Hoteli ya Bwawani, mfano hai wa ufisadi SMZ


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Hoteli ya Bwawani

MZUNGU mmoja raia wa Ufaransa, Jean Nicolaus, tuliyekutana mwaka 1992 kijijini Jambiani, kusini mashariki mwa kisiwa cha Unguja hakujua kama hoteli aliyoipenda sana miaka ile ingepotea kutokana na ufisadi.

Jean niliyekuta naye nikiwa likizoni, wiki chache kabla ya kurudi kijiji hicho kuoa - Jambiani ndiko asili ya wazazi wangu, na asili ya wakwe zangu – aliniambia: Fukwe hizi bikira ni kivutio cha kwanza. Kivutio cha pili ni Hoteli ya Bwawani. Ni hoteli nzuri sana ile kwani kila nikija ndipo ninapofikia nikiwa mjini.

Ni bahati mbaya mawasiliano yetu yamepotea ingawa angetokea leo Jean, naamini angeugua. Nimemkumbuka kutokana na hali mbaya ya hoteli hii ambayo si Jean peke yake aliyekuwa anatoka udenda kwa vile alivyopenda.

Uzuri wa fukwe za visiwani Zanzibar ni jambo la asili kwa kuwa hazijaharibiwa sana. Tatizo kwa Jean lingekuwa uzuri wa hoteli aliyoitaja ambao asingeukuta tena. Angekuta hoteli iliyofisidiwa kutokana na uongozi mbaya kuanzia hoteli, wizara mpaka serikali kuu.

Hoteli iliyomalizika kujengwa miezi ya mwishomwisho ya utawala wa mzee Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa riasi 7 Aprili 1972, imefisidiwa. Haijafanyiwa matengenezo makubwa kwa miaka mingi. Vyumba vyake havivutii tena kama ilivyokuwa zamani hata kupendwa na wazungu.

Vifaa katiaka vyumba vingi vimeharibika na kuachwa kwa muda mrefu bila ya matengenezo. Eneo la mbele halitazamwi kama lilivyokuwa. Mazingira na mandhari ya kilichosukuma iitwe hoteli ya Bwawani, yanasubiri mwenyewe kung’ara tena.

Ukumbi mkubwa wa mikutano umepoteza mvuto kama ulivyopoteza ukumbi mdogo ulioko jengo jingine la ghorofa moja karibu na bahari. Zile nguvu za utoaji huduma za kisasa zilizokuwepo, hazipo tena. Ukitaka kuhudumiwa utangulize malipo.

Hoteli ya Bwawani mbali na majengo ya vyumba vya kulala na sehemu za kufanyia mikutano, ina jengo la burudani. Sehemu ya chini ni ukumbi wa disko usiotoa sauti nje, na sehemu ya juu ambako ni wazi, kuna baa ndogo na sehemu za kubarizi, pamoja na bwawa dogo la kuogelea linalovutia nyakati za usiku.

Nimetaja hoteli yenye raslimali nyingi. Vyumba vya wageni, ukumbi mkubwa wa mikutano wa Salama, ukumbi mkubwa mwingine wa mikutano ulioko jengo kubwa la hoteli, ukumbi mdogo kwenye jengo dogo, mkahawa na baa ya Pemba vilioko sehemu ya chini ya jengo dogo, ukumbi wa disko uitwao Komba uliogandana na ukumbi mwingine mdogo wa mikutano.

Hoteli ya Bwawani siyo tena ile ambayo mikutano yote ya kitaifa na kimataifa ikifanyika. Siyo tena ile ambayo maveterani wa uandishi na wanataaluma wengine wakifikia miaka ya 1980. Siyo. Nini kimeifikisha ilipo sasa?

Hakuna isipokuwa UFISADI. Baada ya kupunguza mvuto kwa kuelemewa na madeni na kukosa uwezo wa kujiendesha, viongozi hawakutaka kuinusuru, bali kuifanya kitegauchumi chao. Hawakujali hata wafanyakazi wake 260 kwani bado wanatambuliwa kama vibarua.

Viongozi waliokuwa na ushawishi kimadaraka waligawana vyumba. Mmoja utakuta ana vyumba viwili au vitatu: kimoja cha matumizi binafsi, kingine cha wageni wake maalum ambao inawezekana walilipia lakini fedha zikabaki kwao.

Hoteli ikakosa uwezo wa kujiendesha. Ikafikia hatua kwamba mteja alipe ndipo ahudumiwe. Huduma zikawa mbovu na zilizojaa ulalamishi. Ile wanayoita wakaguzi wa hesabu, “Value for Money” ikawa ndoto. Unalipa fedha uhudumiwe, lakini huduma unayoipata hailingani na thamani ya fedha ulizolipa.

Uongozi wa kifisadi ulianza mara tu ilipoingia serikali ya awamu ya sita. Wajanja wakatumia mgongo wa chama kufisidi. Wakati wanaingia, menejimenti ilikuwa imefanikiwa kupata Sh. 60 milioni na kununua vyombo vya muziki nchini Dubai.

Mpango ilikuwa ni kuvitumia kupiga muziki ambapo mapato yangesaidia kuitengeneza na kulipa madeni.

Wajanja waliobebwa na Ikulu wakapora vyombo na kuvimilikisha kitapeli. Ni hapa kila mwezi hoteli ikigaiwa Sh. 1.5 milioni.

Novemba 2004 serikali ililazimisha mradi uliokuja kuwa ni wa kuikamua Bwawani. Ukumbi wa disko, chanzo kikubwa cha mapato, walipewa National Marketing Company (NMC) ambayo nyaraka za msajili wa makampuni zinaonyesha majina ya Haji Omar Kheri na Saleh Ramadhan Ferouz, viongozi waandamizi wa CCM. Lakini Kheri, pia ni Waziri wa Utumishi na Utawala Bora katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Ukodishaji wa ukumbi wa disko wa Komba haukutokana na zabuni ambayo ingeruhusu ushindani. Jina la Ibrahim Hussein (Bhaa) ndilo lililojitokeza awali lakini ilipofikia Disemba 2004, NMC ikaingia kwa utaratibu wa mgawano wa mapato wa asilimia 40-60. Utekelezaji wa mkataba ulianza Januari 2005, makubaliano yakielekeza mkataba uwe unapitiwa kila mwaka.

Taarifa zilizopo hotelini zinasema kwa karibu mwaka mzima tangu mkataba huo ulipomalizika Disemba 2005, ukumbi uliendelea kudhibitiwa bila ya kuwepo utaratibu muafaka wa kugawana mapato.

Kutokana na deni kubwa la umeme, hoteli ilikatiwa umeme na hivyo kuishi miezi kadhaa bila ya umeme kwa kuwa hapakuwa na jenereta hadi lilipokuja kununuliwa na Wizara ya Fedha lakini lilipofikishwa hotelini, likatumika kuendeshea burudani ukumbini. Wageni wakaishi kwa umeme wa kuvizia.

NMC iliyowahi kulalamikiwa kwa kutopeleka mapato CCM ingawa iliposajiliwa mwaka 1999 ilitajwa kama kampuni tanzu ya chama, imefanikiwa kupenya tena kudhibiti ukumbi wa disko katika mkataba mpya unaomsononesha hata waziri wa habari, utamaduni, utalii na michezo, Abdilah Jihad Hassan.

Katibu Mkuu wa Wizara, Ali Mwinyikaji anasema NMC wamepewa haki ya kuendesha ukumbi wa disko kwa mkataba wa mwaka mmoja mmoja kwa gharama ya Sh. 15 milioni kila mwezi. Lakini, wakati ilitarajiwa NMC ilipe kwa mkupuo Sh. 60 milioni, kwenye akaunti ya hoteli zimeingia Sh. 40 milioni tu.

Isitoshe, yapo malalamiko kwamba wizara imesimamia kifisadi makubaliano kwani wakati zabuni iliitishwa, imewapa NMC waliotoa bei ndogo. Waombaji wengine waliojitokeza ni Prime Time waliotoa bei ya Sh. 15 milioni na Zanzibar Media Corporation (ZMC) waliotoa Sh. 17 milioni.

Mwinyikai, mwandishi wa habari kitaaluma, anasema NMC wamethibitisha uwezo huku ZMC “wakishindwa kuthibitisha uwezo wao.” Wizara iliwatoa Prime Time kwa kuwa ni vigumu kuwadhibiti kwani haikusajiliwa Zanzibar.

Hilo linapingwa na Meneja Masoko wa ZMC, Said Khamis: Tuna uwezo wa kuendesha redio, gazeti ambalo halina faida na tunakamilisha taratibu za kuendesha televisheni. Hatuwezi kushindwa kusimamia ukumbi wa disko. Tuna kampuni siyo kama wengine. Tatizo lao (Wizara) hawakutafuta watu wenye utaalamu wa masuala ya benki ili wafahamu ni nini kinachozingatiwa na benki katika kutambua uwezo wa kampunia kulipa. Wangeambiwa kuwa si salio isipokuwa ni mapato ya mwezi. Sasa sisi Zanzibar Media Corporation tuna mapato ya hadi Sh. 200 milioni kwa mwezi, tutashindwaje kulipa Sh. 17 milioni. Wangeleta mtaalamu wa masuala ya benki angefahamu tuliposema kwamba unaweza kukuta akaunti haina kiasi cha pesa kinachotakiwa, lakini fedha nyingi tumewekeza. Tunapata matangazo ambayo yakilipwa fedha zinarudi. Hawakusema ukweli. Wamepotea njia.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: