Hoseah kamwaga mboga, wabunge watamwaga ugali?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Edward  Hoseah

NCHI ina shida. Hatua ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Edward Hoseah, kuitisha mkutano na waandishi wa habari kisha kuzungumzia kile ambacho kila siku taasisi hiyo imekataa kuzungumzia, ni kielelezo kwamba nchi sasa ina shida.

Kwa kawaida Takukuru imekuwa ikisimamia katika sheria yake kwamba ni marufuku kuzungumzia kesi/suala lolote ambalo liko chini ya uchunguzi wake; hii ndiyo imeifanya Taasisi hii ikatae kueleza ilikofikia katika kesi kubwa inazodai inazichunguza.

Miongoni mwa kesi ambazo Takukuru haitaki kuzigusia hadharani kama alivyofanya Hoseah juzi ni pamoja ukwapuaji wa Sh. 40 bilioni uliofanywa na kampuni ya tata ya Kagoda. Hadi sasa Hoseah hajasema nani hasa wamiliki wa Kagoda.

Hajazungumzia ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika ununuzi wa rada, Meremeta na Deep Green. Makampuni haya yamezima kiasi kikubwa cha fedha za walipa kodi.

Sasa Hoseah anapojitokeza hadharani na kuzungumzia tuhuma za kuchunguza posho za wabunge, lakini akigoma kuzungumzia Kagoda na washirika wake, haraka tunajiuliza kuna nini?

Hilo ni swali la kwanza, najua wapo wanaosema kwamba Hoseah ametumia haki yake kikatiba kujibu kauli mbalimbali za wabunge juu ya kuhojiwa kwao na Taasisi hiyo. Lakini zaidi akieleza ni kuweka rekodi sawa juu ya madaraka ya Takukuru katika kutimiza wajibu wake.

Ingawa hoja hii inaweza kuwa na mshiko, lakini si kweli kwamba eti suala la posho za wabunge limepigiwa kelele zaidi kuliko Kagoda, Meremeta, Deep Green au rada  kiasi cha kumfanya Hoseah atoke mafichoni na kuvunja sheria yake mwenyewe. Sheria inayozuia kuficha uchunguzi unaofanyika.

Kinachoonekana hapa ni kwamba Hoseah anataka kujitetea yeye binafsi kwa upande mmoja na Taasisi yake kwa upande wa pili, lakini katika kufanya hivyo amejikuta akiangukia katika mtego mbaya wa mivutano ya makundi.

Hakuna ubishi kwamba Hoseah anakabiliwa na kibarua kigumu juu ya sakata la Richmond, ambalo kwa takribani miaka mitatu sasa limeigawa nchi katika makundi mawili makubwa.

Kwa bahati mbaya makundi haya yanajitokeza kwenye sura ya kuhasimiana. Ndani ya Bunge kuna migawanyiko na kukamiana.

Wapo wanaoamini kwamba viongozi walifanya mchezo mchafu katika kupitisha Richmond; walakini walijua kuwa kampuni hiyo ilikuwa dhaifu mno, lakini waliamua kufumba macho kuruhusu kandarasi.

Wanasema hiyo haikufanyika kwa bahati mbaya, bali kuna mchezo mchafu nyuma yake.

Kwa uchambuzi wa haraka haraka, kauli ya Hoseah ni mwendelezo wa makundi ya Richmond, ni mwangwi wa mapambano ama ya ndani kwa ndani serikalini au kwenye chama tawala, juu ya makundi maslahi.

Ni jambo la kujiuliza tena na tena, Hoseah amepata wapi ujasiri na nguvu za kusimama pekee yake kutangaza mapambano ya hadharani dhidi ya Bunge licha ya kujua kwa hakika kwamba hata mihimili miwili ya madaraka ya dola, yaani Bunge na Serikali (utawala) inasigana kuhusu Richmond na posho za wabunge?

Nani kamtuma Hoseah, je, ameamua kujitoa muhanga mwenyewe au ana kundi kubwa nyuma yake na kwa namna ilivyo, kundi la watawala? Ni akina nani hasa hawa katika mpambano wa sasa?

Kuna habari ambazo hazijakanushwa kuwa Spika Samwel Sitta na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wamepishana kuhusu hatua za kuhojiwa kwa wabunge juu ya uchukuaji wa posho mbili.

Wakati Sitta amekataza mbunge yeyote kuhojiwa katika suala la posho bila ofisi yake kutaarifiwa, Pinda anasema Takukuru itaendelea na mahojiano ya wabunge hao. Hapa ni dhahiri kuna shida, kuna msigano wa mihimili ya madaraka ya dola. Nchi ina shida kubwa.

Kwa muda mrefu habari na uvumi wa kila aina umeenezwa nchini juu ya watu kujipanga kusafishana katika sakata hili. Serikali wakati wa mkutano wa 16 iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya Richmond, ambayo yalikataliwa.

Kwa maneno mafupi serikali ilifukuzwa na taarifa yake na ikapewa hadi Novemba 2009 wakati wa mkutano wa 17 kuwasilisha taarifa ya maana si ubabaishaji ulionekana katika ripoti ya mkutano uliyopita.

Tena ripoti iliwasilishwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima badala ya Waziri Mkuu Pinda mwenyewe.

Sasa kuibuka kwa Hoseah wakati huu, Richmond ikiwa inaepuliwa jikoni, je, ni mbinu ya kuvuruga mjadala na mwelekeo mzima wa sakata hili? Je, ni mbinu za kuleta mgawanyiko zaidi miongoni mwa wabunge?

Haya ni maswali magumu kujibu kwa sababu, si rahisi kujua kama Hoseah amesimama peke yake kwa sasa au kuna kundi kubwa la watu ndani ya serikali nyuma yake, au kuna wadau wa kutaka kashfa ya Richmond ife kifo kibaya?

Juhudi za Hoseah hapana shaka ni njia mojawapo ya kupanua wigo wa mapambano, sasa hoja kubwa ndani ya Bunge ni mbili; moja, kuhusu kuhojiwa kwa wabunge na hatma yao; mbili, kiporo cha Richmond.

Kupanuliwa kwa mapambano haya kunavunja nguvu za wabunge kujielekeza kwenye jambo moja, mgawanyiko unazidi na kwa maana hiyo kile kilichokuwa kinatarajiwa kwenye Richmond hakiwezi kupatikana kwa sasa.

Kuna kila dalili ndani ya serikali kuna mikono inayotaka hali hii iendelee ili kufanya suala la Richmond life kifo cha kawaida, ukijihoji kwa mapana yake inakuwa ni vigumu kuona wabunge wakimnyamazia Hoseah kwa kauli zake za sasa juu ya nafasi ya Takukuru.

Kama ni mahesabu yamepigwa vizuri sana , kwamba wiki ya mwisho ya mkutano wa 17 ambayo ripoti ya Richmond itawasilishwa, hoja nzito imerushwa uwanjani si tu ili kutibua nyongo za watu, ila kuleta hali ambayo inaweza kabisa kugonganisha kwa nguvu zaidi mihimili ya dola.

Haya hakianzishwa na Hoseah, kamati ya wazee wa busara ya Halmashauri Kuu ya CCM ya kutafuta chanzo cha uhasama miongoni mwa wabunge wa CCM na dhidi ya serikali yao, ipo Dodoma kuhojiana na wabunge.

Kamati hiyo inayoongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ikiwa na wajumbe Pius Msekwa na Abdulrahaman Kinana, ingawa ilikwisha kusema haifanyi ukachero wowote dhidi ya wabunge, ina nguvu zake katika kuvuruga mawazo na mitizamo ya wabunge.

Je, haya yote yanatokea kwa bahati mbaya? Kuna mkakati wa kundi au makundi katika haya? Je, kuna mshikamano wa kitaifa katika masuala haya yote au ndo nchi inazidi kujichimbia katika matatizo?

Katika wakati mgumu kama huu yu wapi basi wa kujitokeza na kurejesha taifa katika njia iliyonyooka? Ipo shida kubwa inanyemelea taifa kwa kuwa kidogo kidogo tunageuka jamhuri ya kambale, kila mmoja ni mbabe na mkubwa. Iko shida inakuja, tutaona mengi kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: