Hotuba za Kikwete za kufurahisha wawekezaji


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imesababisha methali ya ‘Karibu mgeni mwenyeji apone’, ichujuke na ikose maana. Maana mpya ni karibu mgeni mwenyeji avurugikiwe, achanganyikiwe awe mtumwa katika ardhi au nyumba yake.

Mwenyeji amekosa uhuru, haki, mamlaka na uwezo wa kumpa jembe mgeni akalime baada ya siku ya nne kama tulivyosoma vitabu vya zamani. Mgeni siku ya kwanza anapewa wali na panza…siku ya nne anapewa jembe akalime…siku ya 11 anaondolewa kwa mateke na ngumi.

Lakini mgeni wa leo hasa anayeitwa mwekezaji, siku ya kwanza anapewa wali kwa panza…siku ya nne anampa jembe mwenyeji akalime…siku ya 11 anamtimua mwenyeji wake kwa ngumi na mateke kwa msaada wa serikali.

Uwekezaji ni balaa. Wawekezaji wa ndani wamepora viwanja vya maskini bila fidia na wamejigawia viwanja vya shule na zahanati bila wasiwasi. Serikali inakemea mchana huku ikitoa vibali usiku.

Wawekezaji wa nje wanalindwa kwa mitutu ya bunduki katika maeneo waliyopewa kwa nguvu huku wenyeji wao wakiangua kilio cha kusaga meno. Ndiyo maana hata hotuba za Rais Jakaya Kikwete zimechusha kiasi kwamba akihutubia leo, kesho yake hukosolewa mno kutokana na kukosa uhalisia—anasema asiyotenda.

Davos

Hotuba aliyotoa Rais Kikwete alipohudhuria mkutano wa kimataifa uliohusu masuala ya uchumi na uwekezaji Davos, Uswisi ilikuwa na mvuto, msisimko mkubwa na ilionyesha anajali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Rais Kikwete, alitetea na kuwapa matumaini wananchi hasa wakulima juu ya umiliki wa ardhi yao ya kilimo.

Alisema katika mkutano huo wa uzinduzi wa mradi wa kilimo kuwa mashamba wa wakulima wadogowadogo katika maeneo yatakayoteuliwa kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa kilimo hayatachukuliwa na wawekezaji.

Miongozi mwa watu maarufu waliohudhuria mkutano huo walikuwa Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki-Moon na viongozi wa Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF) walioandaa mkutano huo.

Lakini mtu anapotazama hali halisi nchini migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wenyeji, matajiri na maskini, watawala na watawaliwa, anagundua haraka kwamba, hotuba ile ililenga kuwafurahisha wakubwa hao wa kimataifa, basi.

Anapokuwa nje, Rais Kikwete ni mtetezi wa haki, mali, urithi na raslimali za taifa kwa maslahi ya raia lakini anapokuwa nyumbani “Kila mtu na lwake ila Mungu wetu sote”.

Maana migogoro yote mikubwa inayoisumbua serikali ya Chama Cha Mapinduzi, katika kipindi chake chote cha miaka mitano iliyopita, ni wananchi kusukumwa nje ya maeneo yao yenye ardhi kubwa yenye rutuba na madini kupisha wawekezaji katika sekta ya madini na utalii.

Kila kona ya nchi hii ama wafugaji wadogowadogo au wakulima wadogowadogo wanahangaika, wanataabika na wanalia bila msaada wa serikali baada ya mashamba yao au viwanja au nyumba au maeneo ya malisho ya mifugo kuchukuliwa na wawekezaji au matajiri au watawala.

Mifano ipo. Wakati anatoa hotuba hiyo iliyojaa matumaini Uswisi, mamia ya wakulima wadogowadogo wanaoishi vijiji vinne vinavyozunguka Bonde la Kiru, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, walikuwa katika mapambano na mwekezaji wa ndani.

Wakulima hao walichoma moto shamba la Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini, Jitu Son katika mgogoro wa ardhi unaendelea.

Mali nyingine zilizoharibiwa katika vurugu hizo zilizotokea ni mashamba manne ya miwa na matreka 12, magari matatu, nyumba mbili, bohari la vyakula, mapipa 20 ya mafuta ya diseli pipa, mifugo na viwanda viwili ambavyo vimechomwa moto.

Shamba la mbunge huyo lilichomwa moto takriban saa moja tangu, Kamati ya Ulinzi na Usalama iliyokuwa inaongozwa na  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Parceko Vicent Kone, kutembelea  mashamba hayo na kuonya wananchi kutojichukulia sheria mikononi.

Si huko tu, katika eneo la Magugu wilayani humo wakazi wanaoishi kando ya mashamba makubwa ya wawekezaji, eneo la Magugu, walikuwa katika vita ya kugombania mipaka.

Wakulima hao waliharibu mazao kwenye mashamba hayo ya wawekezaji, wakitaka waondoke kwa kuwa wanamiliki maeneo ya kijiji kinyume cha taratibu. Karibu ekari 400 za wawekezaji hao zilizopandwa miwa ziliharibiwa kwa kuchoma moto na maeneo mengine mimea ilikatwakatwa.

Aidha, wakulima wadogowadogo wilayani Kilombero wamekuwa katika mapambano na mwekezaji katika mashamba ya miwa.

Sasa, Rais Kikwete anapowaeleza kina Ban Ki-Moon, Clinton huko Uswisi kwamba mashamba wa wakulima wadogowadogo hayatachukuliwa katika uwekezaji mkubwa, kwa nini hajatatua mgogoro wa maelfu ya wakulima wadogowadogo wanaohangaika nyumbani? Hotuba ile ya kuwafurahisha nani?

North Mara

Hadi mwaka 1995 wakazi wa Nyamongo wilayani Tarime walikuwa wakineemeka kutokana na kazi ya uchimbaji dhahabu walau kwa kutumia nyenzo duni.

Lakini serikali ikapeleka kampuni ya Afrika Mashariki Goldmine (AMGM) ikachukua maeneo ya wachimbaji wadogo bila kulipa fidia. AMGM ikauza hisa zake kwa Placer Dome ambayo pia iliuza hisa zake kwa Barrick.

Rais hajui kwamba kuna mamia ya wakazi wa eneo hilo ambao mashamba yao yalichukuliwa na makampuni hayo bila kulipa fidia na serikali haitaki kusimamia wananchi hao walipwe haki zao? Hotuba nzuri Uswisi ina maana gani kama hakuna utekelezaji nyumbani?

Kiongozi gani wa serikali ya CCM hajui wachimbaji wadogo wa tanzanite wanavyodunguliwa kwa risasi za moto na wawekezaji Mererani?

Kiongozi gani hajui unyama ulivyotumika kuhamisha wakazi wa kata nzima ya Msangaji wilayani Mbarali kwa ajili ya kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Ruaha?

Serikali ililipa fidia ya Sh.60,000 kwa nyumba! Lakini baada ya wananchi kuhama, wakasikia eneo hilo anapewa mwekezaji ili aliendeleze.

Kiongozi gani wa nchi hii asiyejua malalamiko ya ardhi ya wakazi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Geita?

Kwa hiyo, kauli ya Rais Kikwete kwamba inathamini uwepo na mchango wa wakulima wadogowadogo ni ya kuteka hisia za mataifa ya nje, UN pamoja na Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF) walioandaa mkutano huo kwamba serikali inawajali raia kumbe sivyo.

Ni kweli CCM imeshinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010 lakini serikali ya CCM, inavyoendesha nchi imeshindwa kwa kishindo. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imeshindwa kutatua matumizi ya ardhi ya kilimo na uwekezaji katika madini, imewaacha wazawa wakiwa watumwa katika ardhi yao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: