Hoseah kajichafua tena, nani atamsafisha?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
DK. Edward Hoseah

DK. Edward Hoseah wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) amelikoroga tena. Kiongozi wa chombo hicho muhimu mno katika jamii ambacho hakika kutajwa kwake kokote pale kungetarajiwa kuamsha hisia na msisimko mkubwa hasa miongoni mwa watu waliokengeuka, kimechafuliwa tena. Mchafuzi ni yule yule, kinara wake.

Chombo ambacho kuundwa kwake kulipaswa kuwa pigo kwa watu wanaotumia vibaya nafasi walizo nazo ndani ya serikali, kinazidi kusiginwa.

Ingawa si haki kusema kwamba Takukuru tangu kuundwa kwake haijafanya lolote la maana hasa ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya kesi zimefikishwa mahakamani, lakini bado kuna tatizo kubwa la kimaadili linalokabili viongozi wa taasisi hii.

Kuna nyakati ofisi hii inatenda kwa njia inayoashiria ama upofu wa makusudi wa kutokujua mambo, au nia ovu ya kutaka kufunika na kupotosha mambo.

Sote tunakumbuka kwamba Andrew Chenge alijiuzulu wadhifa wa waziri wa miundombinu, Aprili mwaka 2008 ikiwa ni kama miezi miwili hivi baada ya kupewa wadhifa huo kufuatiwa kuundwa upya kwa baraza la mawaziri Februari 2008.

Baraza hilo liliundwa kutokana na kuvunjika kwa lililokuwa limeundwa Januari 2006 baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutokana na kuhusishwa katika sakata la Richmond.

Chenye alikabidhiwa wizara hiyo akitokea Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Lakini inafaa pia kukumbusha kuwa Chenge mbali ya kushika wadhifa wa uwaziri katika serikali ya awamu ya nne, pia alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuanzia 1995-2005, akitumika kidogo chini ya rais Ali Hassan Mwinyi na baadaye muda wote wa utawala wa serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa.

Kwa hiyo Chenge anapotajwa kokote ni vema ikaleweka kwamba anatajwa mtu mkubwa, anatajwa mtu ambaye kwa nyadhifa alizoshika serikalini alipaswa kuwa ni mtu anayeishi, kulala na kutembea na sheria.

Kutii na kusisitiza sheria na kanuni kwa kukalia kiti cha mwanasheria mkuu kwa miaka 10 si jambo dogo, maisha yake yanapaswa kuakisi sheria wakati wote.

Lakini mh! Chenge alijiuzulu wadhifa wake kutokana na kile kilichofichuliwa na wapelelezi wa Ofisi ya makosa makubwa ya jinai (SFO) ya Uingereza kuwa alikuwa amejiwekea akiba nono ughaibuni – kiasi cha dola milioni moja, (wakati huo Sh. 1.2 bilioni).

Fedha hizo zilihisiwa kwamba huenda ulikuwa ni mgawo wake katika kufanikisha serikali ya Tanzania kununua rada ya bei mbaya kutoka kwa kampuni ya kuuza vifaa vya kijeshi ya Uingereza ya BaE System.

Katika uchunguzi wa makachero wa SFO, Chenge alitajwa kama mtu aliyefanikisha ununuzi wa rada hiyo ya bei mbaya huku zaidi ya theluthi moja ya fedha za ununuzi ambazo ilitolewa na serikali zikitumika kama rushwa. Hivyo dhana imejengeka kwamba Chenge alishiriki mchezo mchafu katika ununuzi wa rada.

BaE wenyewe wamekwisha kukiri upungufu katika uuzwaji wa rada hiyo kwa Tanzania na imeahidi kuwa itakiri udhaifu huo mahakamani na kwamba wako tayari kutoa kiasi cha Sh. 30 bilioni ambayo ni kama fidia kwa Tanzania.

Mchakato wa kuhitimisha suala hili kwenye vyombo vya sheria nchini Uingereza bado haujakamilika. Kwa maana hiyo kwa kuwa Chenge anatajwa kwenye suala hilo, ambalo ndilo lilimfanya aachie ngazi mwaka 2008 ingekuwa ni vema na haki kama angesubiri utaratibu wa kisheria ufikie mwisho ndipo aseme kwamba yu safi katika hili au la.

Katika mazingira kama hayo, Chenge kuibuka nchini hivi karibuni alipokuwa akiusaka uspika na kusema alikwisha kusafishwa na Takukuru na hata Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) halikuwa kosa la bahati mbaya kwake.

Lakini ilipofika Dk. Hoseah wa Takukuru naye akaingia katika mchezo huo mchafu kumsafisha Chenye kwamba hana kesi katika sakata zima la rada wakati akijua wazi kwamba suala lenyewe halijaisha katika vyombo vya kisheria nchini Uingereza.

Hii ni aina nyingine ya kuitumbukiza taasisi hii ya umma katika mgogoro wa kununua ili kulinda maslahi ya maswahiba wake.

Wote, Chenge na Dk. Hoseah ni weledi wa sheria. Wamebobea, huyu mmoja ana shahada ya falsafa yaani PhD ya sheria na huyu mwingine kwa muda alioshika nafasi ya mwanasheria mkuu inampa sifa sawa na jaji wa Mahakama Kuu.

Pamoja na weledi wote huu, inakuwa ni vigumu kujua nini hasa kiliwatokea hadi kutumbukia katika ‘umbumbu’ mkubwa wa kusafishana hadi ubalozi wa Uingereza ulipoweka rekodi sawasawa?

Itakumbukwa kwamba suala la Richmond awali lilichunguzwa na Takukuru kabla ya Bunge kuunda kamati teule iliyoongozwa na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, kuchunguza mchakato wa mkataba wa Richmond, lakini Takukuru ilisafisha kila kitu na kusema wazi kulikuwa hakuna lolote baya ndani ya mkataba wa Richmond.

Hata pale Takukuru iliposhindwa kwenda mbali zaidi kwa mujibu wa madaraka yake kisheria, haikushauri lolote kwa maana ya kuendeshwa kwa uchunguzi wa kina kwa vyombo vingine ambavyo vingelifikisha suala hilo mwisho mwema.

Ripoti ya Kamati ya Bunge iliitaja Takukuru hususan Dk. Hoseah katika uzembe wa makusudi kwa kufunika kombe katika sakata zima la Richmond. Ilishauri mamlaka husika zimchukulie hatua Dk. Hoseah, lakini hadi leo yupo.

Baada ya kulikoroga katika Richmond, sasa amelikoroga tena katika rada. Swali langu linajikita hapa, je, kwa utendaji na matendo ya Dk. Hoseah hivi Takukuru inaweza kuogopwa kama ukoma na wale wote wanaovunja sheria, kanuni na taratibu za ofisi za umma walizokabidhiwa?

Je, Dk. Hoseah anaweza kuendesha uchunguzi wa jambo lolote lenye manufaa kwa umma kama utendaji wake umetiliwa shaka katika mambo haya makubwa mawili.

Dk. Hoseah anaweza kujenga dhana kwamba anaandamwa, lakini ni vema akakumbuka kwamba Taasisi anayoongozwa ni nyeti na yenye kubeba dhamana kubwa sana katika taifa hili, kwa hiyo kitendo cha kujiruhusu kila wakati kuzingirwa na tuhuma nzito na kubwa kubwa kama hizi, hakimpi usafi wa kuendelea kukalia kiti hicho.

Tuhuma hizi zinamchafua yeye binafsi lakini pia zinachuruzika na kuchafua hata kiti cha ofisi aliyokalia, hii hailindi na kukuza taasisi anayoongoza.

Dk. Hoseah katika suala zima za uchunguzi wa rushwa ya rada hakuwahi kusema kokote hadharani kwamba walikuwa wanamchunguza Chenge, lakini ilikuwa kazi rahisi na kwa kasi kubwa kuibuka na kumsafisha hadharani katika mkakati unaozidi kuthibitisha pasi na shaka yoyote kuwa moyo wake ulikuwa mzito kufanya uchunguzi dhidi ya kigogo huo.

Uzito wa moyo unatokana na hisia za wengi kwamba Takukuru imekuwa ikiendesha upelelezi kwake kwa kutazama sura.

Hisia hizi zilitawala sana wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, na hata wakati kampeni za uchaguzi mkuu, kwani kuna watu waliandamwa si kwa sababu ni wao tu walitoa rushwa au mawakala wao, ila kwa sababu ya mkakati maalum wa kushughulikiana.

Ni hisia kama hizo zilizotawala kwa mfano, alipokamatwa aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Margaret Sitta. Wengi walikumbuka ugomvi wa Dk. Hoseah na Bunge juu ya Richmond, wakati huo Bunge likiwa chini ya Spika wa kasi na viwango, Samwel Sitta.

Hisia mbaya dhidi ya Takukuru zinazojitokeza nchini mara nyingi zimeegemezwa katika upendeleo wa wazi wa kufanyia uchunguzi baadhi ya mashauri ambayo hujitokeza katika picha ya kukomoana na kulipiza kisasi.

Hali hii inaifanya Takukuru kujiondoa kwenye mstari wa kiweledi katika kutimiza wajibu wake kwa jamii. Katika mjumuiko wa mambo haya si uchimvi kuhoji kama Dk. Hoseah bado yuko Takukuru akisubiri nini. Na kama amekataa kuondoka yu wapi basi wa kumuondoa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: