Hongera mliotaka kuiba nauli ya Rais


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

JAMBO la kwanza, nitoe hongera kwa wote waliotaka kuiba pesa zilizotengwa kwa ajili ya kuhudumia safari za nje ya nchi za Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete.

Nawapa hongera kwa sababu mtu mwenyewe kazidi safari, kila siku kiguu na njia – Ulaya, Marekani, China na hata Bara Hindi!

Nadiriki kusema bora pesa hizi zingeibwa, labda Rais wetu angetulia ofisini kwake angalau akasoma mafaili mezani kwake hata kama mafaili yenyewe yatakuwa ya kuagiza makampuni mengine ya kigeni ya kuchimba dhahabu kupewa vitalu vya kuchimba bure na bila kodi. Potelea pote.

Bila Rais wetu kukaa ofisini kwake ni lini tutapata fursa au nafasi kumweleza kero zetu? Madaktari wanagoma, Rais anaondoka kwenda kuhudhuria mkutano wa nchi zenye viwanda na zilizoendelea wakati Tanzania hatuna kiwanda hata kimoja na hatujaendelea.

Madaktari waligoma siku Rais wetu akitokea Ulaya na kutua Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa nchi za Afrika, siku hizi kifupi chake ni AU na siyo OAU tena. Rais anarejea nchini na bila hata kumaliza mwezi tena huyooo Brazili!!!

Tunachoambulia Watanzania ni picha za kiongozi wetu wa nchi akiwa pamoja na Marcio Maximo yule kocha mahiri wa timu ya taifa aliyeondoka nchini miaka si mingi iliyopita.

Na siku mbili baadaye tunaambiwa eti Maximo anakuja nchini kuifundisha Yanga timu ambayo Rais wetu na familia yake wanaishabikia!

Nikajiuliza sana, hivi kiongozi wetu alikwenda Brazili kushughulikia matatizo yetu kama Watanzania au alikwenda huko kuitafutia Yanga kocha? Mimi ambaye sikuona picha ya rais mahala pengine kama viwandani au mashambani huko Brazili, nisemeje?

Bora pesa zenyewe za safari ziibwe bwana, kwani safari zenyewe zinatusaidia nini? Sana sana labda Yanga watakaopata kocha huku wakifadhiliwa na mtu mmoja anayedaiwa kufahamiana na wamiliki wa kampuni moja ya kitapeli iliyochota pesa lukuki kutoka hazina yetu. Yanga bwana!

Jambo la pili nitamke wazi kwamba sioni sababu yoyote ya kutilia shaka habari hizo za kuibwa pesa zilizotengwa kwa ajili ya safari za SINDBAD wetu zilizoandikwa na gazeti hili Jumatano iliyopita. Kwa sababu hakuna aliyekanusha na vyombo vya kushangilia mambo ya viongozi kama TBC1 havijasema chochote.

Kwa wasiojua, Sindbad alikuwa msafiri tena baharia maarufu aliyeishi Baghdad zamani sana, enzi zile za Khalifa Mkuu, Harun el Rashid ambaye alifanya safari kuu saba kila pembe ya dunia na kujionea maajabu mengi ya dunia na hatari lukuki. Kwa hesabu zangu safari za kingozi wetu zimezidi za Sindbad.

Kwa mujibu wa habari hizo za wizi wa mapesa ya nauli ya Rais ni kwamba, maofisa watano wa Wizara ya Mambo ya Nje wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutaka kuiba zaidi ya Sh. 3 bilioni za kumstarehesha Rais wetu na msafara wake huko ughaibuni.

Maofisa waliosimamishwa kazi kwa mujibu wa habari hizo ni Mkuu wa Itifaki, Anthony Itatiro; Kaimu Mhasibu Mkuu, Kasimu Laizer;  Mhasibu, Deltha Mafie; Ofisa wa Itifaki, Shamim Khalifan, na karani wa fedha (cashier) Shaaban Kesi.

Habari hizi zimenifanya nikose usingizi kwa siku kadhaa sasa tangu nizisome Mwanahalisi. Najiuliza maswali mengi bila majibu. Hivi kama dili hili lisingegundulika hawa mabwana watano wangezificha wapi pesa zote hizi? Katika mabenki yetu au ughaibuni kama nanihii, yule wa Vijisenti?

Swali jingine linalonisumbua ni kwamba hili dili moja la shilingi bilioni tatu limevumburuka na kusababisha pesa zote hizo kuokolewa sasa je ni madili mangapi ambayo yalipita bila kugunduliwa na hivyo wahusika kuchota pesa kadri walivyopanga?

Yaani tangu enzi ya Rais wetu mpendwa aliyestaafu, Benjamin William Mkapa, zimekombwa pesa kiasi gani kwa staili kama hii ya kuandaa pesa za safari za rais kumbe hakuna safari yoyote na watu wanalamba dume – mabilioni yasiyopungua matatu?

Nasema hivi kwa sababu mnoko mwenzangu mmoja wa pale Mambo ya Nje kanithibitishia mambo mawili muhimu kuhusu tuhuma hizi. Kwanza kwamba hakukuwepo kabisa na safari yoyote iliyomhusu JK lakini wahusika wakaandaa safari feki na kuiombea pesa! Upo hapo?

Nasikia ziliandaliwa vocha za malipo, zikaandikwa hundi na kupitishwa zote bila tatizo na kupelekwa benki ambako pesa ziltolewa na kuletwa ofisini kwa ajili ya mgao lakini kumbe ngurumbili mmoja ambaye hakuwamo katika dili hilo alipata taarifa na kumtonya mkuu wa usalama.

Jambo la pili nililothibitishiwa ni kwamba Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ndiye aliyelishikia bango jambo hili la wizi na kwamba sasa hivi viongozi wengine karibu wote wamemgomea na wanadai kuwa eti hakuna pesa zilizoibwa bali eti yalikuwa mandalizi ya safari za rais siku za usoni.

Nasikia eti sasa hivi Membe kakalia kuti bovu pale Mambo ya Nje na kwamba kesi hii ya tuhuma za wizi wa pesa ikiisha yeye ndiye atakayebebeshwa lawama na hivyo huenda akang’olewa ili kumrejesha dada yetu Asha-Rose Migiro pale wizarani baada ya kurejea kutoka Umoja wa Maaifa.

Mimi yote hayo sitaki kuyasikia kwa sababu nimeyasikia mengi sana. Ninachotaka kusikia ni kwamba ni mara ngapi mipango kama hii haikuvumburuka kabla ya pesa kulipwa na hivyo wahusika wakakwapua mabilioni?

Je, mara ngapi pesa zilichukuliwa bila mtu yeyote kujua? Hapa ndipo ninapomwomba yule bwana maarufu wa kukagua hesabu za pesa za serikali, Ludovick Utoh aingilie kati na kukagua mahesabu tangu enzi za Mkapa hadi leo kuona kama kila pesa zilipochukuliwa rais wetu alikwenda safari?

Ikigundulika kuna safari ambazo zilitengewa pesa na kweli pesa zikachukuliwa lakini rais hakusafiri, basi hao ndio ‘magumashi’, wahusika wakamatwe, waswekwe korokoroni na kufunguliwa mashitaka.

Nasema tuanzie kipindi cha Mkapa kwa sababu kipindi hicho ndicho mali za umma ziligeuka kuwa mali za ikulu, nyumba za serikali zikawa za watumishi wa serikali, migodi ikauzwa kwa watoto, wakwe, marafiki na wajukuu zao. Tuanzie kipindi hicho hicho kukagua kila safari na kama watu walisafiri kweli.

0
No votes yet