Hugo Chavez: Rais mpenda kuimba, kusali anapohutubia


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Vituko vya Wakubwa

RAIS wa Venezuela , Hugo Chavez ni mwanajeshi wa cheo cha kanali, ingawa aliingia madarakani kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1998. Alichaguliwa tena mwaka 1996 na 2000.
 
Ni miongoni mwa wanajeshi wachache ulimwenguni, walioingia madarakani kwa njia za kidemokrasia. Si hivyo tu, Chavez ni miongoni mwa viongozi wachache duniani ambao waliendelea kutawala nchi zao bila kubadilisha muonekano wake kijeshi. Wengine walikuwa ni Fidel Castro wa Cuba, Jenerali Francisco Franco wa Hispania, Chiang Kaishek wa Taiwan na wengine, hasa kutoka Amerika ya Kusini.
 
Kabla ya kuchaguliwa mwaka 1998 aliwahi kujaribu kutwaa serikali kwa njia ya mapinduzi mwaka 1992, dhidi ya Rais Carlos Andres Perez. Mapinduzi yalishindikana. Inadaiwa kuwa jaribio lilishindwa kutokana na kutoungwa mkono na wanajeshi wengi kwa sababu habari hazikuwafikia mapema.
 
Chavez na wenzake walipokivamia kituo kikuu cha televisheni cha serikali mjini Caracas, walijikuta wamesahau kwenda na hotuba ya Chavez, ya kuwatangazia wananchi kuwa "utawala wa kidhalimu" umekwisha.
 
Badala yake walikamatwa, na yeye akalazimishwa kuutangazia umma, kupitia televisheni hiyohiyo, kwamba mapinduzi yameshindikana na wananchi wote watulie. Hata hivyo aliongeza, bila idhini, maneno yake: "Safari nyingine hakutakuwa na makosa."

Alihukumiwa miaka mitano jela, lakini alipotoka tu alianzisha chama chake na kugombea uchaguzi mwaka 1998.
 
Ushindi wa mwaka 1998 ulitokana na itikadi yake ya mrengo wa kushoto – kama ilivyo kwa nchi nyingine kadha za Amerika ya Kusini, kama vile Nicaragua, Chile, Brazil na Bolivia.

Kwa hiyo, ushindi wake ulitokana na kuungwa mkono na wananchi masikini, hasa wa sehemu za vijijini, ambao walikuwa wamechoshwa na ufisadi wa watawala na kuongezeka kwa kasi pengo kati ya matajiri na masikini.
 
Ikumbukwe kuwa Venezuela ina utajiri mkubwa wa mafuta, ikiwa na akiba ya mapipa bilioni 80. Inazalisha mapipa 2.2 milioni ya mafuta yasiyosafishwa kwa siku.
 
Ni ya sita duniani katika kusafirisha mafuta nchi za nje baada ya Saudi Arabia, Iran, Indonesia, Iraq na Nigeria. Marekani huagiza kutoka Venezuela asilimia 60 ya mahitaji yake ya mafuta kutoka nje. Hizi ni takwimu za mwaka 2007.
 
Hili la Marekani kununua asilimia 60 ya mahitaji yake ya mafuta kutoka Venezuela halikai vizuri, hasa kutokana na uhusiano mbaya uliopo kati ya nchi hizo mbili, unaodumishwa na sera za Chavez.
 
Uhusiano wa Chavez na Marekani ni sawa na ule wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi na Marekani. Viongozi hawa hutumia fedha nyingi kutokana na utajiri wa mafuta katika kuziwekea ngumu sera za Marekani kwa nchi za nje.
 
Sera za Marekani kwa nchi za Amerika ya Kusini, jirani na Venezuela, zimesababisha ushindani mkubwa kati ya mataifa hayo mawili. Kila nchi inataka kuzivuta baadhi ya nchi hizo kuwa upande wake.
 
Chavez ana ushawishi mkubwa kwa nchi kama vile Cuba, Bolivia, Nicaragua, Brazil na Chile. Amekuwa akitoa misaada mikubwa ya kiuchumi kwa nchi hizo ili kuipiku Marekani.
 
Marekani, kwa upande wake, imefanikiwa "kuziteka" Colombia, Honduras, Guatemala na kidogo Argentina. Lakini Chavez amevuka mipaka ya sehemu yake ya dunia na kufanikiwa kuungwa mkono, kwa kiasi kikubwa, na nchi kama Urusi, Iran, China, Libya na Syria.
 
Hivi karibuni alifanya ziara katika  baadhi ya nchi hizo. Aliiunga mkono Iran na kuiahidi kuiuzia mafuta iwapo Marekani itajaribu kuiwekea vikwazo kutokana na mradi wake wa nyuklia. Kule Urusi, Chavez aliwaunga mkono akina Putin kwa kuyatambua majimbo ya Georgia yaliyojitenga, ya Abkhazia na Ossetia ya Kusini.
 
Alisafiri hadi Tripoli, Libya, kuhudhuria sherehe za miaka 40 ya utawala wa Gaddafi ambako picha za televisheni zilimuonyesha akishiriki katika nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na vikundi mbali mbali, za kuyatukuza mapinduzi ya mwaka 1969.
 
Mwaka 2005 na 2006 jarida maarufu la TIME lilimtaja Chavez kuwa ni miongoni mwa watu 100 duniani wenye ushawishi mkubwa.
 
Lakini tukiachia masuala hayo, Chavez anajulikana sana kwa staili yake ya utawala. Hupendelea kuwahutubia wananchi wake kwa njia ya televisheni kila wiki, ambapo hututumia fursa hiyo kuimba na kufanya maombi.
 
Wakati rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro, ambaye ni rafiki mkubwa wa Chavez, alipokuwa anaumwa, Chavez alikwenda Havana kumjulia hali.

Katika mkutano na waandishi wa habari ghafla alianza kuimba na kumuombea Castro apate nafuu kwa haraka, huku akiwashawishi waandishi wa habari nao waitikie kwa sauti kubwa.
 
Mwaka 2008, alikwenda Hispania kwa ajili ya mkutano kati ya nchi hiyo na nchi za Amerika ya Kusini, zilizokuwa zinatawaliwa na Hispania. Wakati Waziri Mkuu wa Hispania, Jose Luis Zapatero, alipokuwa akihutubia, Chavez aliyeketi umbali wa mita chache alisikika akimkatiza mara kwa mara kwa maneno ya kejeli, hadi Mfalme Juan Carlos wa nchi hiyo akamgeukia Chavez na kufoka kwa sauti kubwa: "Kwa nini hunyamazi?"
 
Mara tu baada ya tukio hilo, huko Hispania na Marekani, baadhi ya maadui zake walivaa fulana zenye picha ya Chavez, akiwa amevaa kofia yake ya beret. Fulana hizo zilikuwa na maandishi: "Kwa nini hunyamazi?" 
 
Baadhi yao waliweka miito ya sauti katika simu zao za mikononi iliyokuwa na sauti ya Mfalme Carlos, ikisema hivyo hivyo: "Kwa nini hunyamazi?"
 
Ni katika ziara hiyohiyo huko Hispania, Chavez aliwasumbua wenyeji wake kumpeleka katika duka moja la vitabu mjini Madrid, ambako alisikia kinauzwa kitabu kimoja kiitwacho: "Mazishi ya ubepari."
 
Hiyo ilikuwa wakati wa mwanzo wa kuanguka kwa mabenki na makampuni makubwa huko Marekani na nchi nyingine za Magharibi. Matukio hayo yalisukuma uchumi wa dunia kuathirika vibaya.
 
Katika ziara yake ya Hispania hivi karibuni, Chavez alionana tena na Mfalme Carlos. Alishangaa kumkuta Mfalme huyo kafuga ndevu.  Baada ya kuamkiana akamwambia: "Unafanana sana na rafiki yangu Fidel Castro."
 

0
No votes yet