Hoseah njia panda


Rehema Shaibu's picture

Na Rehema Shaibu - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version
Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah

TUHUMA dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zinazidi  kulundikana.

Ni tuhuma nyingi bali tuangalie chache zifuatazo. Kwanza, kwamba alitumia zaidi ya Sh. 320 milioni kukarabati nyumba ya taasisi hiyo na kuiwekea fenicha kisha “akainunua” kwa Sh. 40 milioni.

Kwa bei ya sasa ya soko, kiwanja peke yake, katika eneo la Oyster Bay iliko nyumba hii kinaweza kugharimu zaidi ya Sh.40 milioni.

Kwa gharama ya kiwanja, ukiongeza gharama ya nyumba iliyokuwemo na kuongeza gharama ya ukarabati na fenicha kama ilivyoelezwa hapo juu, ununuzi wa nyumba hiyo kwa Sh. 40 milioni unazua  utata.

Si hayo tu; kwamba nyumba iliyokarabatiwa na kwa mamilioni kwa ajili ya Mkurugenzi wa TAKUKURU na siyo Hoseah, sasa imenunuliwa na Hoseah na kuacha taasisi bila nyumba kwa mkuu wake.

Kwa msingi huo peke yake, tayari ununuzi huo unakuwa miongoni mwa “ununuzi mbaya” ambao tayari serikali iliishaamua kuwa sharti ubatilishwe. Lakini kwa nyumba ya TAKUKURU, bado kimya.

Lakini kuna jingine hapa kwamba, ingawa nyumba iliuzwa baada ya serikali kutangaza kusitisha zoezi la kuuza nyumba za serikali (2006), hadi sasa mnunuzi hajalipa hata robo ya bei ya “kununulia.”

Pili, Hoseah anatuhumiwa kuibeba Richmond; ile kampuni hewa ambayo ilipendelewa kupewa zabuni ya kufua umeme wakati haina wataalam, utaalam, wala fedha.

Ni TAKUKURU ya Hoseah iliyotoa taarifa kwamba Richmond haikuwa imeleta hasara yoyote kwa serikali; huku hata ambaye hakwenda shule alibaini utukutu wa kifisadi ndani ya mkataba.

Kilicholeta kizaazaa zaidi ni Hoseah kutaka Bunge la Jamhuri lisijadili suala la Richmond kwa madai kuwa tayari taasisi yake ilikuwa imemaliza kazi ya kuchunguza.

Ni ujasiri wa Bunge uliosaidia kuvunja ngome ya usiri wa Hoseah na kuibua mambo ambayo Kamati ya Bunge iliyatumia kupendekeza kuwajibishwa kwa Hoseah.

Tatu, Hoseah anatuhumiwa kuvujisha taarifa za Taasisi ya Makachero ya Uingereza (FSO) inayochunguza kashfa inayohusu ununuzi wa rada nchini.

Inadaiwa kuwa makachero walitaka kuhoji kwa wakati mmoja, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Idris Rashid.

Hata hivyo zimepatikana taarifa zikidai kuwa ni Hoseah aliyefanikisha kuwafikishia taarifa wawili hao na kusababisha wao kupanga majibu ya kutoa dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Dk. Rashid anadaiwa kupokea Sh. 1.3 bilioni kutoka kwenye akaunti ya Chenge nchini Uingereza; fedha ambazo zinahusishwa na mgawo kutoka kwenye hongo kubwa katika ununuzi wa rada kutoka kampuni ya BAE nchini humo.

Wakati Chenge na mkewe wanatuhumiwa kumiliki akaunti yenye zaidi ya Sh. 1.7 bilioni nchini Uingereza.

Chenge, hata hivyo, anatuhumiwa pia kuhamisha kutoka akaunti yake kiasi cha Paundi za Uingereza 600,000 (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 1.3) kwenda kwenye akaunti ya Dk. Rashid katika kipindi ambacho Dk. Rashid alikuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT).

TAKUKURU, taasisi ambayo Hoseah anaongoza, ndiyo inapaswa kuwa mlinzi wa maadili ya nchi na utawala.

Tuhuma ambazo zinamkabili Hoseah hivi sasa zinampunguzia au kumwondolea kabisa sifa za kuongoza asasi inayopaswa kutawaliwa na uadilifu wa hali ya juu.

0
No votes yet