Hongera Dk Shein, hongera Seif Shariff


editor's picture

Na editor - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TANGU uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi nchini, chaguzi za rais, wabunge, wawakilishi na masheha kwa visiwa vya Zanzibar zimekuwa zikigubikwa na vurugu.

Vurugu hizo zilikuwa zilisababishwa na kile ambacho walioshindwa walikuwa wanadai kuporwa ushindi wao halali. Vurugu hizo zilitokea baada ya chaguzi tatu za mwaka 1995, mwaka 2000 na kiasi fulani mwaka 2005.

Katika uchaguzi mkuu wa 1995, Chama cha Wananchi (CUF) kilidai kuporwa ushindi. CUF ilidai mgombea wake Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa mshindi na si Salmin Amour wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na msimamo huo wa CUF, hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar ilichafuka ukazuka uhasama kati ya visiwa vya Pemba na Unguja, hadi Jumuiya ya Madola ilipoingilia kati na kupatanisha. Uliandaliwa mwafaka uliojenga mazingira mazuri ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Lakini, mambo yaliyokuwemo katika mwafaka huo wa kisiasa hayakutekelezwa kiasi kwamba waliingia katika uchaguzi kukiwa na tofauti. CUF iligomea matokeo na Januri mwaka 2001 waliandamana kupinga matokeo hayo.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika kwa amani Kisiwani Pemba, polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuzima; watu kadhaa waliuawa na mamia walikimbilia Kenya kujiokoa. Ili kuondoa hali hiyo, uliandaliwa mwafaka wa pili.

Lakini yalijitokeza yaleyale. Katika hali ambayo wengi hawakuitarajia Rais anayemaliza muda wake Zanzibar, Amani Abeid Karume alikutana na Maalim Seif, wakafikia maridhiano ambayo yalitambuliwa na kutungiwa sheria ili kuanzishwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Maridhiano hayo ndiyo yamesababisha mabadiliko ya hulka, kampeni zikafanyika kwa amani, utulivu na kwa kistaarabu kiasi kwamba ilipotangazwa kwamba Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM ameshinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2010, mpinzani mkuu Maalim Seif alikubali matokeo na akampongeza rais mteule.

Ni kutokana na uungwana, ustaarabu na mwelekeo huo wa busara, kwanza tunampongeza Dk. Shein kwa kuibuka mshindi baada ya Wazanzibar kumpa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Lakini pia tunampongeza Maalim Seif na chama chake kwa kukubali kushindwa katika kinyang’anyiro hicho. Huo ni ukomavu wa kisiasa na uzalendo wa kweli. Sasa tunawasihi mshirikiane kuijenga upya Zanzibar iweze kuwa na maendeleo endelevu kwa maslahi ya wakazi wa Zanzibar.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: