Hotuba ya rais imepuuza mambo muhimu


Karoli Bahati's picture

Na Karoli Bahati - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version

HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la 10 uliofanyika 18 Novemba, 2010 mjini Dodoma, imenigusa sana na kunichokoza. Vizuri niijadili.

Ni kinyume na matarajio yangu. Niliamini rais atatoa mwelekeo mpya wa taifa kimaendeleo kwa miaka mitano ijayo. Nikajua pia atawapa wananchi matumaini kuhusu mikakati ya kuwaondolea umasikini.

Nilijua atadurusu hali ya nchi kimshikamano na kutandika misingi ya namna atakavyoimarisha umoja wa kitaifa uliodhoofika kutokana na tofauti ya maendeleo waliyonayo wananchi.

Yote matatu aliyapuuza. Alichokifanya ni kugusagusa masuala ya jumlajumla. Ilitakiwa aingie kwa undani na kuyatolea majibu. Na hapo ndiyo wananchi wangepata matumaini.

Nilibaini katika maneno yake yasiyokuwemo kwenye hotuba iliyoandikwa, amesema nchi yetu imeingia katika mpasuko mkubwa wa kidini na uchaguzi umetuacha katika hali hiyo, hivyo tunahitaji kuisahihisha.

Hapa rais amezungumza hisia tu na kwa bahati mbaya anazipeleka ndani ya bunge na dunia.

Ninavyokumbuka, kabla na baada ya uchaguzi mkuu, viongozi wa dini walifika ofisi kuu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika safari ya kufikisha walichoita “ujumbe wa amani.”

Viongozi hao waliotoka dini zote kuu, yaani ya Kikristo ikichanganya madhehebu tofauti, na ile ya Kiislamu, walisema wanapeleka ujumbe huo kwa kila chama kilichoshiriki uchaguzi mkuu.

Kwa hatua hiyo iliyoendana na kukaa kwao pamoja kwa minajil ya kupanga kuiombea nchi amani, huo udini anaouzungumzia rais umetokea wapi?
Mpaka kesho, Watanzania tunapokwenda sokoni au dukani hatuulizi duka la Abdallah au la Mathayo. Tunanunua bidhaa bila ya kuzingatia nani mwenye duka fulani.

Tunapanda daladala, bajaji, bodaboda na baiskeli bila ya kumuuliza mwendeshaji “wewe ni wa dini gani” au “bajaji yako mwenyewe Mkristu au Muislamu.” Tunapata huduma kwa uhuru.

Tunakunywa maji ya chupa bila ya kujali ya aina fulani yanatengenezwa na kiwanda cha nani. Mtu ananunua kwa utashi wake siyo kwa kufuata dini.
Watu wamepiga kura bila ya kuzingatia dini ya mgombea. Wapo Wakaristu wamechaguliwa na Waislamu na kinyume chake.

Yeye mwenyewe Rais kupata kura nyingi eneo kama la Rombo ambako Wakristu ni zaidi ya asilimia 98 isingewezekana kama Watanzania wanapiga kura kwa kuangalia dini ya mgombea.

Inafaa rais akapima kwanza uzito wa kauli zake kabla ya kusema jambo zito kwani tungali na utamaduni wa kumsikiliza kiongozi asemacho.

Lakini tuseme kweli Tanzania pana udini; mbona Rais hakutupa maelezo ya mikakati ya kuukomesha? Haikustahili hata chembe rais kuishia kulalamikia tatizo.

Alichosema katika hili ni umoja. Huu ni ukweli lakini iko wapi mipango ya kuhakikisha umoja unaimarika? Au hajui umoja wa Watanzania unahatarishwa sana na kupanuka kwa matabaka kunakotokana na tofauti ya kipato waliyonayo?

Leo wapo wanaosoma kwa uhakika na kujihakikishia ajira kwa urahisi. Lakini wapo wanaosoma kwa kubahatisha. Hali iko hivyohivyo kwa matibabu na hata makazi, mambo yaliyo ni mahitaji ya msingi ya binadamu.

Nilitarajia Rais azungumzie haya na kuwapa wananchi mwelekeo ili warejeshe imani yao kwake na kwa serikali anayoongoza.

Rais angekuwa muungwana kwa kukiri kuwa Watanzania wamepunguza imani kwake na kwa chama chake CCM. Bali tungetaraji aeleze angeshawishije wananchi warudishe imani kwake.

Rais alitumia muda mwingi kueleza mafanikio ya awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Kwanini rais aliyeshinda apiganie kurudi nyuma? Au haamini kuwa hicho anachoita mafanikio ndicho kilichomrejesha madarakani na kwa maana hiyo tayari Watanzania wanafahamu?

Alichotakiwa kukisisitiza ni namna ya kukabili changamoto zilizopo kisera, kimkakati na kidhamira. Ni vigumu katika hotuba ya siku moja rais kuamini anaweza kuzungukia kila wizara na sekta zake na vipaumbele vyake.

Ingetosha tu kutoa mwelekeo wa serikali atakayounda katika mambo hayo.
Watanzania wanajua wanapewa serikali kubwa mno na hivyo kubebeshwa mzigo wa kuigharamia wakati raslimali ni haba na ziliopo zinatumiwa vibaya na viongozi wanaopewa dhamana. Ilikuwa ni chagamoto kubwa kwa rais kueleza atarekebishaje kasoro hizo.

Serikali inasomesha watu wengi kwa gharama kubwa lakini wengi wao huishia nje; mikataba tuliyonayo ya imejaa kasoro na kutoa mianya kwa Watanzania kunyonywa haki zao.

Haitoshi hata kidogo rais kuthubutu kujivunia tarakimu na ikawa ndio mafanikio. Atasemaje akiulizwa ni kiasi gani cha mapato huvuja kila mwaka kutokana na utalii, kwa mfano?

Alichokifanya rais ni sawa na “funika kombe mwanaharamu apite.”
Alipogusia uimarishaji wa demokrasia, akajivunia ongezeko la idadi ya vyama vya siasa, asasi za kiraia, mabaraza ya madiwani na bunge.

Nilidhani angeendelea mpaka kutaja mipango thabiti ya kuimarisha demokrasia kupitia taasisi hizo ikiwemo kuzipatia raslimali za kutosha ili kuziongezea ufanisi.

Hapa ningetaraji ajadili madai ya muda mrefu ya Watanzania kupata katiba mpya. Watanzania wanataka katiba inayozungumzia mfumo mzuri zaidi wa kuendesha uchaguzi ngazi zote: serikali za mitaa, vitongoji na vijiji na ule wa madiwani, bunge na rais.

Inatakiwa katiba inayoshurutisha kuwepo tume huru za kusimamia uchaguzi na kuruhusu wagombea binafsi kushiriki, pamoja na kuidhinisha mahakama au tume maalum ya majaji kuthibitisha matokeo ya urais.

Rais angeeleza ni vipi katiba mpya itatambua muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hasa katika hali ya sasa ambapo upande wa Zanzibar, kuna serikali ya umoja wa kitaifa kati ya vyama viwili tu vya siasa.

Pia rais angezungumzia matumizi ya fedha na raslimali nyinginezo katika siasa na mgawanyo wa madaraka kwa kuzingatia mihimili mitatu ya dola: Serikali, Bunge na Mahakama.

Inasikitisha Rais ameyaacha yote haya kama vile si mambo muhimu yanayohitaji majibu muafaka. Amesahau mambo hayo yanachangia sana maendeleo ya nchi.
Hivi kweli rais anaona ni halali mtu aliyepata kura milioni mbili abaki kijiweni akisubiri miaka mitano ijayo huku kina Zakia Meghji wakitolewa juani na kuteuliwa wabunge bila ya jasho?

Nilidhani rais yeyote makini na mpenda demokrasia angejikita katika kushawishi Watanzania waendelee kusubiri na kumwona kuwa yeye ni rais mzuri isipokuwa tu mfumo ndio mbaya.

Hapa ndipo wabunge wa CHADEMA wanaposimamia. Ulezi wa raia ni moja ya kazi kuu za rais. Kutambua matatizo yao na kuyashughulikia ikibidi kidharura, kunaleta amani ya kweli na utulivu wa moyo na akili.

Kunawachochea kupata hamu ya kuchangia maendeleo ya nchi yao.
CHADEMA wamebainisha manung’uniko yao mbele ya rais na walishasema ndiye rais bali azingatie kilio chao. Inatakiwa waulizwe wanaumizwa na kitu gani?

Kusema kwamba yeye ndiye rais na hakuna mwingine ni kiburi tu cha madaraka. Lakini alichokionyesha zaidi rais ni hofu yake juu ya uhalali wake.
Rais muungwana anajiamini. Anajenga mazingira ya kuongoza na kuunganisha watu wake bila ya kujali utofauti wa vyama vyao.

Hiyo ndiyo mantiki ya kiapo chake: Nitaongoza bila ya kubagua kwa namna yoyote ile; Nitaheshimu, kuilinda, kuihifadhi na kuitetea katiba ya nchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: