na rungu la NECTA. Wengine wote waliosalia wamepewa alama w.

Shule hii imepakana na Kiembesamaki ambayo haina alama w, ingawa imeongoza kwa alama D na F.

Hata Kiembesamaki majengo yake yamepakana na shule ya Sekondari ya Kiislam ya Mazizini. Kati ya wanafunzi 51 wa shule hii ya kiislamu, ni mmoja tu aliyesalimika.

Mifano ni mingi. Angalia shule ya sekondari ya Sufa iliyopakana na shule za Glorian, Mwanakwerekwe C na Nyuki inayomilikiwa na jeshi la wananchi wa Tanzania. Lakini kati ya wanafunzi 40 waliofanya mtihani Sufa, ni saba tu waliosalimika huku Nyuki, Mwanakwerekwe C na Glorian, kukiwa hakuna aliyeguswa.

Nenda mbele zaidi. Fika Unguja mjini. Hapa kuna shule za sekondari za Hamamni, Benbella, Vikokotoni, Haile Selasie na Tumekuja. Shule zote hizi ziko ‘pua na mdomo’; wanafunzi wake “wanadurusu pamoja” na wanashirikiana na kutegemeana kwa kila kitu.

Lakini kati ya wanafunzi 176 waliofanya mitihani Hamamni, ni wanafunzi 14 tu waliopita kwenye chujio. Hawa 14 wamekosa alama w, lakini wanaongoza kwa D na F.

Kutokana na hali hiyo, natilia shaka uamuzi wa NECTA. Hii ni sawa na nyumba ya mtaa huu ikawaka moto, ile ya jirani ikasalimika ila moto huo ukaunguza nyumba zilizopo mtaa wa pili.

Kufuta matokeo ya baadhi ya shule hizo na kuacha nyingine zikiendelea kupeta, kwa kisingizio kuwa mitihani kwenye shule zao haikuvuja, hakuwezi kukubalika.

Kama mtihani umevuja kwenye shule moja, hauwezi kutovuja kwenye shule nyingine jirani, hasa kwa kuwa mtihani huu hufanywa kwa zaidi ya siku 14.

Kuna mambo matatu makubwa yanayoongeza mashaka zaidi kwenye uamuzi huu wa NECTA.

Kwanza, Dk. Ndalichako anasema mtihani umevuja na kwamba baadhi ya wanafunzi waliingia kwenye chumba cha mtihani na karatasi za majibu.

Lakini wakati mitihani hiyo ikifanyika, vyombo vya habari viliwanukuu baadhi ya wasimamizi wa mitihani wakisema “hakuna udanganyifu.”

Hakuna aliyesema wanafunzi wameingia kwenye vyumba vya mitihani na majibu wala aliyedai kuwa wapo baadhi waliokamatwa na simu. Wote waliohojiwa walisema, “Kila kitu kinakwenda vizuri kama kilivyopangwa.”

Walisema, “Hakuna lolote baya ambalo limetokea kwenye siku hii ya kufanyika kwa mitihani ya taifa,” na kwamba hadi mitihani inamalizika hakuna mwanafunzi aliyeripotiwa kupelekwa polisi kwa kosa la udanganyifu.

Pili, hoja kwamba udanganyifu umefanyika kwenye chumba cha mtihani haiwezi kukubalika.

Kwa mfano, wanafunzi wasiopungua 172, hawawezi kutosha kwenye chumba kimoja. Wanahitaji vyumba visivyopungua vinane (8).

Hivyo basi, kama kuna uvujaji wa mitihani, itakuwa umewahusisha wasimamizi wasiopungua 16 kwa shule moja na zaidi ya 200 kwa shule zote hizi.

Tatu, ni vigumu kwa shule moja ya Zanzibar ikavujisha mitihani na kuacha kuambikiza shule nyingine kutokana na zilivyojengwa, ushirikiano wake kati ya wanafunzi na wanafunzi na hata walimu kwa walimu.

Mathalani, mtihani hauwezi kuvuja Hamamni halafu usivuje Ben Bella. Wala hauwezi kuvuja Jang’ombe na usivuje Kidongochekundu. Vilevile, hauwezi kuvuja Mikinguni, ukashindwa kuvuja Lumumba, Nyerere na Shaurimoyo.

Aidha, kama mtihani umevuja Zanzibar, hauwezi kushindwa kuvuja Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na hata Rukwa, ambako ndiko wanafunzi wengi waliofanya vizuri wanatoka.

Ni vigumu kuamini pia kwamba kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, mtihani huu uliopenya siku mbili kabla siku kamili ya mtihani wenyewe, usiweze kuenea hadi Mtwara, Lindi, Sumbawanga na pengine Ruvuma.

Hii inathibitishwa na yale yaliyotokea mwaka 1997 ambapo mitihani ilivuja Dar es Salaam ikaangukia Mtwara, Lindi na kumalizikia Zanzibar. Vinginevyo, Dk. Ndalichako aseme, “Wanafunzi wa shule hizi wamefundishwa kuikataa mitihani ya nje.”

Kama hiyo haitoshi, kutokana na ukubwa wa alama hii ya (w), uvujaji wa mitihani huu, sharti uhusishe walimu wakuu wa shule. Taarifa ya NECTA haitaji mahali popote kuwa uvujaji huu wa mitihani ulihusisha walimu.

Mwandishi wa makala haya, Juma Said amejitambulisha kuwa ni mwalimu visiwani Zanzibar na msomaji wa siku nyingi wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu Na 0652 013301.
0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)